Asubuhi, Baraza la Usalama lilikutana kusailia hali katika Afrika Magharibi. Haile Menkerios, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa alipohutubia Baraza la Usalama alizungumzia juu ya ziara yake ya karibuni katika Guinea na maeneo jirani, iliokusudiwa kuandaa utaratibu wa kulisaidia Bodi la Uchunguzi la UM kuendeleza ukaguzi wa vyanzo vya fujo ziliozuka nchini tarehe 28 Septemba mwaka huu. Alisema wadau husika wengi nchini Guinea pamoja na kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi kwa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) wote, kwa pamoja, wanaunga mkono rai ya kuanzisha Bodi la Uchunguzi la kimataifa litakaloshughulikia tukio la Septemba. Baada ya mkutano wake na Baraza la Usalama, Menkerios alizungumza na waandishi habari waliopo Makao Makuu, ambao aliwaeleza kuhusu dhamira ya KM ya kuanzisha uchunguzi wa vurugu la Guinea haraka iwezekanavyo, pindi atapatiwa idhini ya kuyafanya hayo na Baraza la Usalama. Menkerios alisema Raisi wa Guinea, Dadis Camara amemuahidi kuwa atashirikiana kikamilifu na tume ya uchunguzi ya UM.