Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 3 duniani kote ndiye awezaye kusoma na kuelewa hadithi fupi na hali si shwari - UNICEF

Taswira wa darasa la mfano linalolenga kuonesha Mgogoro wa kujifunza duniani. Darasa hili lililoandaliwa na UNICEF liko makao makuu ya UN jijini New York, Marekani.
© UNICEF/Chris Farber
Taswira wa darasa la mfano linalolenga kuonesha Mgogoro wa kujifunza duniani. Darasa hili lililoandaliwa na UNICEF liko makao makuu ya UN jijini New York, Marekani.

Mtoto 1 kati ya 3 duniani kote ndiye awezaye kusoma na kuelewa hadithi fupi na hali si shwari - UNICEF

Utamaduni na Elimu

Mkutano wa Ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu duniani ukianza leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limetoa taarifa inayoeleza idadi ya Watoto wasiojua kusoma imeongezeka ulimwenguni ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita. 

Anold Kayanda
Watoto wasiojua kusoma wameongezeka duniani - UNICEF

Jijini New York, Marekani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, UNICEF wameweka mfano wa darasa kando mwa bustani ya mawaridi, darasa hili linaitwa “Darasa la Mgogoro wa kujifunza”, lengo ni kufikisha ujumbe wa changamoto ya elimu duniani hivi sasa.

Darasa hilo limewekwa ubao na madawati lakini theluthi moja ya madawati hayo yametengenezwa kwa mbao na kuwekwa mabegi ya mgongoni ikiwakilisha theluthi moja ya Watoto wenye umri wa miaka 10 wanaokadiriwa kuwa na uwezo wa kusoma na kuelewa ulimwenguni.

Mtoto 1 kati ya 3 mwenye umri wa miaka 10 duniani kote ndiye anayeweza kusoma hadithi rahisi- Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji UNICEF

Kabla ya Janga la COVID-19 miaka miwili iliyopita watoto waliojua kusoma wenye umri wa miaka 10 ulimwenguni walikuwa nusu lakini sasa UNICEF linasema idadi yao ni theluthi moja hii ikiwa sawa na mtoto mmoja kati ya watatu ndio mwenye uwezo wa kusoma na kuelewa hadithi fupi.

Walimu wasio na uwezo wanaajiriwa kufundisha watoto

Katika taarifa yake iliyotolewa jijini New York Marekani Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell ameeleza sababu za kuporomoka kwa uwezo wa Watoto kujua kusoma ni shule zilifungwa muda mrefu kipindi cha janga la CORONA na kuwaacha mamilioni ya Watoto bila ujuzi wa msingi wa kusoma na kuhesabu, elimu haikuwa bora na kufichua mapungufu mengi ndio maana idadi ya Watoto wasiojua kusoma na kuhesabu imeongezeka kwa kiwango cha kushtusha na kuonya hii ni hatari kwa Maisha ya baadae ya watu wote duniani.

Wanafunzi wakiwa darasani wakisoma hesabu huko shule ya msingi ya Soanierana nchini Madagascar
© UNICEF/Rindra Ramasomanana
Wanafunzi wakiwa darasani wakisoma hesabu huko shule ya msingi ya Soanierana nchini Madagascar

Tupandacho sasa kwenye elimu ndio kivuno chetu cha baadaye

Taarifa hiyo imemnukuu Bi Russell akisema “mifumo yetu ya elimu ndio mwelekeo wa maisha yetu ya baadaye. Tunahitaji kubadili mwelekeo wa sasa au itatubidi kukabiliana na matokeo ya kushindwa kuelimisha kizazi chote. Viwango vya chini vya kujifunza vya leo inamaanisha fursa ndogo kesho.”

Wakati viongozi wakikutana katika Mkutano wa marekebisho ya mfumo wa elimu UNICEF imetoa wito kwa serikali kujitolea kuwafikisha Watoto elimu bora kwa kuongeza uwekezaji kwenye elimu, kuweka mazingira salama ya kujifunzia, kuandikisha Watoto wengi shule na kuboresha maslahi ya walimu.

Ujiwa wa walimu unakatisha tamaa

Mkuu huyo wa UNICEF amesema hali ya sasa ni mbaya “shule hazina rasilimali, walimu wanalipwa ujira mdogo, walimu wengine wasio na sifa wanaajiriwa, msongamano wa wanafunzi madarasani, mitaala ya kizamani na vyote hivi vinasababisha Watoto kushindwa kufikia uwezo wa juu wa ufaulu.”