Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtetezi Haki za Binadamu wa UM alalama, jamii ya kimataifa yawavunja moyo wahamiaji wa ndani wa Usomali

Mtetezi Haki za Binadamu wa UM alalama, jamii ya kimataifa yawavunja moyo wahamiaji wa ndani wa Usomali

Walter Kaelin, Mjumbe wa KM juu ya Masuala Yahusuyo Haki za Binadamu za Wahamiaji wa Ndani Waliong\'olewa Makazi, amekamilisha ziara ya wiki moja nchini Usomali kutathminia hali ya umma ulionaswa kwenye vurugu liliopamba katika taifa hili la Pembe ya Afrika.

Alinakiliwa akisema kutokea Nairobi, hii leo, kwamba "jamii ya kimataifa imewakatisha tamaa na kuwavunja moyo wahamiaji wa ndani wa Usomali milioni 1.5 kwa kushindwa kuwasaidia kihali, katika kipindi ambapo mzozo wa kiutu unaendelea kudidimia na kuharibika zaidi nchini mwao." Alisema fungu kubwa la wahamiaji wa ndani, aliopata fursa ya kuwahoji, walimweleza kwamba waliyahama makazi yao kwa sababu ya mapigano ya kihorera yalioshtadi kwenye sehemu za Kati na maeneo ya Kusini katika Usomali, ikijumlisha mji mkuu wa Mogadishu. Alisema alishtushwa sana na viwango vya mapigano na uhasama uliosakama kwenye maeneo hayo ya Usomali ambao huathiri zaidi raia wa kawaida. Alithibitisha kwamba vitendo hivyo vilikiuka pakubwa haki za binadamu na sheria za kiutu za kimataifa, hususan kwenye mashambulio ya kihorera na upigaji mabomu kwenye makazi ya raia, makosa ambayo alisema yanafannywa na makundi yote yenye silaha, yanayohasimiana na ambayo hayajali kuadhibiwa na sheria. Walter Kaelin, Mjumbe wa KM juu ya Haki za Binadamu kwa Wahamiaji wa Ndani ni profesa wa sheria katika Chuo Kiku cha Bern, kilichopo Uswiss na ameshika wadhifa huo tangu mwaka 2004.