Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa ajira wamchochea kufuata kipaji anachotumia kuelimisha jamii kuhusu usawa wa jinsia

Msanii huyu Anna Nkyalu kutoka Tanzania anatumia kipaji chake kusongesha usawa wa jinsia.
UN/Ahimidiwe Olotu
Msanii huyu Anna Nkyalu kutoka Tanzania anatumia kipaji chake kusongesha usawa wa jinsia.

Ukosefu wa ajira wamchochea kufuata kipaji anachotumia kuelimisha jamii kuhusu usawa wa jinsia

Wanawake

Kuelekea siku ya wanawake duniani tarehe 8 mwezi huu wa Machi tunaelekea nchini Tanzaina ambako msichana mmoja mhitimu wa Chuo Kikuu amejikuta akiendeleza kipaji chake cha kuchora picha badala ya kubeba chaki kufundisha wanasayansi kutokana na ukosefu wa ajira, hatua ambayo imemfungulia milango mingi zaidi.

Msichana huyo si mwingine bali ni Anna Nkyalu ambaye alisomea ualimu wa masomo ya Kemia na Bailojia katika Chuo Kikuu nchini Tanzania.

Akihojiwa na Ahimidiwe Olutu wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam, UNIC nchini Tanzaina, Anna amesema, "nafanya sanaa ya kuchora michoro mbalimbali lakini natumia kalamu au peni. Sanaa ya kalamu au peni ni sanaa ambayo watu wengi wanaona ni ngumu kwa sababu unavyotumia kalamu hauwezi kufuta na hata kama ukifuta, inabidi nihakikishe sikosei na hata kama nikikosea basi niyakubali makosa na yawe katika mfumo ambayo yanaweza kuvutia kwa mtazamaji."

Kwa nini aliachana na chaki na kubeba kalamu

Alipoulizwa kitu gani kilimsukuma kuchora, Anna anasema amekuwa anapenda kuchora tangu akiwa mdogo hadi hata alipokuwa elimu ya juu lakini kuchora hasa kwa ajili ya kipato ilikuja baada ya kukosa ajira alipohitimu Chuo Kikuu. "Kwa ule muda wote ninafanya nimeanza mwaka 2019 baada ya kumaliza chuo kutokana na changamoto za ajira nikaamua kufanya hii sanaa kama sehemu ya kunipatia kipato. Kama mtu akitokea akitaka nimchoree picha au kama kuna picha nimeichora na mtu akaiona akaipenda akainunua basi ikawa ndio sehemu ya kazi yangu kuanzia mwaka huo wa 2019."

Soundcloud

Anna amesema anakumbana na changamoto lukuki katika kazi yake hii ya usanii wa picha kwa kuwa "imeshazoeleka kuwa wasichana hawawezi kufanya vitu vikubwa na vizuri kama wanaume. Akiona unakutana na watu wengi hususan wanaume ni wengi kwenye hii fani, na wasichana ni wachache. Na mtu akiona msichana hakuchukulii uzito au hakuamini. Huku familia nayo inakuwa ina wasiwasi kwamba mtoto wetu vipi huyu anapoteza muda. Kwa hiyo hizo ni changamoto."

Nimesoma ualimu Chuo Kikuu ili kufundisha Kemia na Bailojia lakini sasa natumia kalamu kuchora picha na kutumia ujumbe kwa jamii- Anna Nkyalu, Msanii

Kuhusu gharama ya picha zake, Anna amesema inategemea mnunuzi kama ni mzawa au ni mtalii akisema wazawa wengi bado hawajatambua uzito wa kazi za sanaa na pia gharama huendana pia na ukubwa wa picha lakini kwa watalii huuza kuanzia dola 100 za kimarekani na kuendelea.

Tweet URL

Picha iliyomgusa zaidi

Alipoulizwa picha ambayo imemgusa zaidi katika kazi zake zote ambazo amewahi kuzifanya, Anna ametaja picha aliyoipatia jina Komesha Ukatili dhidi ya wanawake ikionesha sura ya mwanamke akiwa amezibwa mdomo huku vidole vya mkono huo vikiwa vimechorwa maua, fedha na bunduki. Anna anasema, "hii picha nimechora kupinga unyanyasaji wa wanawake kwenye jamii yangu, kama unavyoona hapa ni mwanamke amefungwa na pesa, dini, bunduki na maua na zawadi kama upendo ili asiongee kutokana na manyanyaso anayokutana nayo."

Amesema picha hiyo imetengeneza badiliko, ni ujumbe binafsi kwa jamii kuwa "tunaweza kujitoa kwenye unyanyasaji sisi wanawake, na jamii pia inaweza kuacha kuwanyanyasa wanawake kwa kutowazuia wasiongee. Mazungumzo ndio njia nzuri ya kutatua matatizo kuliko kumfanya mtu asiongee kuhusu vile vitu anavyohisi ndani na vinazidi kumnyanyasa hususan ukatili."