Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA77

MKUTANO WA 77 WA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Pata habari kutoka UNGA77

Mambo sasa yameiva kwa ajili ya Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Wakati dunia inaanza taratibu kujikwamua kutoka katika janga baya kabisa la COVID-19, mjadala wa ngazi ya juu wa mkutano wa 77 kwa kiasi kikubwa utafanyika kwa viongozi kuweko kwenye ukumbi mashuhuri wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, tofauti ya miaka miwili iliyopita ambapo viongozi wengine walikuweko ukumbini na wengine walitoa hotuba zao kwa njia ya video. 
 
Katika ukurasa huu, Habari za UN itakupatia kiti cha mbele kabisa kutoka kwenye kumbi zote. Kupitia simu yako ya kiganjani au rununu bila kusahau kompyuta yako au kishkwambi, utafuatilia hotuba za wakuu wa nchi na serikali wakati wakitoa ainisho au majawabu ya changamoto zinazokabili Dunia hivi sasa, sambamba na wanavyoshiriki katika mkutano wa ngazi ya juu wa Marekebisho ya Mfumo wa Elimu, kushughulikia janga la chakula duniani, maadhimisho ya miaka 30 ya Azimio la UN kuhusu haki za watu wa makabila madogo halikadhalika mzozo wa Ukraine.

Rambaza kwenye majukwaa yetu ya mitando ya kijamii

Twitter: Habari za UN
Youtube: Habari za UN

20 SEPTEMBA 2022

Hii leo katika Habari za UN Flora Nducha anakuletea jarida likianza na Habari kwa Ufupi ikianza na ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu Antonio Guterres akitaka ubia wa kimataifa kukabili mgawanyiko unaozidi kushamiri kila uchao. Kisha Rais wa Brazil  na kwingineko kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola aina ya Sudan nchini Uganda.

Mada kwa kina ni kuhusu kijana mkimbizi anayesoma Canada ambaye amenuia kuwasaidia wenzake aliowaacha katika kambi za Kakuma na Dadaab nchini Kenya.

Sauti
12'23"
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia ufunguzi wa mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN
UN /Cia Pak

Tunahitaji ubia wa dunia wakati huu ambao mgawanyiko unazidi- Guterres

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeanza hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amezungumza wakati wa ufunguzi akigusia masuala lukiki ikiwemo mgawanyiko wa kisiasa na kijiografia duniani, mizozo, uhaba wa chakula, ongezeko la gharama ya maisha, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia akisema maendeleo yaliyofikiwa katika Nyanja mbali mbali yanakwamishwa na mgawanyiko wa kisiasa na kijiografia.