Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu bado Afrika haina ujumbe wa kudumu Baraza la Usalama- Congo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Congo, Jean-Claude Gakosso akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 26 Septemba 2022
UN /Cia Pak
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Congo, Jean-Claude Gakosso akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa 26 Septemba 2022

Ajabu bado Afrika haina ujumbe wa kudumu Baraza la Usalama- Congo

Masuala ya UM

Jamhuri ya Congo imesema ni ajabu ya kwamba Afrika ambayo ushiriki wake katika masuala ya kimataifa ni dhahiri lakini bado haijpatiwa nafasi ya kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kauli hiyo ya Congo-Brazaville imetolewa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Jean-Claude Gakosso wakati akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, leo Jumatatu ikiwa ni siku ya sita.

Bwana Gakosso amesema marekebisho ya Baraza la Usalama yamesalia kuwa mjadala usio na mwisho na ambao kila uchao unatokomea bila suluhisho.

“Afrika lazima ichukue nafasi yake katika jamii ya kimataifa, na kufikiria vinginevyo ni kuonesha ubinafsi na kwenda kinyume na mwelekeo wa historia,” amesema Bwana Gakosso.

Waziri huyo wa Jamhuri ya Congo amesema kuendelea kukwepa wazo la kujumuisha nchi mbili za Afrika kama wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni sawa na “kuchagua kwa utashi kuwekea sifa mbayá chombo chetu adhimu.”

Amesema “sisi wawakilishi wa nchi washirika tunaokutana hapa kwenye Umoja wa Mataifa lazima tuchague heshima leo na siku zote tuondokane na fikra potofu za zama za kale kuhusu Afrika, fikra ambazo kwa muda mrefu zimedhalilisha eneo hili la dunia.”

Vikwazo dhidi ya Cuba

Waziri Gakosso ametumia pia hotuba yake kuzungumzia vikwazo dhidi ya Cuba ambavyo amesema vinaendelea kusababisha machungu kwa wananchi wake. Vikwazo hivi vingalikuwa vimefutiliwa mbali siku nyingi.

“Kwa niaba ya nchi yangu natoa wito kutoka mimbari hii kwa busara ya wananchi wa Marekani na viongozi wake, viongozi ambao kama tunavyojua hawana lolote wanalohusiana nalo na vikwazo hivi vya zama za vita baridi.