Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Taarifa za hapa na pale

Inga-Britt Ahlenius, Mkuu wa Idara ya UM ya Uchunguzi wa Makosa ya Udanganyifu na Ulaji Rushwa (OIOS) alikutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu na kuwazindua ya kwamba moja ya shuruti muhimu zilizowekwa kudhibiti bora utekelezaji wa shughuli za UM, miongoni mwa watumishi wa taasisi hii ya kimataifa ni kuhakikisha kunakuwepo uwazi kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, na pia uwajibikaji unaoridhisha, hususan ilivyokuwa wafanyakazi hawa wanaitumikia taasisi maalumu ya kimataifa yenye mazingira yasio ya kikawaida na ya aina pekee.

Utekelezaji wa MDGs Kijijini Mbola, Tanzania - Kilimo na Mazingira (Sehemu ya Pili)

Wasikilizaji, kwenye makala ya kwanza kuhusu huduma za wanavijiji wa Mbola, katika Mkoa wa Tabora, Tanzania za kuyakamilisha yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati, tulikupatieni dokezo na fafanuzi za Kaimu Naibu wa Kilimo na Mazingira, Eliezer N. Kagya ambaye anasimamia utekelezaji wa malengo hayo kwenye eneo husika. Alielezea namna wanavijiji wanavyoshiriki na kushirikishwa kwenye huduma za pamoja za kuondosha njaa kwenye eneo lao, kwa kutumia kilimo cha kisasa. Kwenye sehemu ya pili ya mazungumzo yetu, Kagya anazingatia matokeo ya aina gani yatakayojiri katika mwaka wa pili, kwenye sekta ya kilimo na mazingira, baada ya kuanzishwa mradi huu muhimu wa MDGs wenye lengo la kuondosha njaa na kuimarisha maendeleo ya kuchumi na jamii yatakayokuwana natija kwa wote.

Wahajiri wa Burundi kufadhiliwa makazi na UNHCR

Katika miaka mitano iliopita Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limefadhilia makazi wahamiaji 58,000 waliorejea Burundi kutoka matifa jirani na nchi za kigeni, msaada ambao uliowawezesha kujenga nyumba mpya na kupata matumaini ya maisha bora kwa siku zijazo.

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeupokea mwaka 2008 kwa hamu kuu ilivyokuwa Baraza Kuu lilipitisha azimio la kuufaya kuwa ni Mwaka wa Kuimarisha Usafi wa Kimataifa, baada ya mashirika ya UM kuthibitisha kwamba watu bilioni 2.6, sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu duniani, ikijumuisha watotomilioni 980, hunyimwa mazingira safi, hali ambayo huathiri sana afya na kuzusha maelfu ya vifo vinavyotokana na maradhi ya kuambukiza ambayo yanazuilika.

Utekelezaji wa MDGs Kijijini Mbola, Tanzania - Kilimo na Mazingira (Sehemu ya Kwanza)

Mnamo siku za nyuma tulianzisha vipindi maalumu kuhusu juhudi za kizalendo za wenyeji wa kijiji cha Mbola, katika Mkoa wa Tabora, Tanzania za kuharakisha utekelezaji wa ile miradi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ili kuikamilisha kwa wakati, kama ilivyopendekezwa na maafikiano ya jumuiya ya kimataifa katika mwaka 2000. Miradi hii ipo chini ya uongozi wa UM na hufadhiliwa na wahisani mbalimbali wa kutoka sehemu kadha wa kadha duniani.

UM kujumuika na Kenya kudhibiti utulivu na kuhudumia misaada ya kiutu nchini

KM wa UM Ban Ki-moon ameripotiwa kuingiwa na ‘wahka’ mkuu kuhusu ongezeko la hali ya wasiwasi, na mfumko wa vurugu liliotanda karibuni nchini Kenya, kufuatia uchaguzi uliomalizika wiki iliopita. Msemaji wa KM aliripoti kwamba Bw. Ban alishtushwa sana na taarifa alizopokea zilizothibitisha kwamba darzeni za raia waliunguzwa moto majuzi katika mji wa Eldoret walipokuwa ndani ya kanisa. Kadhalika KM aliarifiwa watu mia tatu ziada walishauawa baada ya kufumka ghasia na vurugu kufuatia kumalizika kwa uchaguzi wa taifa na kutangazwa matokeo ambayo hayakuwaridhisha baadhi ya vyama vilivyoshiriki kwenye upigaji kura huo.

2007 ulikuwa mwaka maututi hadi kwa watumishi wa UM duniani

Raisi wa Chama cha Watumishi wa UM, Stephen Kisambira aliripoti ya kuwa katika mwaka 2007 watumishi 42 wa UM waliuawa katika sehemu kadha za dunia wakati walipokuwa wanatekeleza wajibu wao wa kazi – idadi hiyo ilijumuisha vile vile wafanyakazi 17 waliouawa mnamo Disemba 11 na bomu la kujitolea mhanga katika mji wa Algiers, Algeria.

MONUC inasaidia kuandaa usalama DRC kwa mkutano wa upatanishi

Shirika la UM linalosimamia ulinzi wa amani katika JKK (MONUC) limearipoti kwamba linaisaidia Serikali ya taifa kuandaa mazingira ya usalama, kuambatana na mkutano utakaofanyika tarehe 6 Januari (2008) kwenye Jimbo la Goma, katika eneo la mashariki kuzingatia suluhu ya upatanishi na masuala ya kusukuma mbele shughuli za maendeleo katika eneo la mapigano.

UM kuanzisha tena duru mpya ya mazungumzo ya Sahara ya Magharibi

Duru nyengine ya mazungumzo ya kutafuta suluhu juu ya mzozo wa Sahara ya Magharibi inatarajiwa kukutana katika mji wa Manhasset, kwenye Jimbo la Long Island, New York kuanzia Januari 7 hadi 9, majadiliano ambayo yatasimamiwa na UM. Kikao cha safari hii kitafuata taratibu ya mikutano iliopita, kwa kulingana na hisia kuu ya wawakilishi wa Morocco na Chama cha Ukombozi cha Frente Polisario, ambao hupendelea mazungumzo yao yawe ya faragha.

Operesheni za UNAMID katika Darfur zahitajia msaada ziada kidharura, asisitiza KM

Ripoti ya KM juu ya suala la kupeleka vikosi mseto vya UNAMID vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika Darfur imeonya kwamba mafanikio yaliojiri kwa sasa ni haba sana, na hayataviwezesha vikosi hivyo vya kimataifa kuyatekeleza majukumu yake kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama. Hali hii, alitilia mkazo, itaunyima umma wa Darfur utulivu na amani ya wa muda mrefu inayotakikana kidharura katika eneo lao.