Amani inaimarika Sudan Kusini lakini bado tuna changamoto: Agany

22 Septemba 2022

Amani nchini Sudan Kusini inaendelea kuimarika huku idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani wameanza kurejea katika makazi yao kwenye maeneo ambako utulivu umerejea na serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha mkataba wa amani unadumiswa amesema makamu wa Rais wa Sudan Kusini Hussein Abdelbagi Akol Agany akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza kuu hii leo mjini New York Marekani.

Bwana ASgany ameanza hotuba yake kwa kuzungumzia suala la elimu ambayo amesema inapewa kipaumbele kikubwa na serikali hasa ukizingatia vita vilivyosababisha watu wengi kukimbia makwao na kuwa wakimbizi wa ndani nan je imesababisha changamoto kubwa katika elimu. 

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha watoto wanapata elimu kwa kila njia serikali imeongeza bajeti ya elimu hadi kufikia asilimia 17.

Amani na usalama

Makamu huyo wa Rais amesema pande zinazopigana nchini Sudan Kusini zimejitolea kutekeleza makubaliano ya amani ambayo yameimarisha usalama nchini humo.

Ameongeza kuwa mkataba wa amani, uliotiwa saini na Serikali na vikundi vya upinzani miaka minne iliyopita, ulimaliza miaka mingi ya migogoro katika taifa hilo changa zaidi duniani, lililokuwa huru tangu Julai 2011.

"Kutokana na amani ya kiasi, wakimbizi wa ndani na wakimbizi wamekuwa wakirejea nyumbani kwa hiari, ingawa kujumuishwa tena rasmi katika jamii kunasalia kuwa changamoto kutokana na rasilimali chache.”

Zaidi ya hayo, amesema pande hizo zimeafikiana kuhusu ramani ya kukamilisha kazi zilizosalia chini ya makubaliano hayo, ambayo yatafungua njia ya uchaguzi pindi kipindi cha mpito kitakapokamilika mwaka wa 2025.

Makamu wa Rais ameongeza kuwa muundo wa vikosi vya pamoja vya kitaifa pia umeanzishwa, akielezea maendeleo kama kama hatua kubwa kuelekea mabadiliko yao na utaratibu wanaoutaka.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa makubaliano ya amani unakabiliwa na changamoto kadhaa, "Ikiwemo vikwazo vilivyowekwa na washirika wa kimataifa kwa watu binafsi na mashirika havisaidii katika mchakato huu.”

Kwa mantiki hiyo makamu huyo wa Rais ametoa wito” Tunaiomba jumuiya ya kimataifa na hususan Umoja wa Mataifa kupitia upya vikwazo hivyo zinavyolenga watu binafsi na vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya Sudan Kusini ili kuruhusu ukamilishaji wa masuala yaliyosalia ambayo yameainishwa kwenye barabara ya makubaiano mapya ya amani.”

Mafuriko na uhaba wa chakula

Bwana Agany pia ameripoti kuhusu changamoto nyingine zinazoikumba Sudan Kusini. 

Amesema hadi asilimia 80 ya nchi hiyo imeathiriwa na mafuriko kwa miaka mitatu mfululizo, na hivyo kudhihirisha kuwa "Mabadiliko ya tabianchi ni ya kweli".

Ili kupunguza athari kwa maisha na uwezo wa watu kuishi, mamesema serikali ya Sudan Kusini inachangia dola milioni 10 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP kusaidia jamii zilizofurushwa na machafuko ambazo nyingi ni za wakimbizi wa ndani.

"Hata hivyo, tunahitaji kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kufikia maeneo yote ya jamii zilizoathirika na mafuriko na na ukame," amesema.

Ameongeza kuwa serikali pia ilifanya tathimini mapema mwaka huu, ambayo ilibaini kuwa takriban watu milioni 6.8, zaidi ya nusu ya watu wote nchini humo  wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na wengine milioni 2.37 katika kiwango cha dharura.

“Hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula imechochewa zaidi na mchanganyiko wa sababu kama mafuriko, ukame wa muda mrefu, tatizo la usalama na athari za janga la COVID-19.”

Athari za COVID-19

Akizungumzia juhudi za kukabiliana na COVID-19 Bwana Agany amearifu kuwa  Sudan Kusini imeweza kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona kupitia hatua za Madhubuti na zilizolengwa. 

Na matokeo yah atua hizo ni kiwango cha chini sana cha wagonjwa na vifo.

Hadi kufikia Mei 9, amesema ni wagonjwa 17,513 tu waliothibitishwa wa COVID-19, pamoja na vifo 138, vimeripotiwa tangu kuanza kwa janga hili, na chanjo imeshatolewa kwa asilimia 45miongoni mwa watu wazima.

"Pamoja na habari hizi nzuri za kiafya, janga hili limekuwa na athari mbaya kwa uchumi, kuanzia kushuka kwa uzalishaji wa ndani na ukusanyaji wa mapato, ukifuatiwa na kupanda kwa gharama ya maisha," amesema.

Ameongeza kuwa "Madhara haya ya kiuchumi yamefika mbali, yanadhoofisha sana, kwa mfano rasilimali watu, haswa katika elimu, kwani hatua za kufunga kila kitu kuzuia kusambaa zaidfi kwa ugonjwa huo kuliwanyima watoto wa umri wa kwenda shule fursa za kusoma."

Kuchagiza amani kwa njia ya upatanishi

Bwana Agany pia hotuba yake imeangazia juhudi za Sudan Kusini za kukuza amani na utulivu, katika kanda na kwingineko.

Amesema nchi hiyo imefanikiwa kupatanisha mzozo wa silaha katika nchi jirani ya Sudan, juhudi ambazo zimesaidia kusainiwa kwa makubaliano ya amani mwaka 2020.

"Sudan Kusini iko tayari kupatanisha mzozo uliopo kati ya jeshi la serikali na vikosi vya FFC nchini Sudan ili hatimaye Sudan iweze kufurahia amani ya kudumu," amesema.

Ameongeza kuwa hivi majuzi, mamlaka  ya nchi hiyo ilijitolea kupatanisha mvutano kati ya Misri na Ethiopia katika kutokubaliana kwao juu ya ujenzi wa bwawa kuu la Renaissance la Ethiopia, na katika hali zingine zinazohusisha mzozo wa Tigray.

Amesema "Kwa kushiriki katika kuleta amani na utulivu wa kikanda, Sudan Kusini imedhihirisha uwezo wake kama mshirika wa kuaminika katika kutafuta amani na usalama wa kikanda na kimataifa.”

Ameendelea kusema kwamba “Zaidi ya hayo, Jamhuri ya Sudan Kusini inachangia kikosi kimoja katika vikosi vya kulinda amani ambavyo ni sehemu ya majeshi ya Afrika Mashariki katika kuleta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.”

Akigeukia vita ya Ukraine, bwana Agany ameainisha jinsi ambavyo vimeharibu maisha ya watu nchini humo na kuathiri uchumi wa dunia.

"Kwa mtazamo wa kimaadili, serikali ya Sudan Kusini inatoa wito kwa Urusi na Ukraine kusitisha aina zote za uhasama na kutatua mzozo huo kupitia mazungumzo ya kidiplomasia na yenye kujenga ili kuepusha madhara zaidi."
TAGS: Sudan Kusini, amani na usalama, elimu, Ukraine, DRC, COVID-19, uhakika wa chakula, WFP

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter