Mashariki ya Kati
“Tunaweza kufikia mustakabali ulio na Israel salama na iliyoko kando mwa taifa la Palestina linaloweza kujiendesha na lililo huru. Hii inahitaji juhudi endelevu, za kujitolea na ujasiri wa kisiasa kutoka kwa pande zote."
Sigrid Kaag, Kaimu Mratibu Maalum wa UN kwa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati alipohutubia Baraza la Usalama Februari 2025
MAELEZO
Umoja wa Mataifa unashirikiana na wadau wa kikanda na kimataifa katika juhudi zake za kuondoa mvutano, huku ukihamasisha kuimarika kwa hali bora kwenye eneo hilo, na kusongesha mashauriano ya kisiasa ili hatimaye kutimia kwa jawabu la kuweko kwa mataifa mawili yaani Israeli na Palestina pamoja na amani ya kina, ya kudumu Mashariki ya Kati.
UN NA SUALA LA PALESTINA
Katibu Mkuu
Katibu Mkuu huchukua hatua yeye mwenyewe binafsi au kupitia wajumbe wake kwa maslahi ya diplomasia ya kuzuia mizozo, kusaka amani na ujenzi wa amani Mashariki ya Kati. Halikadhalika yeye huwakilisha Umoja wa Mataifa kwenye mazungumzo ya pande nne kuhusu Mashariki ya Kati, Quartet. Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati humwakilishi Katibu Mkuu kwenye masuala yote yanayohusu mchakato wa amani.
Baraza Kuu
Baraza Kuu la UN , linaloundwa na wajumbe wote wanachama wa Umoja wa Mataifa, limekuwa likijihusisha na katika kusaka suluhu ya amani kwenye Suala la Palestina tangu mwaka 1947. Kamati ya kusimamia Haki zisizopingika za Watu wa Palestina ilianzishwa na Baraza Kuu mwaka 1975.
Baraza la Usalama
Baraza la Usalama lina wajibu wa msingi wa kulinda amani na usalama duniani. Baraza limeshughulikia suala la Mashariki ya Kati na Suala la Palestina katika matukio kadhaa.
UNRWA
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, (UNRWA) kwa kiasi kikubwa ndio lenye operesheni kubwa zaidi za Umoja wa Mataifa huko Mashariki ya Kati, likitoa huduma za afya, elimu, misaada na huduma za kijamii kwa zaidi ya wakimbizi milioni 5 wa kipalestina walioko Jordan, Lebanon, Syria, Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwemo Yerusalemu Mashariki.
UNTSO
Hili ni shirika la Umoja wa Mataifa la kusimamia Mikataba, (UNTSO) liliidhinishwa na Baraza la Usalama huko Palestina mwaka 1948, operesheni ya kwanza ya ulinzi wa amani kuanzishwa na Umoja wa Mataifa.
Baraza la Haki za binadamu
Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu limeshughulikia suala la Palestina wakati wa vikao vyake vya kawaida na maalum. Hufanya kazi kwa karibu na Mtaalamu Maalum kuhusu hali ya haki za binadamu kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa tangu 1967.
UNSCO
UNSCO ni ofisi inayomwakilishi Katibu Mkuu na huongoza mfumo wa Umoja wa Mataifa kwnye juhudi zote za kisiasa na kidiplomasia zinazohusiana na mchakato wa amani ikiwemo Mazungumzo ya pande nne (Quartet). UNSCO pia huratibu kazi za kiutu na maendeleo za mashirika ya Umoja wa Mataifa na program kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa na Israeli, kwa kusaidia mamlaka za Palestina na wapalestina.