Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani Cabo Delgado inaimarika, asanteni wadau- Msumbiji

Waziri Mkuu wa Msumbiji Adriano Afonso Maleiane akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa
UN /Cia Pak
Waziri Mkuu wa Msumbiji Adriano Afonso Maleiane akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa

Amani Cabo Delgado inaimarika, asanteni wadau- Msumbiji

Masuala ya UM

Tumefikia maendeleo makubwa katika kutokomeza ugaidi kwenye jimbo la Cabo Deldago nchini Msumbiji, amesema Waziri Mkuu wa Msumbiji, Adriano Afonso Maleiane wakati akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo, ikiwa ni siku ya tano ya mkutano huo.

Bwana Maleiane amesema maendeleo hayo yanatokana na hatua ambazo Msumbiji yenyewe imechukua ikiwemo kuimarisha vikosi vyake ya usalama pamoja na huduma za maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili kupunguza hali ngumu ya maisha inayoweka hatarini wananchi kutumbukia kwenye ugaidi.

Shukrani SADC, EU na Rwanda

Ameongeza pia mafanikio hayo ni pamoja na usaidizi wa kikanda na kimataifa akitaja Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC, Muungano wa Ulaya, EU pamoja na serikali ya Rwanda, ambayo ilipeleka vikosi vya kijeshi huko Cabo Delgado.

“Hatua iliyochukua Msumbiji katika kukabili ugaidi duniani ni ya aina yake kwa minajili ya kuwa hatua ya pamoja ya kikanda  na kwamba harakati zinazoendelea Cabo Delgado zinawezesha kurejesha hali ya usalama na hatimaye wananchi waweze kurudi kwenye makazi yao,” amesema Waziri Mkuu Maleiane.

Amesema hatimaye kupitia mpango wa ujenzi mpya wa Cabo Delgado, shughuli za kiuchumi na kijamii zitaendelea tena kwenye  maeneo ambayo awali yaliathiriwa na ugaidi.

“Tunatoa shukrani kwa wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wamesaidia Msumbiji kukabili ugaidi; kutoa msaada wa kibinadamu na kusaidia kujenga miundo ya kijamii na kiuchumi kwenye maeneo yaliyoathirika,” amesema Waziri Mkuu huyo.

Mgao wa kuku kutoka FAO kwa ajili ya ufugaji kwa wakazi wa  Cabo Delgado nchini Msumbiji waliokumbwa na dharura kufuatia mapigano kwenye eneo hilo.
©FAO/Fábio de Sousa
Mgao wa kuku kutoka FAO kwa ajili ya ufugaji kwa wakazi wa Cabo Delgado nchini Msumbiji waliokumbwa na dharura kufuatia mapigano kwenye eneo hilo.

Kujisalimisha kwa RENAMO,asante UN na wadau

Amegusia pia mchango wa Umoja wa Mataifa katika kufanikisha mpango wa kuwezesha wapiganaji wa zamani wa RENAMO kujisalimisha, kukabidhi silaha na kujumuishwa pia kwenye jamii, DDR.

Amesema hadi leo hii wapiganaji wa zamani 4,002 katiya 5,221 wamepitia mchakato huo na kwamba matarajio ifikapo mwishoni mwa mwaka mchakato wa DDR utakamilika, jambo ambalo litakuwa ni muhimu sana katika kukamilisha Mkataba wa Kitaifa wa amani na maridhiano uliotiwa saini tarehe 6 mwezi Agosti mwaka 2019 kati ya serikali ya Msumbiji na RENAMO.

Amesema, “kukamilika kwa hatua hii tutaweza kujikita katika mipango ya muda mrefu ya ujumuishaji ambayo ni muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa mchakato wa amani na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Kituo cha SADC cha kuratibu dharura za tabianchi

Ujenzi wa nyumba zinazohimili mabadiliko ya tabianchi huko Msumbiji baada ya miji ya pwani kupigwa na vimbunga Idai na Kenneth.
UN-Habitat/Veridiana Mathieu
Ujenzi wa nyumba zinazohimili mabadiliko ya tabianchi huko Msumbiji baada ya miji ya pwani kupigwa na vimbunga Idai na Kenneth.

Waziri Mkuu huyo amewaeleza washiriki kuwa mabadiliko ya tabianchi yameweka Msumbiji katika ufuatiliwaji wa kudumu kwa kuwa hivi karibuni imekumbwa na vimbunga, mvua kubwa, mafuriko na ukame, majanga ambayo yamesababisha vifo na uharibifu wa mali na miundombinu.

“Kati ya mwaka 2019 na 2022, Msumbiji imepigwa na vimbunga, Idai, Kenneth, Guambe, Chalane, Ana na Gombe,” amesema Bwana Maleiane.

Hata hivyo amesema ili kukabili changamoto zinazohusiana na upunguzaji na usimamizi wa majanga ya asili, “Msumbiji kwa uratibu na nchi za kusini mwa Afrika na wadau tumeanzisha mwaka 2021, kaskazini mwa nchi kituo cha operesheni za kibinadamu na dharura cha SADC.”

Amesema kituo hicho kinalenga kupatia nchi za SADC mbinu na taasisi zenye uwezo wa kushughulikia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na dharura nyingine zinazohitaji hatua za haraka, zilizoratibiwa na kwa wakati kwa nchi yoyote ile mwanachama.