Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA 77 kumulika majawabu ya kuleta marekebisho ya changamoto duniani

Abdulla Shahid Rais wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 akikabidhi nyundo ya mwenyekiti, kwa Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 Csaba Kőrösi. Kushoto ni Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres.
UN/ Evan Schneider
Abdulla Shahid Rais wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA76 akikabidhi nyundo ya mwenyekiti, kwa Rais wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 Csaba Kőrösi. Kushoto ni Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres.

UNGA 77 kumulika majawabu ya kuleta marekebisho ya changamoto duniani

Masuala ya UM

Csaba Kőrösi raia wa Hungary leo ameapishwa kuwa Rais wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akibainisha kuwa kipindi chake cha uongozi kitamulika majawabu ya changamoto kupitia mshikamano, uendelevu na sayansi.
 

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini New York, Marekani baada ya kuapishwa, Bwana Kőrösi ametumia pia fursa hiyo kutangaza maudhui ya mjadala mkuu wa mkutano wa ngazi ya juu kuw ani “Wakati muhimu: Majawabu ya kuleta marekebisho kwa changamoto zinazofungamana.”

Marekebisho ya jamii ya kimataifa na UN- Kőrösi

Ameeleza kuwa jamii ya kimataifa lazima iendelee kujirekebisha, sambamba na kurekebisha Umoja wa Mataifa, likiwemo Baraza Kuu sambamba na “kuimarisha ushirikiano wetu kupitia kuaminiana.”

Tukio la kuapishwa kwa Bwana Kőrösi lilitanguliwa na kufungwa kwa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, tukio ambalo lilitoa fursa pia kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuhutubia wajumbe.

“Miezi 12 iliyopita imeakumbwa na mfululizo wa changamoto kubwa. Ongezeko la bei ya bidhaa, kudorora kwa uwezo wa watu kununua bidhaa, ongezeko la ukosefu wa uhakika wa mtu kupata chakula, na kiza kinene kinachotanda kwenye mfumuko wa bei,” amesema Katibu Mkuu.

Changamoto nyingine amesema ni dharura ya kiafya iliyoibuka ya ugonjwa wa ndui ya nyani au Monkeypox, mafuriko, joto kali, vimbunga na majanga mengine ya asili.

Katibu Mkuu ametaja pia hali ya dharura nchini Pakistani ambako katika ziara yake ya mwishoni mwa wiki ameshuhudia akisema, “ ni jambo ambalo si la kufikirika kuona eneo ambalo ni mara tatu ya ukumbwa wa nchi yangu ya Ureno, limefurika, na machungu ambayo watu wanapitia.

Csaba Kőrösi, Rais wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa mkutano wa 76, (UNGA 76)
UN/ Manuel Elias
Csaba Kőrösi, Rais wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA 77 akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungwa kwa mkutano wa 76, (UNGA 76)

Mkutano wa UNGA 77 ni jaribio kwa ushirikiano wa kimataifa- Guterres

Kwa Katibu Mkuu Guterres, mkutano wa UNGA 77 utakuwa ni mtihani kuliko wakati wowote ule kwa ushirikiano wa kimataifa .

“Mkutano huu utaendelea kupima mshikamano na kuaminiana baina ya mataifa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa mwelekeo una changamoto na hautabiriki.

Hata hivyo amesema kwa kutumia “mbinu tulizonazo—yaani Diplomasia, mashauriano na maafakiano, tunaweza kuendelea kusaidia watu na jamii duniani kote. Tunaweza kufungua njia bora na mustakabali wenye amani zaidi kwa watu wote.”

Rais wa UNGA 76 naye atoa neno

Ikiwa ni kikao chake cha mwisho kama Rais wa Baraza Kuu, Abdulla Shahid amehutubia akisema aliahidi Urais wa Matumaini uliojengwa kwenye miali mitano ya matumaini: Kuibuka kutoka COVID-19, Kujikwamua kiendelevu, Kujibu mahitaji ya sayari dunia, kuheshimu haki za binadamu na kuchechemua Umoja wa Mataifa.

Akihitimisha amesema “katika kila siku ya siku 365 zilizopita, mimi na timu yangu tulifanya kazi kufanikisha dira hiyo. Tulikuwa na vikao 103 vya wazi, tulipitisha maazimio 307 na maamuzi 140.”