Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jarida la Habari

08 Machi 2021

Hii leo Jumatatu Machi Nane ni siku ya wanawake duniani na jarida letu leo limejikita na siku hiyo tukimulika wanawake katika habari yetu kwa ufupi halikadhalika mashinani. Na kwa kuwa ni jumatatu, tuna mada kwa kina na leo tunakwenda nchini Tanzania kwake Ramlat Omar kijana wa kike ambaye anasimulia ni vipi amebadilika kutoka kuwa msichana hatarishi kwenye jamii yake hadi kuwa mkombozi na mjasiriamali wa kupita mlango hadi mlango kunusuru siyo tu vijana wa kike kama yeye bali pia wa kiume na vile vile wanawake kupitia mbinu alizopata kutoka shirika la kiraia la Restless Development.

Sauti
13'24"

05 Machi 2021

Hii leo jaridani ni mada kwa kina tunakwenda Tanzania ambako mhitimu wa Chuo Kikuu aweka alichosomea pembeni na kuanza kutumia kalamu ya wino kuchora picha, kulikoni? Habari kwa ufupi imesheheni taarifa kuhusu saratani, Corona na ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis nchini Iraq na leo katika kujifunza kiswhahili ni uchambuzi wa methali, Chozi la akupendaye hutoka kwenye chongo au kengeza! Karibu basi na mwenyeji wako ni Flora Nducha.

Sauti
15'48"

03 Machi 2021

Hii leo jaridani tunamulika siku ya usikivu wa masikio duniani halikadhalika siku ya wanyamapori duniani. Kumbuka kuwa mtu mmoja kati ya wanne yuko hatarini kupoteza uwezo wa sikio lake kusikia. Je wewe unatunza sikio lako namna gani? Kuhusu wanyamapori, wito unatolewa kutunza misitu kwani ndio makazi siyo tu ya wanyamapori bali pia ni chanzo cha bayonuai bora kwa uhai wa viumbe vyote na sayari dunia. Kisha ni TANZBATT_!3 tukimulika Sajini Mkamati yeye akionesha mchango wa wanawake katika ulinzi wa amani, katika kuelekea siku ya wanawake duniani wiki ijayo.

Sauti
11'59"

02 Machi 2021

Hii leo jaridani, Flora Nducha anaanzia huko Somaliland ambako Umoja wa Mataifa umepeleka mashine za kuwezesha wagonjwa kuvuta hewa ya oksijeni wakati huu hospitali zimezidiwa kutokana na  janga la COVID-19 linaloleta mkwamo kwa wagonjwa kupumua. Kisha anammulika Mkurugenzi Mkuu mpya wa shirika la biashara duniani, WTO, Ngozi Okonjo-Iweala ambaye amenaza rasmi jukumu lake akiwa mwanamke wa kwanza na pia mwafrika wa kwanza kushika wadhifa huo.

Sauti
14'3"

01 Machi 2021

Hii leo jumatatu ya Machi Mosi ni mada kwa kina tukimulika mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa huko nchini kenya ambaye anatumia taka za plastiki kutengeneza matofali ya kutengenezea barabara Lakini kuna muhtasari wa habari ukimulika ubaguzi duniani, mwandishi wa habari kufariki dunia baada ya kuswekwa rumande huko Bangladesh na shambulizi huko Yemen. Mashinani tunaangazia COVID-19 na UKIMWI. Karibu na mwenyeji wako ni Flora Nducha.

26 Februari 2021

Leo Ijumaa ni mada kwa kina ikijikita huko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako walinda amani wanawake kutoka Tanzania wakihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa. Walinda amani hao chini ya TANZBATT_8 wamefanya ziara na kukutana na wanawake wa maeneo mbalimbali ikiwemo Matembo.

Sauti
11'11"

25 Februari 2021

Jaridani hii leo Flora Nducha anamulika teknolojia na hatua ambazo serikali zinapaswa kuchukuliwa ili ziweze kunufaisha kila mtu na zilete maendeleo ya watu. Watunga sera wakiwemo wabunge wana jukumu lao, ni kutoka UNCTAD. Kisha anakwenda Tanzania hususan mkoani Kigoma ambako kilimo hifadhi charipotiwa kurejesha ujana kwa wakulimia, kivipi? Na mwisho ni kule Uganda ambako msichana mmoja anasema ingawa janga la COVID-19 limemwachia kilema cha kutokuwa na mguu lakini katu halitapora ndoto yake ya maisha. Makala tunamulika matumizi ya dawa za kuuawa wadudu kwenye mboga za majani.

24 Februari 2021

Hii leo jaridani tunaanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako wananchi licha ya madhilla wanayopitia mashariki mwa nchi hiyo wanashikamana na wanasaidiana ili angalau kupunguza machungu. Kisha ni suala la mgao wa mlo shuleni ambao sasa umekwenda mrama kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. Huko Amerika ya kati hali ya chakula nayo ni tabu. Makala leo tunamalizia mahojiano yetu na mtaalamu wa lishe huko Njombe mkoani Tanzania kuhusu umuhimu wa matunda mwilini tukizingatia mwaka wa kimataifa wa matunda na mboga mboga.