Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA77

MKUTANO WA 77 WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Pata habari kutoka UNGA77

Mambo sasa yameiva kwa ajili ya Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Wakati dunia inaanza taratibu kujikwamua kutoka katika janga baya kabisa la COVID-19, mjadala wa ngazi ya juu wa mkutano wa 77 kwa kiasi kikubwa utafanyika kwa viongozi kuweko kwenye ukumbi mashuhuri wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, tofauti ya miaka miwili iliyopita ambapo viongozi wengine walikuweko ukumbini na wengine walitoa hotuba zao kwa njia ya video. 
 
Katika ukurasa huu, Habari za UN itakupatia kiti cha mbele kabisa kutoka kwenye kumbi zote. Kupitia simu yako ya kiganjani au rununu bila kusahau kompyuta yako au kishkwambi, utafuatilia hotuba za wakuu wa nchi na serikali wakati wakitoa ainisho au majawabu ya changamoto zinazokabili Dunia hivi sasa, sambamba na wanavyoshiriki katika mkutano wa ngazi ya juu wa Marekebisho ya Mfumo wa Elimu, kushughulikia janga la chakula duniani, maadhimisho ya miaka 30 ya Azimio la UN kuhusu haki za watu wa makabila madogo halikadhalika mzozo wa Ukraine.

Rambaza kwenye majukwaa yetu ya mitando ya kijamii

Twitter: Habari za UN
Youtube: Habari za UN

Csaba Kőrösi  Rais wa UNGA77 akiendesha mjadala wa wazi wa Baraza Kuu katika siku ya mwisho ya mjadala huo
UN Photo/Cia Pak

Körösi, akunja jamvi la mjadala wa ngazi ya juu wa UNGA77

Magari yaliyotanda kuzunguka makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuhakikisha usalama wakati wa wiki ya mjadala wa ngazi ya juu wa viongozi kwenye Baraza Kuu UNGA77 sasa yameondoka na barabara iliyofungwa kufunguliwa, polisi wengi na maafisa wa ujasusi ambao walizuia njia za kuelekea kwenye jengo la Umoja wa Mataifa, nao wametrejea kwenye majukumu yao ya kila siku, kilomita za vyuma vilivyokuwa vizuizi kuzunguka eneo hilo la Umoja wa Mataifa New York, vinavyojulikana kama Turtle Bay navyo vimesafirishwa kwa malori hadi kwenye maghala kusubiri hadi mwakani kwani wiki ya mjadala wa ngazi ya juu imemalizika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  .