Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Asubuhi, Baraza la Usalama lilikutana kusailia hali katika Afrika Magharibi. Haile Menkerios, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Kisiasa alipohutubia Baraza la Usalama alizungumzia juu ya ziara yake ya karibuni katika Guinea na maeneo jirani, iliokusudiwa kuandaa utaratibu wa kulisaidia Bodi la Uchunguzi la UM kuendeleza ukaguzi wa vyanzo vya fujo ziliozuka nchini tarehe 28 Septemba mwaka huu. Alisema wadau husika wengi nchini Guinea pamoja na kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi kwa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) wote, kwa pamoja, wanaunga mkono rai ya kuanzisha Bodi la Uchunguzi la kimataifa litakaloshughulikia tukio la Septemba. Baada ya mkutano wake na Baraza la Usalama, Menkerios alizungumza na waandishi habari waliopo Makao Makuu, ambao aliwaeleza kuhusu dhamira ya KM ya kuanzisha uchunguzi wa vurugu la Guinea haraka iwezekanavyo, pindi atapatiwa idhini ya kuyafanya hayo na Baraza la Usalama. Menkerios alisema Raisi wa Guinea, Dadis Camara amemuahidi kuwa atashirikiana kikamilifu na tume ya uchunguzi ya UM.

Susana Malcorra, Naibu KM juu ya Masuala ya Ulinzi Amani katika Idara ya Operersheni za Amani za UM (DPKO) wiki hii anayatembelea Makao Makuu ya Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) yaliopo El Geneina, Darfur Magharibi. Alipokuwepo huko alizungumza na walinzi amani wa UNAMID na aliwahimiza kujitahidi, kadiri wawezavyo, kuwalinda na kuwahifadhi wafanyakazi wa UNAMID na raia wa Darfur, hasa katika kipindi kigumu cha hivi sasa.

John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa Kufarajia Misaada ya Dharura sasa anazuru Uganda kwa siku nne. Ijumatano Holmes alizuru jimbo la Acholi kaskazini, na alikutana na raia waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano, na pia kuonana na wenyeji wao, na aliwasiliana na maofisa wa utawala wa kienyeji na kutoka serikali za jimbo, halkadhalika. Vile vile Holmes alikutana na watumishi wa UM na wale wenye kuwakilisha mashirika yasio ya kiserikali. Ripoti za Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura inasema Holmes aliingiwa moyo kuhusu maendeleo alioyoyaona Uganda Kaskazini akilinganisha na ziara yake ya mwisho huko mnamo miaka miwili iliopita. Licha ya hayo Holmes alisisitiza umma dhaifu wa eneo hilo, bado unahitajia kufadhiliwa misaada maridhawa ya kimsingi na jumuiya ya kimataifa, ili kuwawezesha kurudi makwao na kustarehea mazingira ya utulivu na amani.

Ripoti mpya iliochapishwa bia na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) na Benki Kuu ya Dunia juu ya uchanjaji watoto wachanga duniani imeeleza kwamba idadi kubwa ya watoto wameweza kupatiwa tiba ya chanjo dhidi ya maradhi, kuliko wakati wowote mwengine kihistoria. Kadhalika, iliripotiwa maendeleo makubwa yamepatikana katika utengenezaji wa tiba ya chanjo duniani, kadhia ambayo imeonyesha ustawi mkubwa kabisa. Takwimu za ripoti zimeeleza kwamba watoto wachanga milioni 108 walifanikiwa kupatiwa chanjo kinga duniani, dhidi ya maradhi, katika mwaka 2008. Lakini hata hivyo, ripoti ilikumbusha bado kunahitajika mchango wa dola bilioni moja kila mwaka kuweza kukamilisha, kwa mafanikio, kampeni za kuwachanja watoto wachanga ziada dhidi ya maradhi, katika zile nchi 72 zilizo maskini sana. Matibabu ya chanjo za kuhifadhi maisha, ambayo hupatikana kwa urahisi katika nchi tajiri, ripoti ilitilia mkazo, hunyimwa watoto wachanga milioni 24 katika dunia, fungu ambalo ndilo lenye kukabiliwa zaidi na hatari ya maambukizo ya magonjwa yanayosumbua watoto wa umri mdogo.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) limetangaza Ripoti mpya kuhusu Maendeleo ya Wanadamu kwa Mataifa ya Amerika ya Kati. Ripoti ilieleza ya kuwa eneo la Amerika ya Kati ni moja ya maeneo ya dunia yenye vurugu kubwa kabisa na ambapo matumizi ya nguvu yamekuwa mambo ya kawaida. Kwa mujibu wa UNDP, hali ya wasiwasi na ukosefu wa usalama katika Amerika ya Kati ni mzigo mkubwa kuumudu kwa wenye madaraka, hususan katika kipindi mataifa ya eneo yanajitahidi kudhibiti huduma za maendeleo. Lakini UNDP inaamini tatizo la vurugu linaweza kurekibishwa, kwa mafanikio, pindi mfumo wa kidemokrasia utatekelezwa kama inavyopaswa, na kuhishimiwa na wote katika Amerika ya Kati.