Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ROHINGYA

Rohingya

Wakimbizi warohingya
WFP/Saikat Mojumder

“Hadi Jumatano ya wiki hii, zaidi ya warohingya 500,000 kutoka Myanmar wamesajliwa katika operesheni ya pamoja iliyoendeshwa na mamlaka za Bangladesh na UNHCR,”

Andrej Mahecic, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR mjini Geneva, Uswisi.

HALI HALISI

Mzozo katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ulishika kasi zaidi mwezi Agosti mwaka 2017 kufuatia ghasia dhidi ya waislamu wa kabila la Rohingya. Vikosi vya serikali vimekuwa vinadai kuwa operesheni hizo zinalenga kuondoa magaidi. Hata hivyo mamia ya maelfu ya raia wamekumbwa na ukatili wa kutisha, ikiwemo kushuhudia mauaji, kubakwa na hata mali zao kuharibiwa. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa tangu Agosti mwaka jana hadi hii leo zaidi ya warohingya 700,000 wamekimbilia nchi jirani  ya Bangladesh.

 

JUHUDI ZA UMOJA WA MATAIFA KUSAKA SULUHU

Tangu kuanza kwa mzozo huo, Umoja wa Mataifa na wadau wake wamekuwa mstari wa mbele kusaka suluhu ya kudumu. Suala la utaifa miongoni mwa warohingya ni moja ya tatizo ambapo wengi wao hawana utaifa. Hoja ya kutekeleza mpango wa utatu kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, serikali ya Bangladesh na Myanmar wa kurejeshwa kwa hiari nyumbani warohingya nayo bado haijapata nuru kutokana na hofu ya kule ambako wakimbizi hao watarejea. Hayo yakiendelea mazingira duni katika kambi wanamoishi huko Bangladesh na maeneo walikojificha huko Mynmar nako ni wasiwasi mkubwa. Hivi karibuni  msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu masuala ya kisiasa Miroslav Jenča, alipigia chepuo umuhimu wa kupatia suluhu suala la utaifa huku Kamishna mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi akisisitiza suala la kuweka mazingira bora kabla ya warohingya kurejea nyumbani ili kuwahakikishia siyo tu usalama bali ustawi endelevu.

HABARI ZA UN KUHUSU ROHINGYA

Bofya hapa kupata habari za Umoja wa Mataifa kuhusu Rohingya.

HATUA ZA KIBINADAMU

Kwa sasa, pepo za monsuni katika baharí ya Hindi zikitishia usalama wa warohingya huko Bangladesh, Umoja wa Mataifa unazidi kupaza ombi la misaada ya kibinadamu. UNHCR imeshaonya kuwa hali itakuwa mbaya kwa warohingya waliosaka hifadhi kwenye kambi za Kutupalong na Balukali bila kusahau wilaya ya Cox’s Bazar. Wakati serikali ya Bangladesh inajiandaa kukabili hali itakayotokea wakati wa pepo hizo za msimu, mashirika ya kibinadamu na Umoja wa Mataifa wameandaa kundi maalumu la dharura litakalotoa huduma za kudhibiti na kutibu magonjwa ya kuambukiza, kuimarisha malazi na pia kujenga vituo vya muda vya afya na vyoo.

Kuwa mkimbizi sio kukosa matumaini kwa wanawake wa Rohingya: UNHCR
Uteketezaji wa Rohingya unaendelea Myanmar:Gilmour
Wakimbizi hususan watoto wasirejeshwa Myanmar iwapo mazingira si mazuri-UNICEF