Skip to main content

Tunahitaji ubia wa dunia wakati huu ambao mgawanyiko unazidi- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia ufunguzi wa mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN
UN /Cia Pak
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia ufunguzi wa mjadala mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN

Tunahitaji ubia wa dunia wakati huu ambao mgawanyiko unazidi- Guterres

Masuala ya UM

Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeanza hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amezungumza wakati wa ufunguzi akigusia masuala lukiki ikiwemo mgawanyiko wa kisiasa na kijiografia duniani, mizozo, uhaba wa chakula, ongezeko la gharama ya maisha, mabadiliko ya tabianchi na teknolojia akisema maendeleo yaliyofikiwa katika Nyanja mbali mbali yanakwamishwa na mgawanyiko wa kisiasa na kijiografia.

 

Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.
NASA
Picha ya sayari ya dunia kutumia sateliti. Mabadiliko ya tabianchi yanaiweka hatarini dunia na viumbe vilivyomo.

Amesema mgawanyiko huo unakwamisha kazi ya Baraza la Usalama kwenye utatuzi wa mizozo, unadumaza sheria za kimataifa. Unadumaza kuaminiana na imani ya watu kwa taasisi za kidemokrasia.

Makundi nje ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa yanameguka

Katibu Mkuu amesema hatuwezi kuendelea na hali hii. Hata makundi mbalimbali yaliyoundwa nje ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, baadhi ya wajumbe wa jamii ya kimataifa wametumbukia kwenye mtego wa mgawanyiko wa kisiasa na kijiografia kama kundi la G20.

Amesema kuna hatari ya kuishia kutokuwa na kundi lolote akitanabaisha kuwa “hakuna ushirikiano, hakuna mazungumzo, hakuna utatuzi wa pamoja wa matatizo. Lakini ukweli ni kwamba tunaishi kwenye dunia ambako mantiki ya ushirikiano na mazungumzo ndio jawabu la kusonga mbele. Tunahitaji ubia wa dunia.”

Kwa kuzingatia hali ya sasa ambayo amesema inatia wasiwasi mkubwa, ametaja mambo makuu matatu ambamo ushirikiano wa dunia lazima ushinde mgawanyiko na badala yake kuchukuliwe hatua za pamoja.

Taswira ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Katibu Mkuu António Guterres alipohutubia ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa UNGA77
UN /Cia Pak
Taswira ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Katibu Mkuu António Guterres alipohutubia ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa UNGA77

Chata ya UN itusaidie kuendeleza amani duniaini

Mosi ni jukumu la Umoja wa Mataifa la kufanikisha na kuendeleza amani endelevu duniani.

Amesema dunia hivi sasa imejikita kwenye uvamizi wa Urusi nchini Ukraine huku vita na majanga ya kibinadamu yakisambaa na kusahaulika. Ametaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Yemen, Syria na Afghanistan. Pembe ya AFrika, Ethiopia na Haiti.

Tunapaswa kuendelea kufanyia kazi suala la amani kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa huku akisema katika baadhi ya maeneo kuna nuru ya matumaini.

Nchini Yemen, mkataba wa sitisho la mapigano uko tete lakini angalau unafanya kazi. Huko Colombia, mchakato wa amani unaota mizizi.

“Tunahitaji hatua zaidi za pamoja ziote mizizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na tukiheshiu haki za binadamu,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “tunahitaji kujenga mifumo ya mashauriano ya kuponya migawanyiko,” akitaja moja ya mifumo hiyo kuwa Ajenda ya Pamoja aliyozindua mwezi Septemba mwaka jana wa 2021.

Mradi wa kurejesha mikoko huko Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya umesaidia kuepusha eneo hilo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.
UN/ Thelma Mwadzaya
Mradi wa kurejesha mikoko huko Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya umesaidia kuepusha eneo hilo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.

Hebu tuache kuua mazingira yetu

Jambo la pili amesema ni kumaliza ‘vita yetu ya kuua’ mazingira, akitanabaisha kuwa janga la tabianchi ndio jambo litakaloacha alama kwa zama za sasa.

Amesema ingawa umma duniani kote unaunga mkono hatua kwa tabianchi, bado suala hilo halipatiwi kipaumbele.  Licha ya kutakiwa kupungua, bado viwango vya utoaji wa hewa chafuzi vinaongezeka na mwelekeo ni kuongezeka kwa asilimia 14 muongo huu wa sasa.

Tunajiwekea mikutano na janga la tabianchi, amesema Guterres akieleza kuwa hivi karibuni ameshuhudia mwenyewe kwa macho yake nchini Pakistani ambako theluthi moja ya eneo la nchi imetwama kwenye maji kutokana na mvua za pepo za Monsuni.

“Tunaona kila mahali, sayari dunia ni muathirika wa sera za joto za dunia.” Madhara yake ni makubwa amesema, baa la njaa linanyemelea Pembe ya Afrika, viwango vya joto Kali Ulaya, China na Marekani. Kasi ya kuzalisha mafuta ya kisukuku nayo imeongezeka.

Katibu Mkuu amesema kwa mantiki hiyo hii leo natoa wito kwa nchi zenye uchumi wa juu duniani “kutoza kodi kampuni zinazozalisha mafuta ya kisukuku, na fedha hizo zieelekezwe kwa nchi zinazoathirika na janga la tabianchi na kwa watu wanaohaha kutokana na ongezeko la bei ya chakula na nishati.

Uzinduzi wa kichocheo cha SDGs

Jambo lingine alilosema linahitaji ushirikiano ni hatua za pamoja kukabili ongezeko la gharama ya maisha kuwahi kutoka likichochewa na vita nchini Ukraine.

Nchi zipatazo 94 zenye wakati bilioni 1.6, wengi wao barani Afrika wanakabiliwa na kimbuga: makali ya kiuchumi na kijmaii kutokana na janga la COVID-19, ongezeko la bei ya vyakula na nishati, mzigo wa madeni, mifumuko ya bei na ukosefu wa fedha.

Kaya moja ng'ombe mmoja bila gharama yoyote
UNEP-UNDP Rwanda/ Jan Rijpma
Kaya moja ng'ombe mmoja bila gharama yoyote

Amesema mvurugano wa kijamii haukwepeki, huku mizozo ikiwa inanyemelea. Haipaswi kuwa hivi, amesema Katibu Mkuu akieleza kuwa, dunia bila umaskini wa kupindukia, iliyojitosheleza na bila njaa si ndoto isiyowezekana. Ni jambo linalowezekana.

Dunia hiyo, amesema, ndio iliyomo kwenye Ajenda 2030 na Malengo ya Maendeleo endelevu, SDGs, lakini inaonekana ndoto kutokana na maamuzi yetu na waathirika wakubwa ni nchi zinazoendelea.

Katibu Mkuu amesema inahitajika hatua za pamoja, “na leo hii natoa wito wa kuzinduliwa kwa Kichocheo cha SDG, kikioongozwa na kundi la nchi 20, G20 ili kuchochea maendeleo endelevu kwa nchi zinazoendelea.”

Amesema mkutano ujao wa G20 utakaofanyika Bali, Indonesia ndio pa kuanzia.

 Na kichocheo hicho  pamoja na mambo mengine msamaha wa madeni na kuongeza kiwango cha fedha zinazotolewa na shirika la fedha duniani, IMF na Benki kubwa, bila kusahau kupanua wigo wa haki mahsusi za mikopo kwa nchi zinazoendelea ili ziwekeze kwenye kujikwamua na katika SDGs.