Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Körösi, akunja jamvi la mjadala wa ngazi ya juu wa UNGA77

Csaba Kőrösi  Rais wa UNGA77 akiendesha mjadala wa wazi wa Baraza Kuu katika siku ya mwisho ya mjadala huo
UN Photo/Cia Pak
Csaba Kőrösi Rais wa UNGA77 akiendesha mjadala wa wazi wa Baraza Kuu katika siku ya mwisho ya mjadala huo

Körösi, akunja jamvi la mjadala wa ngazi ya juu wa UNGA77

Masuala ya UM

Magari yaliyotanda kuzunguka makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuhakikisha usalama wakati wa wiki ya mjadala wa ngazi ya juu wa viongozi kwenye Baraza Kuu UNGA77 sasa yameondoka na barabara iliyofungwa kufunguliwa, polisi wengi na maafisa wa ujasusi ambao walizuia njia za kuelekea kwenye jengo la Umoja wa Mataifa, nao wametrejea kwenye majukumu yao ya kila siku, kilomita za vyuma vilivyokuwa vizuizi kuzunguka eneo hilo la Umoja wa Mataifa New York, vinavyojulikana kama Turtle Bay navyo vimesafirishwa kwa malori hadi kwenye maghala kusubiri hadi mwakani kwani wiki ya mjadala wa ngazi ya juu imemalizika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  .

Sasa kwa vile wajumbe wengi tayari wamerejea katika nchi zao, ni wakati wa kutathmini pengine kipindi hiki chenye pilika nyingi zaidi katika kalenda ya Umoja wa Mataifa. 

Kila mwaka katika nusu ya pili ya mwezi Septemba, New York inakuwa kitovu cha kivutio cha wale wanaopenda siasa za kimataifa, kwa sababu ni hapa ambapo wakuu wa nchi na serikali, mawaziri na wanadiplomasia wa karibu nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa hukutana.

Katika siku ya mwisho ya mjadala huo wa ngazi ya juu, Mwenyekiti wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu, Rais wa Baraza hilo ambaye ni mwanadiplomasia wa nguli kutoka Hungary Csaba Körösi, alitoa muhtasari wa majadiliano yaliyokuwa yakiendelea kwa siku sita mfululizo katika ukumbi huo maarufu duniani.

Msanii Eduardo Kobra na timu yake wakikamilisha mchoro knje ya ukuta wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Mastaifa New York wakati wa kuanza kwa mjadala wa UNGA77
UN News/Matthew Wells
Msanii Eduardo Kobra na timu yake wakikamilisha mchoro knje ya ukuta wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Mastaifa New York wakati wa kuanza kwa mjadala wa UNGA77

Takwimu katika wiki ya mjadala wa wazi

Kwa hiyo mwenyekiti wa UNGA77 na Rais wa Baraza Kuu amehisi wiki hii ilikuwaje? Wacha tuanze na takwimu.

Katika kikao cha kufunga mjadala wa Baraza Kuu, Körösi ametaja takwimu zifuatazo.

Mjadala mkuu wa wazi wa mwaka huu ulihudhuriwa na wazungumzaji 190 wakiwemo wakuu wa nchi 76, wakuu wa serikali 50, makamu wa Rais 4, manaibu waziri mkuu 5, mawaziri 48 na wajumbe wawakilishi 7. 

Mwenyekiti amesema katiuka mjadala huo kulikuwa na wanawake 23 kati ya wazungumzaji. 

Na ingawa kulingana na Rais huyo wa Baraza Kuu, wanawake hao ni zaidi ya asilimia 10 tu ya orodha nzima ya wazungumzaji, jukumu la wanawake katika siasa za ulimwengu haliwezi kutotiliwa maanani.

Wafanyakazi wengi wa sekretarieti ya Umoja wa Mataifa walifanya kazi kwa juhudi zote ili kuhakikisha wiki ya mjadala wa ngazi ya juu inakuwa ya mafanikio, wakiwemo wataalamu wa kiufundi, watafsiri, maafisa wa itifaki na usalama na Csaba Körösi ametoa shukrani zake za dhati kwa wote.

Nini kilichosemwa kwenye mimbari ya Baraza hilo

Mwenyekiti wa Baraza Kuu amejaribu kufanya majumuisho ya mada ambazo wviongozi wanachama wa Umoja wa Mataifa waligusia katika hotuba zao. Ameorodhesha tathimini yake katyika masuala haya matano.

Kwanza, Csaba Körösi amebaini kuwa kuna ufahamu unaoendelea kukua miongoni mwa washiriki katika majadala huo kwamba ubinadamu umeingia katika zama mpya. 

Amesema “Ubinadamu huo unakabiliwa na changamoto mtambuka na ngumu na migogoro ya ngazi mbalimbali, watu wamejikuta katika mabadiliko ya dhana, wakati taratibu na mabadiliko yanayotokea karibu nasi hayawezi kuitwa tena marekebisho rahisi. Tunazungumzia juu ya mabadiliko makubwa katika ulimwengu.”

Ameongeza kuwa "Bado hatuna jina la enzi hizi mpya, bado hatuwezi kuelezea kwa lugha ya kisayansi, lakini tunahisi wazi kuwa yamekuja.”

Taswira ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Katibu Mkuu António Guterres alipohutubia ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa UNGA77
UN /Cia Pak
Taswira ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Katibu Mkuu António Guterres alipohutubia ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa UNGA77

Mwenyekiti huyo wa UNGA77 ameseendelea kusema kwamba "Masharti ya misingi ya ushirikiano wetu wa kimataifa yamebadilika. Tunaishi sasa katika ulimwengu tofauti. Ulimwengu wenye changamoto mpya, vipaumbele vilivyobadilika, majukumu yanyobadilika na mbinu mpya. Kurasa mpya za historia zinaandikwa, pamoja na mafarakano mapya na ushirika mpya, malalamiko mapya na mafanikio mapya."

Pili, mwanadiplomasia huyo kutoka Hungary anaamini, kwamba wazo lilitolewa wazi katika ukumbi wa mkutano wa Baraza Kuu kwamba vita vya Ukraine lazima vikomeshwe. 

“Athari zake zinaonekana duniani kote, mfumuko wa bei, uhaba wa chakula, mbolea, gharama za nishati, hofu juu ya usalama wa mitambo ya nyuklia na tishio la matumizi ya silaha za nyuklia. Lakini vita hivi, ingawa ni vya kiwango kikubwa na cha uharibifu, bado sio pekee ulimwenguni, pamoja na Ukraine, uhasama unafanywa katika maeneo mengine 30. Na hakuna hata moja ya maeneo hayo duniani ambako hali haiboreki.”

Tatu, mada nyingine iliyoguswa na karibu kila mtu, ilikuwa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi amesema Bwana Körösi

“Tumesikia kuhusu nchi zinazokumbwa na ukame na mafuriko kwa wakati mmoja. Tumesikia wito wa kutokomeza hewa chafu na wito wa kusaidia nchi ambazo bila kosa lao zimeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Tumesikia wazi wito wa kuhakikisha haki na kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Körösi. 

Lakini, mwenyekiti huyo wa UNGA77 ameonyesha masikitiko yake, sio kila mtu anaamini kwamba ukuaji wa uchumi unapaswa kusawazishwa na hatua za kupunguza uzalishaji na kulinda bioanuwai.

Nne: Suala lingine lililoleta pamoja hotuba nyingi ni hali katika uwanja wa haki za binadamu na ulinzi wa wale ambao wanaweza kuteseka kutokana na unyonyaji. Hasa kwa makundi kama wanawake na watoto, wawakilishi wa jamii za makundi mbalimbali ya walio wachache, ikiwa ni pamoja na yale ya kikabila, kidini na lugha mbalimbali.

Amesisitiza kuwa "Utofauti ni nguvu, na si udhaifu," 

Tano: Mada nyingine ambayo ilipata uungwaji mkono mkubwa, inahusu haja ya kufanya Umoja wa Mataifa kuwa wa kisasa, kuhuisha kazi ya Baraza Kuu na mageuzi kwenye Baraza la Usalama.

Csaba Körösi amesema "Hii inaambatana na imani yangu kwamba Baraza Kuu linapaswa kujiandaa vyema zaidi kukabiliana na migogoro inayofungamana na Baraza la Usalama linapaswa kuonyesha hali halisi ya karne hii".

Waandishi wa habari wakiwa nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala wa kikao cha 77 ya Baraza Kuu
© Ingrid Kasper
Waandishi wa habari wakiwa nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala wa kikao cha 77 ya Baraza Kuu

Nini kinafuata?

Mwenyekiti huyo wa Baraza Kuu anaamini kwamba baada ya janga la COVID-19, ambalo limesababisha uharibifu mkubwa kwa binadamu, kila mtu anataka kuishi kwa amani, kufanya kazi pamoja na kutafuta suluhu za changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Huko nyuma mwezi wa Juni, baada ya kuchaguliwa kwenye wadhifa wake, Körösi alitaja vipaumbele vya uenyekiti wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu kuwa ni pamoja na kutafuta suluhu kwa msingi wa mshikamano, maendeleo endelevu na sayansi.

"Ili kupata maendeleo, katika kipindi kijacho, tunapaswa kuendeleza nyakati zinazotuunganisha. Ili kuimarisha mshikamano, lazima tujenge uaminifu,” mwanadiplomasia huyo alisema.

Bila kuahirisha kazi hizi muhimu hadi hapo baadaye, tayari wiki hii mwenyekiti huyo anapanga kuanza mfululizo wa mashauriano na wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya umma na jumuiya za kisayansi. Lengo lake ni kuweka msingi imara wa kazi ya kikao cha sasa cha Baraza Kuu.