Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubinadamu uko njiapanda, ni wajibu wetu kuchukua hatua kuunusuru: Ethiopia

Naibu waziri mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen akuhutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu UNGA77
UN Photo/Cia Pak
Naibu waziri mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen akuhutubia mjadala wa wazi wa Baraza Kuu UNGA77

Ubinadamu uko njiapanda, ni wajibu wetu kuchukua hatua kuunusuru: Ethiopia

Masuala ya UM

Naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen amesema dunia inakabiliwa na mitihani mingi hivi sasa na imejikuta ipo njia panda kuanzia suala la mabadiliko ya tabianchi, umasikini uliokithiri, migogoro, ugaidi na mivutano ya kimataifa.

Akihutubia mjadala wa wazi wa Baraza kuu hii leo Bwana. Mekonnen amesema athari za changamoto hizo ni kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya watu na dunia na cha kusikitisha zaidi “Kiwango cha ushirikiano wa kimataifa hivi sasa hakiko katika nafasi inayostahili kushughulikia changamoto hizo.”

Na hivyo ameiomba jumuiya ya kimataifa kulitilia maanani suala na kuboresha ushirikiano wa kimataifa kwa ajili 

Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi

Naibu Waziri mkuu huyo amesema ingawa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ni mtambuka na linaikumba dunia ncima lakini waathirika zaidi ni wale ambao hawausiki katika uzalishaji wa gesi chafuzi inayochangia tatizo hilo mathalani Pembe ya Afrika  ambako amesema “Sehemu kubwa imeathirika na ukame unaojirudia na sehemu zingine zinakabiliwa na mafuriko makubwa.”

Hata hivyo amesema janga hilo la mabadiliko ya tabianchi linaweza kuzuilika hivyo “Natoa wito kwa mataifa yote kutafsiri maneno kuwa vitendo. Lazima tuhakikishe ufadhili wa kudhibiti athari na kuzikabili. Lazima tuchukue hatua kutimiza malengo yetu ya kukomesha uchafuzi wa hew ana hii inahitaji ushirikiano na mshikamano wa kimataifa.”

Amesisitiza kuwa “Afrika haihusiki na uchafuzi unaoleta janga la tabianchi lakini ndio tunaoathirika zaidi na kuchangia zaidi katika kukabili janga hili hivyo natoa wito wa mshikano wa kimataifa katika kuwekeza kwenye hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi”

Mabadiliko kwenye Baraza la Usalama

Kuhusu kulifanyia mabadiliko Baraza la Usalama waziri huyo amesema  wakati umefika wa kuhakikisha chombo hicho muhimu cha Umoja wa Mataifa kinakwenda na hwakati na hali halisi ya sasa duniani , kikiwa jumuishi na chenye usawa.

Ameongeza kuwa dhamira ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ilikuwa kuhakikisha amani duniani , lakini hadi sasa chombo hicho hakijafikia lengo la kuhakikisha ujumuishwaji wa usawa katika nguzo zake .

Mathalani amesema “Afrika haina kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama. Ombi letu la suluhu za Afrika kwa changamoto za Afrika halijatekelezwa. Tunaamini kuyapa uzito maombo haya kunasisitiza uaminifu wa Baraza kwa bara hilo.”

Amesema changamoto za afrika zinaweza kushughulikiwa kwa mitazamo ya Afrika inayozingatia maslahi ya bara hilo nan chi husika.

Amani na usalama

Ethiopia katika miaka minne iliyopita imepiga hatua kubwa za kiuchumi na kimaendeleo lakini pia bado inapitia changamoto nyingi hasa za za amani na usalama hivi sasa kwani Novemba mwaka 2020 mashambulizi dhidi ya jeshi la serikali yalizusha mzozo unaoendelea Kaskazini mwa nchi hiyo Tigray.

Amesema athari zilizosababishwa na mashambulizi ya kundi hilo aliloliita la wahalifu yanaendelea kusababisha zahma kubwa kwa watu wa Ethiopia.

Amesema serikali ya taifa hilo la Pembe ya Afrika lilijaribu kwa kila njia kuepuka mzozo huo lakini kwa bahati mbaya juhudi za kuzuia mzozo huo hazikuzaa matunda.

Hata hivyo amesema bado kuna matumaini na wanawategemea watu wa Ethiopia kutatua mzozo huo kwa pamoja na kuanza mchakato wa kujijenga upyya kama taifa moja lisilo na migawanyiko.

  Ametoa wito wa msaada kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo, kujenga upya taifa hilo na kurejesha amani na utulivu ili kuwaondolea madhila maelfu ya wananchi wanaoendelea kuteseka.

Malengo ya maendeleo endelevu SDG’s 

Naibu Waziri mkuu huyo amesema janga la COVID-19 limechangia kuzorotesha utekelezaji wa SDG’s na ndio maana taifa hilo sasa linajikita katika mikakati ya kuboresha mifumo ya kilimo, uzalishaji, biashara na ukuzaji wa uchumi ili kurejesha SDG’s katika msitari unaotakiwa.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzisaidia nchi za Afrika ili kutimiza malengo hayo na kuhakikisha hakuna mtu au taifa linaloachwa nyuma ifikapo mwaka 2030.

Amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito wa kudumisha ushirikiano wa kimataifa akisema changamoto za dunia hivi sasa zinahitaji umoja na sio migawanyiko na mivutano.