Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Almasi Botswana ni baraka na si laana kama kwingineko- Rais Masisi

Rais Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi wa Botswana akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN
UN /Cia Pak
Rais Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi wa Botswana akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la UN

Almasi Botswana ni baraka na si laana kama kwingineko- Rais Masisi

Masuala ya UM

Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi amehutubia Mjadala Mkuu wa mkutano waw a 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77, na kusema marekebisho yoyote ya muundo wa Umoja wa Mataifa yatakuwa na maana kwa mataifa madogo kama Botswana pale tu yatakaporuhusu kila nchi kushiriki kwa usawa bila kujali ukubwa wao.

Katika hotuba yake ambapo alikuwa wa kwanza kuhutubia leo Alhamisi Septemba 22, Rais Masisi amesema, “mimi na serikali yangu tuna hamu ya kuona wananchi wetu wakiwakilishwa na wakiajiriwa ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, na kwa urais wetu wa Baraza la Uchumi na Kijamii, ECOSOC, naamini Botswana imeonesha uwezo wake ikiwemo uwezo wa vijana wetu ambao wamepatiwa tathmini nzuri kutokana na usaidizi wao kwa sekretarieti ya ECOSOC wakati wa awamu yetu.”

Raia wa Botswana Collen Vixen Kelapile alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la uchumi na kijamii la mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililomaliza kipindi chake wiki mbili zilizopita.

Almasi si laana kwa taifa iwapo itasimamiwa vizuri

Katika hotuba yake, Rais Masisi amegusia pia mchango wa almasi katika uchumi wa Botswana, taifa la kusini mwa Afrika ambalo hivi limevuka kutoka kuwa nchi maskini au nchi ya kipato cha chini na kuwa nchi ya kipato cha kati.

Rais Masisi amewaambia viongozi wanaoshiriki mjadala huo kuwa, «wengi kwenye chumba hiki mnaweza kutambua tu Botswana ya leo ambayo ni nchi ya ngazi ya juu ya kipato cha kati. Hii ni hadhi ambayo tunajivunia nayo kwa sababu tulipopata uhuru miaka 56 iliyopita tulikuwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani. Lakini tulibahatika kubaini kile kilichobainika hivi sasa duniani kuwa ni hifadhi kubwa zaidi ya machimbo ya madini ya almasi kwenye ukanda wa Kimberley. »

Viongozi watangulizi waliweka msingi mzuri wa kusimamia Almasi

Amesema simulizi nzuri ya sasa ya Botswana ni simulizi ya busara za viongozi wetu waliotangulia ambao waliepuka ‘nuksi’ au laana ambayo mara nyingi hufuatia ugunduzi na uchimbaji wa madini katika maeneo mengine duniani.

« Viongozi wetu waliotangulia walichagua badala yake kugeuza simulizi ya kuwa na madini ya almasi kuwa simulizi ya maendeleo, » amesema Rais huyo wa Botswana.

Amesema Botswana kama taifa lisingaliweza kufanikiwa maendeleo yake iwapo lisingaliwa kuwa linalinda na kutetea misingi ya demokrasia iliyojikita kwenye utawala wa sheria, na utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu kwa watu wake.

Tunatekeleza Ajenda ya Pamoja ya Guterres

Rais Masisi amepongeza Ajenda ya Pamoja iliyozinduliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mwaka jana akisema Botswana inaizingatia kwa makini kwa kuhakikisha rasilimali yake adhimu ya almasi inatumiwa kwa maslahi na maendeleo endelevu kwa wananchi wake.

« Nakumbusha chombo hiki adhimu kuwa simulizi ya Botswana ni ushahidi usio na shaka na ulio hai ya kwamba almasi ikisimamiwa vizuri ni kwa maendeleo. Ni kwamba almasi ni suala makini la kujipatia kipato. »

Pamoja na hayo amekiri kuwa wanapata changamoto kubwa ya kuvutia wawekezaji kusaidia kupanua wigo wa sekta ya uchumi  badala ya kutegemea almasi pekee, lakini wataendelea kutumia kila jukwaa kusaka wawekezaji kwenye sekta nyingine.