Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jiulize bila elimu ungalikuwa wapi? Lakini kwa watoto maskini bado elimu ni ndoto- Guterres

Watoto wakiwa wameketi kimduara na mwalimu wao katika kituo cha awali cha maendeleo ya mtoto kwenye kijiiji cha Garin Badjini, kusini-mashariki mwa Nigeria
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Watoto wakiwa wameketi kimduara na mwalimu wao katika kituo cha awali cha maendeleo ya mtoto kwenye kijiiji cha Garin Badjini, kusini-mashariki mwa Nigeria

Jiulize bila elimu ungalikuwa wapi? Lakini kwa watoto maskini bado elimu ni ndoto- Guterres

Utamaduni na Elimu

Bila elimu ningalikuwa wapi? Tungalikuwa wapi wengi wetu humu ndani?  Ndivyo alivyoanza hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati akihutubia viongozi walioshiriki kikao cha ngazi ya juu cha mkutano wa marekebisho ya mfumo wa elimu duniani, kikao kilichofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Katibu Mkuu amewaeleza viongozi hao “kila mmoja wetu kwenye huu ukumbi anatambua kuwa elimu inarekebisha na kubadilisha maisha, uchumi na jamii.”

Amesema hata hivyo elimu hivi sasa badala ya kuwa mwezeshaji wa kuboresha maisha imekuwa sababu ya kuleta mgawanyiko katika jamii kwa kuwa iko kwenye janga kubwa.

“Asilimia 70 ya watoto wenye umri wa miaka 10 katika nchi zinazoendelea hawana uwezo wa kusoma sentensi rahisi. Iwe wako shuleni au hawako shuleni, hawajifunzi,” amesema Guterres.

Watoto wa kike wakisoma pamoja nje ya shule inayosaidiwa na UNICEF huko Tigray nchini Ethiopia
© UNICEF/Esiey Leul Kinfu
Watoto wa kike wakisoma pamoja nje ya shule inayosaidiwa na UNICEF huko Tigray nchini Ethiopia

Matajiri wapata elimu bora huku maskini wakihaha

Kitu cha kusikitisha zaidi kwa mujibu wa Katibu Mkuu, “matajiri wana uwezo wa kupata rasilimali bora zaidi, shule na Vyuo Vikuu bora na hivyo kuwawezesha kupata ajira bora, ilhali maskini, hususan wasichana wanakabiliwa na vikwazo vya kupata sifa ambazo zingebadili maisha yao.”

Amesema mifumo ya elimu haipatii kipaumbele uwezo wa kumpatia mwanafunzi fursa ya kujifunza kipindi chote cha maisha yake, walimu hawana mafunzo ya kutosha, hawathaminiwi na wanalipwa ujira mdogo.

“Pengo la kidijitali linagharimu zaidi wanafunzi maskini, na pengo la elimu linazidi kupanuka zaidi na zaidi.”

Elimu ipatie wanafunzi uwezo wa kujifunza jinsi ya kujifunza

Ametaka elimu bora iwezesha kusaidia maendeleo binafsi na mwanafunzi maisha yake yote. Lazima isaidie watu kujifunza jinsi ya kujifunza, ikijikita katika utatuzi na ushirikiano. Lazima iweke misingi ya kujifunza, kuanzia kusoma, kuandika, hisabati, sayansi, dijitali na stadi za kijamii na kihisia.

Lakini zaidi ya yote ametaka elimu iwezeshe wanafunzi kuwa na uwezo wa kukabiliana na dunia ya sasa ya ajira inayobadilika kila uchao.

Tusaidie watoto wakamilishe masomo- Vanessa

Balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Vanessa Nakate naye alipata muda wa kuhutubia mkutano huo ambapo amesema, “leo mko hapa nyote kusaidia kusaka majawabu ambayo yataleta marekebisho kwenye mifumo yetu ya elimu na ili ikidhi mahitaji na malengo.”

Amesema ni lazima kila mtu awezesha watoto wote wawe na fursa ya elimu, na “lazima tuwasaidie wasalie shuleni. Mustakabali wao unategemea elimu.”

Malala Yousafzai, Mjumbe wa amani wa UN na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel akihutubia UN.
UN /Mark Garten
Malala Yousafzai, Mjumbe wa amani wa UN na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel akihutubia UN.

Viongozi msipitishe ahadi za kibahili - Malala

Kwa upande wake, mshindi wa tuzo  ya amani ya Nobel kwa mwaka 2014, Malala Yousafzai ametoa wito kwa viongozi kutotoa ahadi za kibahili na za muda mfupi na badala yake, “wekeni ahadi za kuzingatia haki ya kukamilisha elimu na kuziba pengo la fedha.”

Bi. Yousafzai amesema “lazima mtumie mamlaka mliyo nayo kuchukua hatua. Tengeni asilimia 20 ya bajeti yenu kwenye elimu. Nchi za vipato vya juu ongezeni msaada, futeni madeni na wekeni mfumo sawia wa kodi duniani ili nchi za kipato cha chini ziweze kutumia fedha zaidi kwa ajili ya wasichana.”

 

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 akijisomea nyumbani kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul baada ya serikali ya Taliban kutangaza kuwa shule hazitafunguliwa kwa ajili ya watoto wa kike wa darasa la 7 hadi 12.
© UNICE/Mohammad Haya Burhan
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 akijisomea nyumbani kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul baada ya serikali ya Taliban kutangaza kuwa shule hazitafunguliwa kwa ajili ya watoto wa kike wa darasa la 7 hadi 12.

Zaidi ya nchi 130 zaweka ahadi nzito za kuchochea mifumo yao ya elimu

Mwishoni mwa mkutano, ilitolewa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka ofisi inayosimamia mkutano huo ikisema kuwa zaidi ya 130 zinazoshiriki kwenye mkutano zimeahidi kuchochea mifumo yao ya elimu, na kuchagiza hatua ili kumaliza janga la kujifunza duniani.

Ahadi hiyo imekuja baada ya vikao 115 vya mashauriano vilivyoleta pamoja viongozi, walimu, wanafunzi, mashirika ya kiraia na wadau wengine, vikao ambavyo vilikusanya mapendekezo kuhusu majukumu yanayopaswa kutekelezwa haraka.

Takribani nusu ya mataifa hayo, yamepatia kipaumbele mikakati ya kukabiliana na fursa ya kujifunza iliyopotea, huku theluthu moja ya nchi zikiahidi kusaidia ustawi bora wa kisaikolojia na kijamii kwa wanafunzi na walimu.

Nchi mbili kati ya tatu pia zimetaja hatua za kuondokana na gharama za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za elimu kwa jamii zilizo hatarini, ilihali asilimia 75 ya nchi hizo 130 zimesisitiza umuhimu wa sera za elimu zinazingatia masuala ya jinsia.

Taarifa hizo zinapatia msisitizo dhima ya elimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na uhusiano wake na majanga ya tabianchi, mizozo na umaskini.

Hatua za kushughulikia kujikwamua baada ya coronavirus">COVID-19 na kurejea katika mwelekeo wa kufanikisha SDGs pia zimetajwa huku wakisisitiza umuhimu wa ugunduzi katika elimu ili kuandaa wanafunzi wa leo kuweza kukabiliana na dunia inayobadilika kwa kasi kubwa.

Kuhusu Mkutano wa Marekebisho ya mfumo wa elimu

Mkutano wa marekebisho ya mfumo wa elimu ni mpango mkuu wa Ajenda ya Pamoja iliyozinduliwa na Katibu Mkuu mwezi Septemba mwaka 2021.

Mkutano huu unafanyika wakati wa UNGA77 kwa lengo la kuweka elimu katika ajenda kuu ya kisiasa na kuchagiza hatua, mshikamano na majawabu.