Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi sasa inasonga mbele baada ya majanga mfululizo- Rais Ndayishimiye

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye wa Burundi akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN
UN /Cia Pak
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye wa Burundi akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN

Burundi sasa inasonga mbele baada ya majanga mfululizo- Rais Ndayishimiye

Masuala ya UM

Jumuiya ya kimataifa hii leo imejulishwa kuwa Burundi hivi sasa imekwamuka kutoka katika janga la kisiasa ambalo sio tu lilisababisha vifo vya wananchi bali pia liliharibu mazingira na inaelekea kwa kijasiri njia ya mafanikio.

Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye amesema hayo akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 jijini New York, Marekani.

Amesema Burundi inajaribu kuelekea njia hiyo ya kuvuna faida za  amani na usalama, utulivu na utangamano wa kijamii vilivyorejeshwa kutokana na mchango wa wananchi wa Burundi wenyewe, “lakini pia ni kwa mchango kutoka jumuiya ya kimataifa.

Rais Ndayishimiye amesema ni kwa mantiki hiyo wanapenda kuona utashi wa amani, udugu na haki kuwa ni suala linalowagusa watu wote ili kila mtu duniani aweze kuishi kwa amani na utu kikamilifu.

Amani DRC kupitia mchakato wa Nairobi

Rais huyo wa Burundi ambaye sasa in Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameomba Jamii ya Kimataifa iunge mkono mchakato wa Nairobi wenye lengo la kuleta amani ya kudumu mashariki mwa nchi Jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Halikadhalika ameomba Umoja wa Mataifa kusaidia kukabiliana na vikundi vya kigaidi ambavyo vinaanza kuingia kwenye baadhi ya maeneo ukanda wa Afrika Mashariki bila kusahau maeneo mengine ya dunia.

Amezungumzia kuwa tayari DRC ni mwanachama wa EAC kwa hiyo viongozi wa jumiuiya hiyo imeazimia kuleta utulivu kwenye taifa ili sema viongozi wa EAC wameweka lengo la kuleta utulivu kwenye ukanda mzima wa jumuiya hiyo ili hatimaye wakazi wa eneo hilo waweze kujikita katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mchakato wa Nairobi kwa taifa la DRC au Nairobi Conclave, ni mazungumzo yanayofanywa chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC ambayo tayari DRC ni mwanachama.

Mkutano wa kwanza ulifanyika Aprili 8 mwaka huu wa 2022 na mkutano wa pili ulifanyika tarehe 21 mwezi Aprili mwaka huu. Mikutano yote ilifanyika Nairobi Kenya na ni ya ngazi ya marais.

Reli kutoka Uvinza-Musongati-Gitega-Bujumbura-Uvira-Kindu

Akihusisha maendeleo hayo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi, Rais Ndayishimiye amezungumzia uboreshaji wa miundombinu ya usafiri wa anga, maji na barabara nchini mwake.

Ametaja mradi wa ujenzi wa usafirishaji kwa reli kutoka Uvinza, Musongati, Gitega, Bujumbura, Uvira hadi Kindu, akisema reli hii itaunganisha nchi tatu ambazo ni Tanzania, Burundi na DRC kwa upande wa baharí  ya India na Atlantiki.

“Mradi huu mkubwa wa reli utaleta sio tu maendeleo makubwa kwa uchumi wa nchi zetu tatu, bali pia utarahisisha usafiri wa watu na bidhaa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Rais Ndayishimiye.