Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amehuzunishwa na kifo cha Brigedia Jenerali Ahmed Moinuddin, Makamu Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi Amani vya UM katika Sudan Kusini (UNMIS), ambaye aliuawa Alkhamisi, mnamo tarehe 22 Oktoba, baada ya shambulio liliotukia Islamabad, Pakistan wakati akiwa mapumzikoni. KM alitumia salamu za pole ukoo wa wafiwa, wafanyakazi wa UNMIS na kwa Serikali ya Pakistan, na alitumai watu walioendeleza shambulio, watashikwa haraka na kufikishwa mahakamani.

Shirika la UM la Kuisaidia Afghanistan (UNAMA) limeripoti maandalizi ya kufanyisha duru ya pili ya uchaguzi, yanayotayarishwa na Kamisheni ya Uchaguzi Huru (IEC) hivi sasa yamepamba moto nchini. Taarifa zinaeleza karatasi za kura zimeshahapishwa na kugawanywa kwenye vituo mbalimbali ndani ya nchi, na wakati huo huo vifaa vya kuendeshea uchaguzi navyo pia vimeshafungwa na vimeanza kuenezwa mnamo siku ya leo. Shirika la UNAMA limesema litachukua kila hadhari, kuhakikisha makosa yaliofanyika karibuni kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi, hayatorudiwa tena, na inatumai matokeo ya mwisho ya duru ya pili yataaminika na kukubaliwa na umma. Kuhakikisha hayo, KM amempeleka Afghanistan, Wolfgang Weisbrod-Weber, Mkurugenzi wa Kitengo cha Masuala ya Asia na Mashariki ya Kati katika Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM kuwa Naibu Mjumbe Maalumu kwa Masuala ya Kisiasa na atamsaidia Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghansitan, Kai Eide kusimamia vyema shughuli hizo. Weisbrod-Weber anatarajiwa kusalia Afghanistan kwa miezi mwili ijayo.

Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Uhalifu na Madawa ya Kulevya (UNODC) imewasilisha ripoti mpya yenye kubainisha athari haribifu, zilizovuka mipaka, zinazotokana na biashara haramu ya kasumba inayovunwa katika Afghanistan, taifa ambalo ndipo asilimia 92 ya kasumba ya ulimwengu inakadiriwa inaoteshwa na kuvunwa. Kwa mujibu wa ripoti ya UNODC, tani 900 za kasumba na tani 375 za heroini zinazosafirishwa kutoka Afghanistan, huathiri usalama na afya ya raia wa nchi za Balkan na katika yale maeneo ya Eurasia. Misafara ya biashara ya magendo ya madawa haya ya kulevya imeonekana kutawanyika vile vile kwenye mataifa ya Ulaya, Shirikisho la Urusi, Bara Hindi na pia katika Uchina. Ripoti ya UNODC inasema kasumba na heroini ni madawa ya kulevya yenye kumudu soko linalogharamiwa faida ya dola bilioni 65 kila mwaka, ambalo hukidhi mahitaji ya walevi wa madawa wanaokisiwa milioni 15, waliozagaa sehemu mbalimbali za dunia, na husababisha vifo 100,000 kila mwaka. Kadhalika waathirika wa madawa ya kasumba ndio miongoni mwa watu wanaoambukiza, kwa kasi, virusi vya ugonjwa wa UKIMWI kwa kiwango kisichowahi kushuhudiwa kihistoria, wakati fedha za faida zinazokusanywa kutoka biashara ya madawa ya kulevya ndizo zinazotiliwa shaka kutumiwa kupalilia vitendo vya ugaidi, na kuwapatia waasi wanaopinga serikali uwezo wa kununua silaha, na huwafadhilia pia makundi ya wahalifu wa mipangilio kuendeleza shughuli zao.

Edmund Mulet, KM Msaidizi juu ya Masuala ya Ulinzi wa Amani asubuhi aliripoti mbele ya Baraza la Usalama kuhusu shughuli za Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT). Alilenga zaidi ripoti yake juu ya hali ya usalama na mizozo ya kiutu iliopamba Chad mashariki na kaskazini-masharikiya Jamhuri ya Afrika ya Kati (JKK). Mulet alielezea namna huduma za polisi wa Chad zinavyoendelezwa kudhibiti usalama na utulivu kwenye kambi za wahamiaji na raia waliong'olewa makazi ndani ya nchi, waliotokea jimbo la Chad mashariki, shughuli ambazo zikidhibitiwa zitarahisisha huduma za kupeleka misaada ya kihali kwa waathirika hawo. Mulet alisisitiza operesheni za amani kieneo hazitofanikiwa kukamilisha malengo yake bila ya kuhakikisha kunapatikana maendeleo kwenye mazungumzo ya kusawazisha uhusiano baina ya Chad na Sudan, na bila ya kusuluhisha ile mizozo ya ndani iliyoyakabili mataifa haya mawili.