Burkina Faso imejiwekea mpango wa kurejesha utulivu – Rais Damiba

Rais Paul Herni Sandaogo Damiba wa Burkina Faso akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN /Cia Pak
Rais Paul Herni Sandaogo Damiba wa Burkina Faso akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Burkina Faso imejiwekea mpango wa kurejesha utulivu – Rais Damiba

Masuala ya UM

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 ukiwa umeingia siku ya nne hii leo, Rais Paul Damiba wa Burkina Faso amesema tayari wamejiwekea mpango mkakati wa kurejesha utulivu nchini mwake wakati huu ambapo anaongoza serikali ya mpito kuanzia kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Januari mwaka huu.

Rais Damiba amesema hali ya usalama Burkina Faso alianza kuzorota mwaka 2015 na kilele kufikia mwaka 2020/2021 hali iliyosababisha changamoto kama vile ukimbizi wa ndani, kutwama kwa shughuli za kiuchumi.

Hata hivyo amesema wameandaa mpango mkakati kukabili hali hiyo.

Mkakati huo ni “mosi kukabilia ugaidi na kulinda mipaka yetu, pili, kukabili janga la kibinadamu, kurekebisha serikali yetu na kuimarisha utawala bora, na mwisho maridhiano ya kitaifa na utangamano wa kijamii.”

Na ili kutekeleza mkakati huo, Rais huyo wa Burkina Faso amesema serikali ya mpito imechukua hatua kama vile, Mosi kupanga upya mfumo wa ulinzi wa taifa na hatua thabiti mashinani dhidi ya ugaidi na vikundi vilivyojihami. Pili kukabili misimamo mikali, kauli za chuki na unyanyapaa wa baadhi ya jamii, ujumuishaji kwenye jamii kwa wapiganaji wa zamani, na usaidizi wa kujumuisha upya kijamii na kiuchumi waathirika wa matukio ya ugaidi.”

Amesema hatua nyingine ni kutokomeza rushwa, kuendeleza haki na uwiano pamoja na elimu kuhusu uraia na amani.

Elimu inaonekana kama suluhisho muhimu kwa migogoro mingi katika Sahel.
© UNICEF/Seyba Keïta
Elimu inaonekana kama suluhisho muhimu kwa migogoro mingi katika Sahel.

 

Ukanda wa Sahel

Akizungumzia utulivu, amani na usalama kwenye ukanda wa Sahel, Rais Damiba amesema si suala la nchi zilizo eneo hilo peke yake kwa kuwa  hali katika nchi za ukanda huo ni matokeo ya uhamiaji wa magaidi kutoka kaskazini kwenye kusini mwa bara la AFrika.

“Uvukaji mipaka unahatarisha amani na usalama duniani. Hivyo ni muhimu wa jamii ya kimataifa kutambua hilo na kupatia suluhu. Hatua zilizochukuliwa hadi sasa zinapongezwa lakini hazikidhi mahitaji na mazingira ya sasa,” amesema Rais Damiba.

Ametumia hotuba hiyo kupongeza hatua ya Rais wa Muungano wa Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kumteua Rais Mahamoudou Issoufou wa Niger kuongoza tathmini ya mkakati  kati ya AU na UN kwenye ukanda wa Sahel.

Amesema ujumbe huo usaidie kuandaa mapendekezo ya jinsi ya kuimarisha hatua za kimataifa kwenye janga la usalama ukanda wa Sahel.