Mshikamano wa kimataifa umekwenda kombo ni wakati wa kubadili mwelekeo huo: Kagame

21 Septemba 2022

Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia katika mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema jumuiya ya kimataifa na mshikamano wa kimataifa viko njia panda katika wakati ambao vinahitajika kuliko wakati mwingine wowote.

Amesema miaka ya 2020 itakumbukwa katika histori kwamba ni wakati ambao ushirikiano wa kimataifa umepoteza dira, hata hivyo amesema mwelekeo uko bayana ambao ni ajenda ya kusongesha maendeleo , afya, na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema “Marekebisho katika mfumo wa afya kimataifa ni kipaumbele na shukran kwa shirika la afya la Umoja wa Mataifa Who na wadau wengine wa kimataifa .”

Rwanda afya ni kipaumbele chetu

Amsema mathalani nchini kwake Rwanda zaidi ya asilimia 90 ya watu wana bima ya afya hatua ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha afya “Na hii inadhihirisha kwamba inawezekana kwa kila nchi bila kujali kiwango chake cha kiuchumi kufanya huduma za afya kupatikana na kwa gharama nafuu kwa kila mtu kote duniani.”

Rais Kagame pia ametoa wito wa kuendelea kutunisha mfuko wa kimataifa wa ufadhili Global Fund na muungano wa chanjo duniani GAVI kwani mchango wake ni mkubwa na umedhihirika wakati wa janga la COVID-19 hasa Afrika ambako amesema ajenda ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa ndio ajenda ya Afrika pian a kwamba bara hilo lina uwezo wa kutimiza ajenda hiyo.

Afrika Bado inasuasua kwenye SDGs

Ameongeza kuwa pamoja na kuwa na uwezo wa kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ikizingatiwa kwamba ni maskani kwa uchumi unaokua kwa kasi duniani lakini bado bara hilo linaendelea kujikongoja .

Ametoa wito wa ukuaji wa uchumi kuwa jumuishi ili kupunguza pengo la walio nacho na wasio nacho na tayari amesema mipango imeshawekwa na endapo itajumuisha wadau wote ikiwemo sekta binafsi basi basi inawezekana kutimiza malengo ya SDGs.

Kingine kitakachosaidia kusongesha mchakato huo amesema ni kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU ambao ni daraja la kutimiza malengo hayo , sanjari na matumizi ya teknolojia bunifu ambayo itaruhusu nchi za Afrika kuchukua hatua bila kupunguza kasi ya maendeleo.

Kuhusu Amani na usalama

Kuhudu kudumisha Amani na usalama Afrika na duniani kote Rais huyo wa Rwanda amesema “Ni muhimu sana kwa afrika na jumuiya nzima ya kimataifa kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu katika ulinzi wa amani na juhudi za ujenzi wa amani kwa kuheshimiana.”

Ameendelea kusema katika wiki zijazo Rwanda inajiandaa kupokea wimbi la wakimbizi wa waomba hifadhi waliokuwa vizuizini nchini Libya na ameshukuru msaada na uungwaji mkono kutoka kwa kamishina mkuu wa wakimbizi na Umoja wa Mataifa kwa ujumla katika hilo.

Pia ameziomba nchi zingine kuzingatia wajibu wao wa kimataifa “Tunatoa wito kwa wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kuzingatia wajibu wao wa kisheria kwa dhamira ya mshikamano. Mshimkamano huu ni ishara ya wazi kwamba tunaweza kushirikishana kushughulikia changamoto mtambuka. Afrika yenyewe ni chanzo cha suluhu”

Ameongeza kuwa ni dhahiri kwamba pengo la kutokuwepo usawa duniani ni changamoto ambayo inaweza kutatuliwa tuu kwa kushirikiana kwa pamoja.

Kwa mantiki hiyo amehitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba taifa lake liko tayari kuhakikisha firsa zinapatikana kwa usawa hasa kwa wanawake na wasichana na amesema mwezi Novemba mwaka huu mkutano wa kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia utafanyika Kigali Rwanda.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter