Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatangaza viongozi vijana 17 kusongesha SDGs, miongoni ni kijana Gibson kutoka Tanzania

Vijana viongozi 17 waliotangazwa leo na Umoja wa Mataifa kwa harakati zao za kusongesha SDGs
Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu vijana
Vijana viongozi 17 waliotangazwa leo na Umoja wa Mataifa kwa harakati zao za kusongesha SDGs

UN yatangaza viongozi vijana 17 kusongesha SDGs, miongoni ni kijana Gibson kutoka Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa umetangaza kundi la viongozi vijana 17 kutoka pande mbali mbali duniani ili kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, hatua iliyofanyika wakati huu ambapo mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN, UNGA77 unaendelea.

Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kuhusu vijana, ambayo ndio inasimamia mpango huu inasema uteuzi huu  hufanyika kila baada ya miaka miwili kutambua vijana waleta mabadiliko ambao wanaongoza hatua za kukabili changamoto kubwa zinazokabili dunia hivi sasa na kuchagiza SDGs.

Kati ya vijana 5,400 waliochaguliwa ni 17

Uteuzi wa vijana hao akiwemo Gibson Kawago mjasiriamali wa tabianchi kutoka Tanzania, ulitokana na tangazo lililotolewa mapema mwaka huu la kusaka vijana hao ambapo majina 5,400 kutoka nchi 190 yaliwasilishwa.

Maeneo ambayo vijana hao wanahusika nayo ni maendeleo endelevu, haki za binadamu, amani na usalama na walio miongoni mwa waliochaguliwa wana umri wa kati ya miaka 17 hadi 29, wakiwemo wasanii, wanaharakati wa mazingira, wachechemuzi wa masuala ya jinsia, wabunifu na wengine.

Vijana viongozi wameendelea kuwa wagunduzi hata katikati ya majanga

Akizungumzia uteuzi huo, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa UN kwa vijana, Jayathma Wickramanayake  amesema, “kundi hili la vijana viongozi wa SDGs kwa mwaka 2022 linajumuisha vijana ambao wanatekeleza hatua mbalimbali za uanaharakati wa vijana na uchechemuzi pindi linapokuja suala la kuhoji mamlaka na kujenga dunia bora kwa watu wote.”

Gibson Kawago kutoka Tanzania miongoni mwa vijana viongozi wa Umoja wa Mataifa wa kusongesha SDGs mwaka 2022 akiwa kwenye karakana yake ambako hutengeneza bidhaa za kuzalisha umeme kwa kutumia betri chakavu za kompyuta au nyinginezo.
Gibson Kawago
Gibson Kawago kutoka Tanzania miongoni mwa vijana viongozi wa Umoja wa Mataifa wa kusongesha SDGs mwaka 2022 akiwa kwenye karakana yake ambako hutengeneza bidhaa za kuzalisha umeme kwa kutumia betri chakavu za kompyuta au nyinginezo.

Amesema hata wakati wa janga la coronavirus">COVID-19, tabianchi na ukosefu wa utulivu duniani, vijana hao wameonesha mnepo, ugunduzi na kusaka majawabu bunifu kwa changamoto kubwa zinazokumba dunia.

Kauli ya Gibson Kawago

Miongoni mwao ni Gibson Kawago mwenye umri wa miaka 27 kutoka Tanzania, yeye ni mjasiriamali wa tabianchi na muasisi wa taasisi ya WAGA inayotengeneza betri aina ya lithium na Ion kutoka katika betri chakavu za kompyuta.

Bwana Kawago anasema, “vijana wana nguvu na uwezo wa kubaini changamoto, kutafuta teknolojia zilizoko na kuibuka na majawabu ya mnepo, safi na rafiki kwa mazingira. Sisi ndio mustakabali, na hivyo tunahitaji kusongesha SDGs.”

Bofya hapa kupata orodha nzima ya vijana viongozi wa SDGS.