Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Hichilema amesema Zambia itatumia vijana wake kuinua uchumi

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema wa Zambia akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN
UN /Cia Pak
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema wa Zambia akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN

Rais Hichilema amesema Zambia itatumia vijana wake kuinua uchumi

Masuala ya UM

Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amesema wameazimia kutumia vijana kama kichocheo cha kusongesha uchumi wa taifa hilo kwa kuzingatia kuwa theluthi mbili ya wananchi wake wana umri wa chini ya miaka 25.

Akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Hichilema amesema, “kwa kutazama mwelekeo wa siku za usoni na msisitizo wa uwiano wa kizazi ni muhimu kwetu sisi.”

Tutasaidia vijana wagunduzi ili kuchochea uchumi wa Zambia

Hivyo amesema serikali ya Zambia inasaka kunufaika na kuvuna faida ya kundi hilo kwa kuwekeza kwa vijana na wengine wenye nguvu kwa ajili ya mustakabali bora.

“Kwa hiyo tunaunga mkono kuanzishwa kwa ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya vijana,” amesema Rais Hichilema .

Amesema hatua hiyo itahamasisha vijana wengi kujishirikisha katika shughuli mbalimbali kama vile uwakilishi wa kisiasa, mafunzo ya stadi za maisha, elimu, kusaidia vijana wagunduzi, na bila shaka ujasiriamali, kupitisha maamuzi, na nyanja zote za kisiasa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira.

Elimu ndio mkombozi na mleta usawa

Rais huyo wa Zambia amezungumzia hatua walizochukua kuboresha sekta ya elimu nchini mwake akisema wanatambua kuwa “elimu ndio mleta usawa na wanatoa elimu bure ya msingi na sekondari.” Amesisitiza kuwa elimu ndio urithi bora kwa mtoto.

Na katika kufanikisha utoaji bora wa elimu na huduma za afya kwa mwaka wa 2022 pekee wameajiri walimu zaidi ya 30,000 na wahudumu wa afya 11,000.

Tumeshuhudia madhara ya hali mbayá ya hewa

Kwetu sisi, madhara ya mabadiliko ya tabianchi si mageni, amesema Rais Hichilema akisema yameendelea kuathiri nchi yao.

“Hebu niwaeleze kuwa hivi karibuni nusu ya eneo la Zambia lilipata viwango vya joto kupindukia na mazao hayakumea kabisa kutokana na ukame, huku nusu nyingine ilikumbwa na mafuriko katika msimu mzima, hii si kawaida, ni madhara ya mabadiliko ya tabianchi.”

Amesema matukio kama hayo ni kumbusho la madhara ya mabadiliko ya tabianchi, hivyo “tunahitaji majawabu ya kina na ushirikiano katika hatua zetu za kikanda na kimataifa za kukabili mabadiliko ya tabianchi.”