Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya vikwazo haramu dhidi ya Zimbabwe, tumeweza kudhibiti COVID-19- Rais Mnangagwa

Rais wa Zimbabwe Emmerson Dambudzo Mnangagwa akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN
UN /Cia Pak
Rais wa Zimbabwe Emmerson Dambudzo Mnangagwa akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN

Licha ya vikwazo haramu dhidi ya Zimbabwe, tumeweza kudhibiti COVID-19- Rais Mnangagwa

Masuala ya UM

Nchini Zimbabwe licha ya vikwazo haramu vya kimataifa tulivyowekewa, tumeweza kudhibiti janga la COVID-19, amesema Rais wa taifa hilo la kusini mwa Afrika Emmerson Mnangagwa wakati akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Alhamisi ya tarehe 22 Septemba mwaka 2022.

Ikiwa ni siku ya tatu ya Mjadala huo Mkuu, Rais Mnangagwa amesema licha ya vikwazo hivyo haramu vya kiuchumi “tumeweza kutekeleza mkakati wetu wa kitaifa wa kukabili COVID-19 uliotegemea kwa kiasi kikubwa rasilimali zetu za ndani na uwezo wetu wa kitaifa.”

Amesema hatua ya serikali yake ya kuchukua hatua mapema kabla ya tatizo, imewezesha taifa hili kufikia viwango vikubwa vya utoaji wa chanjo dhidi ya Corona, chanjo ambayo imetolewa pia kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea.

Ushirikiano wa Zimbabwe na Umoja wa Mataifa

Katika kutekeleza ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, hususan suala la kumuondoa kila mwananchi kutoka lindi la umaskini, amesema ushirikiano kati ya Zimbabwe na wadau wake ikiwemo Umoja wa Mataifa ni kipaumbele.

Amesema kupitia ubia, kumetekelezwa miradi mbalimbali ya kutokomeza umaskini na njaa kwenye jamii ikiwemo zile za wakulima wadogo.

“Mathalani katika ngazi ya kaya, miradi ya kuwapatia pembejeo za kilimo, vifaa na usaidizi wa kiufundi, imewezesha ongezeko la uhakika wa chakula katika kaya na kitaifa,” amesema Rais Mnangagwa huku akisema hata hivyo ukame wa katikati ya mwaka huu wa 2022 na vimbunga na mvua kubwa vimeleta mtikisiko.

Mfanyakazi wa afya akiwa katika Maaabara ya kupima COVID-19 katika hospitali ya Mlipo nchini Zimbabwe
© ILO/KB Mpofu
Mfanyakazi wa afya akiwa katika Maaabara ya kupima COVID-19 katika hospitali ya Mlipo nchini Zimbabwe

Mapinduzi ya viwanda vijijini

Rais Mnangagwa ametumia pia hotuba yake kujulisha washiriki juu ya mkakati uliochukuliwa na taifa hilo wa kuleta mapinduzi vijijini kwa lengo la kuhakikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Amesema wamejenga miundombinu ya kijamii katika maeneo ya ndani zaidi ya taifa hilo,  zikiwemo shule, kliniki, huduma za maji na kujusafi na huduma nyingine za kijamii.

“Na kwa muktadha huo huo, tunaendeleza maendeleo ya kijamii vijijini kwa kuzingatia urithi au bidhaa asilia ya kila eneo, ili kuhakikisha kila mkazi ana mbinu za kujipatia kipato,” amesema Rais Mnangagwa.

Katika medani za kimataifa ametaka marekebisho ya mfumo wa fedha wa kimataifa ili uweze kuwa na manufaa kwa kila taifa.

Vikwazo dhidi ya Zimbabwe

Vikwazo dhidi ya Zimbabwe vimewekwa na Marekani, Uingereza na Muungano wa Ulaya.

Vikwazo hivi vilianza mwaka wa fedha wa 2001/2002 na chanzo chake ni Mpango wa marekebisho ya umiliki wa ardhi ulioanzishwa na Rais wa kwanza wa nchi hiyo hayati Robert Mugabe, mpango ambao ulishuhudia kupokonywa ardhi wakulima wachache weupe na ardhi hiyo ikagawanywa kwa raia wa Zimbabwe wasio na ardhi.

Habari zinasema tangu wakati huo, vikwazo hivyo vimesababisha Zimbabwe kupoteza fursa ya kupatiwa zaidi ya dola Bilioni 100 kama msaada au mikopo kutoka kwa nchi, halikadhalika shirika la fedha duniani, IMF, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.