Umoja wa Mataifa ni nyumba ya ushirikiano na Baraza Kuu ni Maisha ndani ya nyumba hii: Guterres

13 Septemba 2022

Kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA77 kimefunguliwa rasmi hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezikumbusha nchi wanachama kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu za changamoto zinazoikabili dunia kwa ushirikiano.

Guterres pamoja na kumshukuru Rais wa Baraza la 76 kwa uongozi wake wa kipindi cha mwaka mmoja ameeleza kuwa changamoto zilizokuwa zinashughulikiwa bado hazijaisha na hivyo dunia bado inakabiliwa na hatari katika kuendeleza amani haki za binadamu na maendeleo endelevu.

Guterres amesema changamoto hizo ni kuanzia kwenye “Mabadiliko ya tabianchi, kuanguko kwa mfumo wa kifedha wa kimataifa nakuathiri zaidi nchi zinazoendelea, umasikini, ukosefu wa usawa, njaa, mgawanyiko mpaka kutoaminiana.”

Mkuu huyo wa umoja wa Mataifa ameeleza ili kushughulikia changamoto zote hizo na nyingine nyingi katika kikao cha 77 cha Baraza kuu lililoanza rasmi hii leo kunahitajika mshikamano endelevu wakati wa kushughulikia changamoto zinazoingiliana na kueleza kuwa wapo sehemu sahihi kuonesha ushirikiano kwakuwa “Umoja wa Mataifa ni nyumba ya ushirikiano na Mkutano wa Baraza Kuu ni Maisha ndani ya nyumba hiyo” na kwamba wajumbe wa Baraza hilo “wanawakilisha moyo unaodunda wa ushirikiano wa Kimataifa”

Amewaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa dunia nzima inawatazama wao kuhakikisha wanatumia zana zote walizonazo katika kujadiliana na kubuni suluhu zote na rasilimali walizonazo kwa njia ya mijadala na kidiplomasia. 

Csaba Kőrösi, Rais wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akihutubia mkutano wa kwanza wa kikao hicho.
UN Photo/Evan Schneider
Csaba Kőrösi, Rais wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, akihutubia mkutano wa kwanza wa kikao hicho.

Milango ya ushirikiano ipo wazi 

Kwa upande wake Rais wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu Csaba Kőrösi, amesema anafuraha kuwa amepokea wadhifa huo wakatia ambapo Rais wa 76 Abdulla Shahid amefanikisha mambo kadhaa ikiwemo kuunda ofisi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa na kwamba uongozi wake utaendelea kufanya akzi kuhakikisha unafuatilia ripoti ya Ajenda Yetu ya Pamoja. 

Rais huyo wa UNGA77 amezungumzia umuhimu wa kushirikiana na kusema pamoja na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Uchumi na Kijamii pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ameahidi pia kufanya kazi sambamba na asasi za kiraia kwakuwa wana ujuzi wa masuala mengi ya mashinani. 

“Ninakusudia kuendeleza mchakato muhimu wa uhuishaji, pamoja na kutekeleza mageuzi muhimu yanayoendelea hivi sasa ambayo yanaongozwa na Katibu Mkuu, kufanya Baraza Kuu na Umoja wa Mataifa kuendana na maudhui yanayolingana.”

Ameeleza pamoja na kushirikiana na serikali katika kufanya maamuzi mengi lakini serikali hazina hatimiliki za mawazo mazuri peke yake na hivuo nilazima kuvuka kuta za Umoja wa Mataifa na kusaka ushauri kwa wengine.

“Tunapofanya kazi lazima tushirikiane na washirika wetu wa mashirika ya kiraia, wasomi, sekta binafsi, kuwezesha watafiti na watendaji kutupatia ufumbuzu ambao umejikita katika ukweli, kuwa na taarifa sahihi na zilizothibitishwa na sayansi.”

Ameeleza pia katika ulimwengu unaoendelea kupona kutokana na changamoto mbalimbali zinazoukabili ulimwengu ni vyema watu wote kushirikiana hata pale kunapokuwa na changamoto ya kijiografia kwakuwa hata Umoja wa Mataifa ulianzishwa katikati ya vuguvugu duniani. 

“Umoja wa Mataifa uliundwa kutoka kwenye majivu ya vita na uharibifu nia ikiwa kuwa kisima cha utatuzi kujibu changamoto kubwa za wanadamu ambao wanataka kufanya kazi pamoja na kwamba sisi tunaweka nguvu mpya kwenye umoja, ushirikiano mzuri wa pande nyingi na kuzingatia kile kinachotuunganisha.” 

Amehitimisha hotuba yake kwa kukumbusha kuwa dhamira yao ni kujumuika pamoja kunapokuwa na kutoelewana na kujenga madaraja wakati kuna kina kirefu cha mgawanyiko. “Ukumbi huu uliundwa kama mahali pa kujenga uaminifu, kuleta amani na usalama, maendeleo na haki za binadamu. Tuna deni kwa wapiga kura wetu bilioni 8, watu ambao tuko hapa kuwahudumia, kufanikiwa katika malengo yetu”. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter