"Katika zama za mitikisiko, dhima ya UN ni muhimu kuliko wakati wowote," Katibu Mkuu UN

15 Septemba 2022

Kipindi cha mwaka mmoja uliopita kimekuwa cha majanga yaliyoingiliana na makubwa na ambayo yameendelea kuongezeka kwa ukumbwa na makali yake, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, akitaja janga la COVID-19, vita nchini Ukraine, kuongezeka kwa janga la tabianchi.  Amesema majanga hayo yamevuka mipaka na yamefanya dhima ya Umoja wa Mataifa kuwa muhimu zaidi kuliko wakati wowote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo katika ripoti yake ya mwaka kuhusu Dhima ya Umoja wa Mataifa, ripoti ambayo hutolewa mwanzoni mwa mwaka mpya wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao huanza mwezi Septemba kila mwaka, siku chache kabla ya kuanza kwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu, UNGA.

Guterres amesema janga la Corona limeota mizizi na huku chini ya asilimia 20 ya wakazi wan chi za kipato cha chini wakiwa ndio wamepata chanjo pekee, suala la kujikwamua kutoka janga hilo bado halina usawa.

Kuhusu vita ya Ukraine, amesema imesababisha machungu kwa mamilioni ya watu nchini humo nan je ya nchi hiyo na imepazia sauti madhara ya janga la tabianchi na ukosefu wa usawa uliodumu muda mrefu.

Kwa kuzingatia yote hayo, Katibu Mkuu amesisitiza kwenye utangulizi wa ripoti yake kuwa mwaka mzima wa 2021, Umoja wa Mataifa kama jukwaa la ushirikiano wa kimataifa na mshikamano uliitisha wadau na kusongesha uchechemuzi wa kimataifa na ushirikiano, kama miongoni mwa hatua ili kupunguza umaskini, kukabili mabadiliko ya tabianchi, kuchochea nishati bora, marekebisho ya kidijitali na mifumo ya chakula.  

“Kwa pamoja katika mifumo ya Umoja wa Mataifa, tulitoa sera na majawabu, kusaidia kuunda mikakati na kupaza sauti za walio mstari wa mbele na wanaoenguliwa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa ulihamasisha hatua za kupunguza ukosefu wa usawa na kuhamasisha rasilimali na kuchochea uwekezaji wa maendeleo endelevu.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ni mwongozo wa kufikia mustakabali bora na endelevu kwa wote.
© UNDP
Malengo ya Maendeleo Endelevu ni mwongozo wa kufikia mustakabali bora na endelevu kwa wote.

Ajenda yetu ya Pamoja

Katibu Mkuu amezungumzia pia Ajenda ya Pamoja iliyozinduliwa na UN ikiwa na mapendekezo na majawabu ya changamoto za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kujenga jamii yenye usawa zaidi, yenye mnepo na endelevu kwa kuzingatia ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs pamoja na haki za binadamu.

Ripoti hiyo, amesema, ina mapendekezo ya njia za kujenga utangamano wa kijamii na mshikamano, kuzuia na kusimamia majanga na kutatua vitisho vya sasa vya usalama na vinavyoibuka.

“Kujibu ripoti hiyo, nchi wanachama wameridhia mapendekezo ambayo yanaweza kusongesha haraka, na wanashiriki kwa kikamilifu kwenye yale ambayo yanahitaji kazi zaidi na mashauriano ili kufanikisha Ajenda ya Pamoja.”

Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la UN kilichofanyika usiku kuhusu Ukraine
© UN /Mark Garten
Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la UN kilichofanyika usiku kuhusu Ukraine

Amani na Usalama viko kwenye tishio kubwa

Katibu Mkuu Guterres amesema muundo wa amani na usalama duniani umezidiwa uwezo, kama inavyodhihirishwa na vita ya Ukraine. Halikadhalika, vitisho vinavyoibuka pamoja, ushindani wa kimkakati kijiografia na ukosefu wa usawa vinaleta madhara siyo tu kwa watu waliokumbwa kwenye mizozo.

“Umoja wa Mataifa umeweka mbinu mbalimbali za kuzuia, kupunguza, kushughulikia na kutatua mizozo, kulinda raia, kukabili vitisho vinavyokumba wanawake na watoto, na kujenga njia za kujikwamua kutoka kwenye mizozo na majanga ili kuweko na maendeleo na amani endelevu,” amesema Guterres akigusia Yemen ambako Umoja wa Mataifa umefanikisha mkataba mpya wa sitisho la mapigano wa miezi miwili ambao umepunguza ghasia nchini humo.

“Kufuatia kuibuka kwa vita ya Ukraine, tulizungumza mara kwa mara kuunga mkono mamlaka ya taifa hilo, uhuru wake na mipaka yake kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa na juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za kimataifa na uwajibikaji,” amesema Guterres akiongeza kuwa, “tulishiriki pia katika mashauriano ya kufanikisha uuzaji nje ya nchi hiyo bila kikwazo chochote kwa nafaka na mbolea ili kusaidia kukabilia janga la uhaba wa chakula duniani, hatua ambayo ilifanikisha kupitishwa kwa makubaliano ya Usafirishaji Nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Mkataba huo ulitiwa saini baina ya Urusi, Ukraine na UTuruki chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa tarehe 22 mwezi Julai mwaka 2022.

 

Hatua za kibinadamu

Mkuu huyo wa UN amesema juhudi za kiutu zinazotekelezwa na shirika hilo zinalenga kusaidia watu wengi  waliotumbukizwa kwenye uhitaji kutokana na majanga yaliyoonga mizizi au mizozo isiyoisha, majanga ya asili, mabadiliko ya tabianchi na madhara ya janga la COVID-19.

Mwaka 2021, mipango ya usaidizi wa dharura iliyoratibiwa na  Umoja wa Mataifa ilihitaji dola bilioni 37.7 ili kutoa huduma za kuokoa maisha na ulinzi kwa watu milioni 174 katika nchi 60. Ukarimu wa wahisani pamoja na wadau wetu, tuliweza kuchangisha dola bilioni 20.25 na kufikisha misaada kwa watu milioni 107.

“Juhudi zetu za kumaliza ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana zilijumuisha Jukwaa la Usawa wa Vizazi, ambalo lilichochea ahadi kwenye sera na miradi na uchechemu pamoja na dola bilioni 40,” amesema Bwana Guterres akitanabaisha kuwa, kama sehemu ya kazi za shirika, za kuhamasisha hatua kinga dhidi ya ukatili na usaidizi kwa manusura, mpango wa Spotlight ulitenga dola milioni 48 kusaidia mashirika ya kiraia na ya wanawake huko mashinani, sambamba na kuimarisha mipango ya hatua ya kitaifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika nchi zaidi ya 30 duniani kote.

Dhima ya UN ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote ule

 

Katika juhudi zake zote hizo, Katibu Mkuu amesema, Umoja wa Mataifa ulisalia ukiongozwa na Chata yake, mifumo ya haki za binadamu, Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na mikataba mingine ya kimataifa inayolenga kupata mustakabali bora, endelevu, wenye ustawi na jumuishi kwa wote na asiweko mtu  yeyote anayeachwa nyuma.

Guterres ametamatisha akisema, katika zama za sasa za mitikisiko, dhima ya Umoja wa MAtaifa ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote. “Tunafahamu fika kuwa kitendo cha kusubiri kuchukua hatua tatizo linapotokea ndio linakwamisha dunia.”

Akimulika siku zijazo, Bwana Guterres amesisitiza kuwa mwaka ujao, “tutaendelea kusaidia kujenga mnepo na kupunguza machungu, huku tukisongesha mipango ya muda mrefu iliyoainishwa kwenye Ripoti ya Ajenda yetu ya Pamoja ili kuzuia majanga, kukabili hatari na kujenga mustakabali endelevu kwa wote.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter