Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mali tuko mwelekeo sawa wa mpito unaokoma Machi 2024- Kanali Maiga

Abdoulaye Maïga, Kaimu Waziri Mkuu wa Mali akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA77
UN /Cia Pak
Abdoulaye Maïga, Kaimu Waziri Mkuu wa Mali akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA77

Mali tuko mwelekeo sawa wa mpito unaokoma Machi 2024- Kanali Maiga

Masuala ya UM

Katika siku ya tano ya Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 jijini New York, Marekani, Mali imesema iko kwenye mwelekeo sahihi wa kipindi cha serikali ya mpito kilichoanza mwezi Agosti mwaka 2020 na ukomo wake mwezi Machi mwaka 2024.

Akihutubia mkutano huo, Kaimu Waziri Mkuu Abdoulaye Maïga amesema tayari wameshapitisha sheria ya uchaguzi inayohusisha kuanzishwa kwa mamlaka huru ya usimamizi wa uchaguzi na tayari kumeunda kamisheni ya kutunga katiba mpya, kamisheni inayojumuisha wajumbe kutoka pande mbalimbali za jamii ya Mali.

Mali yakabiliwa na changamoto 4 kwa mpigo

Amesema si watu wengi watatambua kuwa Mali ni nchi pekee duniani ambayo inakabiliwa na changamoto nne za kiusalama kwa wakati mmoja; ugaidi, mapigano baina ya makabila  yanayochochewa na magaidi na vikundi vinavyoungwa na serikali za kigeni, uhalifu wa kuvuka mipaka na ghasia zinazofanywa na watu binafsi.

Kanali Maiga amesema sambamba na harakati za kurejea katika utulivu wa kikatiba, Mali inaendelea kupambana bila kuchoka dhidi ya ukosefu huo wa usalama hususan kwa vikundi vyenye misimamo mikali vinavyohusika na ukatili wote kwa wananchi wetu wenye amani.

“Nina furaha kusema kuwa vikundi vya kigaidi vimedhoofishwa kwa kiasi kikubwa, na hofu sasa iko kwao. Hata hivyo bado vikundi hivi vinaweza bado kuleta madhara katika majaribio yao ya kutishia uhuru wa mipaka yetu na kujenga hofu miongoni mwa wananchi wetu,” amesema Kaimu Waziri Mkuu huyo wa Mali.

Amesema vikosi vyetu jasiri vya ulinzi na usalama vimeazimia kukabili vitisho vinavyotoka upande wowote ule.

Uimarishaji wa jeshi la serikali

Kaimu Waziri Mkuu Maiga amesema chini ya uongozi wa Kanali Assimi Goita, ambaye ndiye Rais wa serikali ya mpito Mali, seirkali inaendelea kuimarisha juhudi zake za kuajiri, kufundisha, kupatia vifaa na kujenga uwezo wa jeshi la ulinzi na usalama nchini humo.

“Naweza kusema hapa kuwa operesheni ya mashambulizi iliyofanywa hadi hivi sasa imewezesha majeshi yetu kupata Ushindi dhidi ya vikosi vamizi. Vimewezesha serikali yetu kutwaa tena na kuimarisha mamlaka yake kwenye eneo la Mali, sambamba na kuchagiza kurejea kwa maelfu ya raia wetu kwenye makazi yao ya awali,” amesema Kanali Maïga.

Hata hivyo amesema “tunafahamu sote kuwa majawabu ya kijeshi na usalama yana ukomo na ndio  maana katika kuunga mkono harakati za kijeshi, serikali ya Mali imepitisha mkakati mpana unaojumuisha hatua za kisiasa, kijamii na maendeleo, ambao unahusisha mathalani kupatia wananchi wetu huduma za msingi kama za kijamii ili kukabili mchanganyiko wa changamoto zinazowakabili tangu mwezi Januari mwaka 2012.”

Tunashukuru MINUSMA lakini mpango uangaliwe upya

Walinda amani kutoka MINUSMA wakizungumza na wanakijiji kuhusu changamoto zao Gao, Kaskazinimashariki mwa Mali.
MINUSMA/Harandane Dicko
Walinda amani kutoka MINUSMA wakizungumza na wanakijiji kuhusu changamoto zao Gao, Kaskazinimashariki mwa Mali.

Kuhusu mchango wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA, Kanali Maiga ametumia hotuba yake kusema kuwa katika “harakati zetu ngumu za kusaka amani, utulivu na maendeleo endelevu, wananchi wa Mali wanasalia na shukrani kubwa kwa juhudi na kujitoa kwa hali na mali kwa MINUSMA tangu kuanzishwa kwake mwezi Julai mwaka 2013 hadi hii leo, lengo likiwa ni kusaidia Mali kurejesha mamlaka yake kwenye eneo lote la nchi.”

Hata hivyo amesema ni changamoto kubwa kuwa takribani miaka 10 tangu kuanzishwa kwa MINUSMA, lengo lake bado halijafikiwa licha ya maazimio lukuki ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Ndio maana serikali ya Mali inasisitiza ombi lake, mara kwa mara la kubadili mwelekeo wa utendaji, MINUSMA iendane na mazingira ambamo kwayo ilianzishwa na kutekeleza kwa ubora zaidi jukumu lake na mamlaka za Mali,” amesema Kanali Maïga.

Amesema ni kwa mantiki hiyo ni muhimu kwa MINUSMA kusalia kuwa kikosi cha usaidizi wakati kinasaka kuleta utulivu Mali na kwamba “serikali ya Mali inapinga ushawishi wowote wa kigeni unaojaribu kuhamasisha makundi yaliyoko kihalali nchini Mali kutumikia ajenda za siri ikiwemo kutumia kisingizio cha haki za binadamu ili kuleta vurugu Mali.”