Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya Juakali ijumuishwe kwenye kauli ya kujikwamua upya kwa ubora- Ruto

Willliam Samoei Ruto, Rais Kenya akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York, Marekani 21- SEptemba 2022
UN /Cia Pak
Willliam Samoei Ruto, Rais Kenya akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York, Marekani 21- SEptemba 2022

Sekta ya Juakali ijumuishwe kwenye kauli ya kujikwamua upya kwa ubora- Ruto

Masuala ya UM

Rais William Ruto wa Kenya amesema kauli mbiu iliyozoeleka duniani ya kujenga upya kwa ubora baada ya janga la COVID-19 linapaswa kuongezewa sentensi ili ikamilike vizuri na kuwa na maana ya kufikia wale walio chini zaidi.

Akihutubia kwa mara ya kwanza Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 jijini New York, Marekani Rais Ruto amesema kauli hiyo lazima ikamilike kwa kusema Kujenga Upya kwa Ubora kuanzia chini na kujumuisha sekta ya juakali.

Juakali ‘hustlers’ wajumuishwe kwenye kauli hii

Kauli ya kujenga upya kwa ubora inalenga kujifunza kutoka makosa ya awali na kujenga uhimili na mnepo, “lakini nadhani tuna fursa  bora ya kuzingatia kauli hii kwa kuipaisha zaidi kwa neno na vitendo kwa kuongeza B nyingine yaani Building Back Better from the Bottom,” akimaanisha Tujenge Upya kwa ubora kuanzia chini.

Rais Ruto amesema kujenga upya kuanzia chini ni jambo jema kwa kuwa linahusisha kundi kubwa la wanaochangia kwenye uchumi lakini wameenguliwa.

“Watu bilioni waliooenguliwa wanahaha kujipatia kipato cha siku ili waweze kuishi kwenye maeneo ambayo hayana fursa,” amesema Ruto.

“Vipaji vyao, matumaini, mnepo na nguvu walizo nazo mara nyingine hutambulika kama kupambana,” amefafanua Ruto.

Juakali hawaonwi na watunga será lakini hawakati tamaa

Wakiwa hawaonwi na watunga sera na halifikiwi na huduma nyingi za umma, “juakali hawapuuzii chochote, wanapitia magumu na hatimaye mara nyingi hufanikiwa.”

Amenukuu kauli ya raia mmoja wa Marekani inayosema, “vitu vinaweza kuwafikia wale wanaosubiri, lakini ni vile tu vilivyoachwa na juakali.”

Rais huyo wa Kenya amesema ni “ni wakati wa kuimarisha mnepo wa taifa letu; kujumuisha juakali hawa kupitia mikakati ya makusudi na juhudi za uchumi jumuishi kwa Kujenga Upya kwa Ubora kuanzia chini.

Kunufaika na uchumi wa buluu- Kenya tuko makini

Rais Ruto ametumia pia hotuba yake kuelezea vile ambayo wamejiandaa kunufaika na uchumi wa buluu, au uchumi unaotokana na matumizi ya rasilimali za bahari akisema wamejifunza mengi baada ya mkutano wa mwaka 2018 wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari, mkutano uliofanyika nchini Kenya.

“Tunaendelea kupigia chepuo matumizi endelevu ya rasilimali za baharí kwa kutambua kuwa uwekezaji bora ni muhimu na unaweza kumaliza njaa, kupunguza umaskini, kuweka fursa za ajira na kuchochea ukuaji uchumi,” amesema Rais huyo wa Kenya.

Amesema Kenya tayari inapitia upya Mkakati wake wa kitaifa wa uchumi wa buluu, ili kuimarisha mifumo ya kijamii ya  usimamizi wa rasilimali za maji iwe kwenye maziwa, mito, pwani na baharini.

“Mkakati huu unatarajiwa kuchangia katika maendeleo yetu ya kiuchumi kupitia uhakika wa chakula na lishe bora, maendeleo ya kanda za pwani na vijijini na kuongeza kipato kupitia minyororo ya thamani ya bidhaa, usafirishaji wa bidhaa za bahari na utalii,” amesema Rais Ruto.