Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ni jawabu la amani na usalama duniani- Guterres

Nargiz Shekinskaya wa UN News akimhoji Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.
UN /Mark Garten
Nargiz Shekinskaya wa UN News akimhoji Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

Elimu ni jawabu la amani na usalama duniani- Guterres

Utamaduni na Elimu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema iwapo angalipatiwa fursa ya kuchagua kitu kimoja ili kuboresha hali ya dunia hivi sasa, ikiwemo amani na usalama, kitu hicho kingalikuwa ni elimu.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kuelekea kuanza kwa mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa kesho jumanne, Guterres amesema“kama ningalitakiwa kuchagua kitu kimoja kuimarisha hali ya dunia, amani na usalama, kuimarisha uelewa wa tabianchi na hatua kwa tabianchi, hilo lingalikuwa elimu.”

Elimu bora itapunguza ukosefu wa usawa duniani

Amesema anapoangalia chochote ambacho kingalipunguza ukosefu wa usawa duniani, kitu hicho ni elimu. Kwa hiyo mkutano wa viongozi kuhusu marekebisho ya elimu ni wakati wa kuhamasisha jamii nzima ya kimataifa, kufanya nchi kutambua kuwa lazima ziwekeze zaidi kwenye elimu.

Halikadhalika amesema mkutano huo ufanye nchi zilizoendelea zitambue wajibu wao na taasisi za kifedha kusaidia nchi zinazoendelea ili ziwezeke kwenye elimu.

Ajenda ya Pamoja ndio suluhu

Alipoulizwa ni marekebisho yapi makubwa ya kimuundo ambayo angalipenda kufanya wakati wa uongozi wake, Katibu Mkuu amesema cha msingi ni kuona kila nchi inatekeleza Ajenda ya Pamoja ambayo ni msururu wa miradi, ikiwa na mawazo yote yenye lengo la kuhakikisha Umoja wa Mataifa ni fanisi na wakati huo huo ushirikiano wa kimataifa unakuwa wa tija.

Vijana wanaoshiriki mkutano wa siku tatu wa marekebisho ya elimu duniani, mkutano unaofanyika kwenye makao makuu ya UN jijini New York, MArekani
UN News/Abdelmonem Makki
Vijana wanaoshiriki mkutano wa siku tatu wa marekebisho ya elimu duniani, mkutano unaofanyika kwenye makao makuu ya UN jijini New York, MArekani

Wapitisha maamuzi wameweka pembeni hoja ya mabadiliko ya tabianchi

Na kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu amesema, kwa sasa yaonekana wapitisha maamuzi katika baadhi ya nchi hawapatii kipaumbele kutokana na changamoto nyingine duniani ikiwemo vita ya Ukraine na utoaji wa hewa chafuzi umeongezeka.

Kwa hivyo amesema ”tunahitaji kuongeza usaidizi kwa kuweka uhimili, kwa kujenga miunndombinu endelevu ambayo ni muhimu kwa hizo nchi kukabiliana na madhara ambayo tayari yanaleta changamoto, wakati huu ambapo athari zinakwenda kwa maeneo ambayo mengi yao duniani kwa kiasi kikubwa hayachangii kwa kiasi kikubwa katika madhara ya mabadiliko ya tabianchi duniani.”

 

Mjini Istanbul, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaangalia meli ya WFP SSI Invincible 2, ikielekea Ukraine kuchukua shehena kubwa zaidi ya nafaka ambayo bado inasafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.
UN Photo/Mark Garten
Mjini Istanbul, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaangalia meli ya WFP SSI Invincible 2, ikielekea Ukraine kuchukua shehena kubwa zaidi ya nafaka ambayo bado inasafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

Diplomasia ya tahadhari na mafanikio yake

Kuhusu siasa zenye mwelekeo wa kimaeneo au kijiografia, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa diplomasia ya tahadhari na makinifu inavyoweza kuleta mabadiliko dhahiri kwenye masuala magumu, ikiwemo uhaba wa chakula duniani ambao umechochewa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Akitumia mfano wa Makubaliano ya usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi uliotiwa saini mwezi Julai mwaka huu, Katibu Mkuu amesema, mkataba umeonesha kuwa diplomasia makinifu bado ina uwezo wa kufanikisha kile ambacho diplomasia ya ‘makelele” haiwezi.”

Amesema mkataba huo usingaliwezekana iwapo hatukufanya kazi bila kukata tamaa na kwa utashi, tukiepuka kuunda mazingira ambamo kwayo pande zote husika zingalianza kuvurugana.

Katibu Mkuu amesema kwa mtazamo wake, kilichofanyika kufanikisha mkataba huo, kinaweza kuwa ndio mwongozo katika kutatua majanga mengi duniani. “Hebu tufanye kila liwezekanalo kuanzisha upya umuhimu wa diplomasia makinifu katika kutatua majanga ya sasa duniani.

Ukosefu wa uwezo wa kifedha na kupata chanjo unakwamisha maendeleo ya uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea
ILO/K.B. Mpofu
Ukosefu wa uwezo wa kifedha na kupata chanjo unakwamisha maendeleo ya uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea

COVID-19 na nini kifanyike

Alipoulizwa kuhusu nini kifanyike ili afya ya umma ipatiwe kipaumbele kwenye ajenda za serikali kama njia mojawapo ya kuhimili majanga ya kiafya kama janga la COVID-19, Katibu Mkuu amesema jambo muhimu kwanza ni kupatia jawabu suala la chanjo kwenye maeneo ambako bado ni tatizo.

“Na hili ni jambo ambalo mfumo wa Umoja wa Mataifa unahamasisha. Pili; ni muhimu sana kupatia msamaha wa madeni nchi ambazo ziliathirika na karantini wakati wa COVID-19 ili hatimaye ziweze kujikwamua.”

Amerejelea kauli yake ya kustaajabishwa na kitendo cha nchi tajiri kuchapisha matrilioni ya fedha ili kuchechemua uchumi wao, huku nchi zinazoendelea zikishindwa kufanya hivyo kwa kuwa zikifanya hivyo thamani ya sarafu zao itaporomoka. Kwa hiyo ametaka kuanzishwa tena kwa mshikamano wa kimataifa.