Skip to main content

Tufanye kazi pamoja turejeshe SDGs kwenye mwelekeo sahihi

Taswira ya ukumbi wa Baraza Kuu la UN wakati wa mkutano kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwenye makao makuu New  York, Marekani
UN /Mark Garten
Taswira ya ukumbi wa Baraza Kuu la UN wakati wa mkutano kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwenye makao makuu New York, Marekani

Tufanye kazi pamoja turejeshe SDGs kwenye mwelekeo sahihi

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika mkutano wa kutathmini mwelekeo wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema majanga lukuki yanayokumba dunia hivi sasa yanasababisha nia ya kufanikisha malengo hayo ifikapo mwaka 2030 kuendelea kuyoyoma.

Akihutubia viongozi wa nchi na vijana walioshiriki mkutano huo jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu ametaja majanga hayo kuwa ni pamoja na vita, mizozo, mabadiliko ya tabianchi, kutoweka kwa kuaminiana, mgawanyiko, umaskini, ukosefu wa usawa, ongezeko la gharama za maisha, kupanda kwa bei ya chakula na nishati huku vipato vinaporomoka, halikadhalika ukosefu wa ajira.

“Kila janga linarudisha nyuma SDGs na katika mazingira kama hayo, inashawishi kuweka kando vipaumbele vyetu vya maendeleo, visubiri siku njema lakini maendeleo hayawezi kusubiri,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mlkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano kuhusu SDGs 2022 jijini NEw York, Marekani
UN /Cia Pak
Katibu Mlkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano kuhusu SDGs 2022 jijini NEw York, Marekani

Elimu ya watoto wetu haiwezi kusubiri

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa elimu ya watoto haiwezi kusubiri, ajira zenye staha haziwezi kusubiri, usawa kwa wanawake na watoto wa kike haviwezi kusubiri, halikadhalika afya bora, hatua sahihi kwa tabianchi navyo haviwezi kuwekwa kando visubiri kesho.

Amesema katika hayo yote, vijana na vizazi vijavyo wanadai hatua, “na hatuwezi kuwaangusha huu ni wakati wa kuchukua hatua.”

Guterres amesema nyote mlio hapa na wengine mnaofuatilia mkutano huu kwa njia mbalimbali kutoka pande mbalimbali za dunia, mnanipatia matumaini makubwa kwamba tunaweza kuweka mikono yetu kwenye gurudumu la maendeleo na kulisongesha mwelekeo mpya.”

Vijana hawa wakimbizi kwenye makazi ya Kyangwali nchini Uganda sasa wanapata kipato kutokana na mradi wa kurejeleza chupa za plastiki unaotekelezwa na wadau wa UNHCR, Care International Uganda.
UN News
Vijana hawa wakimbizi kwenye makazi ya Kyangwali nchini Uganda sasa wanapata kipato kutokana na mradi wa kurejeleza chupa za plastiki unaotekelezwa na wadau wa UNHCR, Care International Uganda.

Mwelekeo ambao amesema utanusuru SDGs na kurejea katika mwelekeo sahihi wa kujenga dunia bora isiyomuacha yeyote nyuma.

Tunahitaji uwekezaji na fedha kutoka sekta ya umma na binafsi, amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa, hiyo ndio njia pekee endelevu ya kutatua ukosefu wa usawa uliojikita katika kila nchi, huku ikitoa hakikisho ya kwamba dunia haitotumbukia kwenye mdororo wa uchumi.

Serikali zinatakiwa kuwekeza

Serikali ziwekeze kuliko wakati wowote ule katika afya, elimu na ustawi wa wananchi wake wakiwemo wakimbizi na wahamiaji.

“Tunahitaji kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili kulinda watu dhidi ya mitetemo ya kiuchumi, huku tukiongeza fursa za ajira, hasa kwenye dijitali, huduma za malezi na uchumi usioharibu mazingira,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika kuinua wanawake na Watoto wa kike katika maeneo yote bila kusahau kunusuru sayari dunia.

UN Web TV
Amanda Gorman (Poet & Activist) recites poem for the SDG Moment 2022

Lakini Zaidi ya yote amesema hakutaweza kuweko kwa mustakabali endelevu bila amani, kwa hiyo, “kwa kukumbatia amani na stahmala na Zaidi ya yote kuishi maadili hayo kila siku, tunaweza kusogea hatua moja mbele kufikia dunia endelevu, sawa na haki kwa wote ambayo kila mtu anahitaji.”

Ametamatisha hotuba yake akisema “majukumu yaliyo mbele yetu ni makubwa. Vijana wanataka hatua, si kwa ajili yao tu bali kwa vizazi vijavyo. Majanga yanayotukabili hayafai kwa dunia iliyoungana. Twende kazini na twende turejeshe dunia yetu kwenye njia sahihi.”

Mabalozi wema wa mashirika washiriki kikao

Mshairi, mwanaharakati na muungaji mkono wa shughuli za shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Amanda Gorman, alitumia jukwaa hilo kushirikisha washiriki na shairi lake kuhusu wajibu wa viongozi katika kutokomeza umaskini na kulinda sayari dunia.

Wakati huo huo, wachechemuzi wa SDGs na nyota wa muziki wa K-Pop kutoka Korea Kusini walitoa ujumbe wao kwa njia ya video wakialika dunia ichukue hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kusongesha maendeleo endelevu.