Skip to main content

UM inaunga mkono rai ya kuhishimu kikamilifu "mfumo wa kikatiba" kuambatana na uchaguzi wa Afghanistan

UM inaunga mkono rai ya kuhishimu kikamilifu "mfumo wa kikatiba" kuambatana na uchaguzi wa Afghanistan

Asubuhi KM Ban Ki-moon aliwaambia waandishi habari waliopo Makao Makuu kuwa anaikaribisha taarifa ya Raisi wa Afghanistan Hamid Karzai, ilitilia mkazo umuhimu wa kuhishimu na kufuata kanuni za katiba kuhusu uchaguzi, ambapo pindi wagombea uraisi watashindwa kupata asilimia inayohitajika, itabidi uchaguzi urudiwe tena ili kumpata mshindi halali.

KM alisema UM utafanya kila iwezalo kusaidia usimamizi wa duru ya pili ya uchaguzi wa uraisi Afghanistan, unaotarajiwa kufanyika tarehe 07 Novemba mwaka huu, kuhakikisha unakuwa ni huru na wa haki, na wenye uwazi unaoridhisha, na unafanyika kwenye mazingira yalio salama. Alisema ustahamilivu na ujasiri walionyesha umma wa Afghanistan wakati wa duru ya awali ya uchaguzi ni lazima utambuliwe na kupongezwa. Aliongeza kusema UM umeunga mkono mchango wa taasisi za Afghanistan kwenye zile juhudi za kuhakikisha kura zote halali zilizopigwa kwenye uchaguzi wa tarehe 20 Agosti zilihisabiwa, na sauti ya umma wa Afghanistan ilipewa usikizi unaofaa.