2007 ulikuwa mwaka maututi hadi kwa watumishi wa UM duniani

2007 ulikuwa mwaka maututi hadi kwa watumishi wa UM duniani

Raisi wa Chama cha Watumishi wa UM, Stephen Kisambira aliripoti ya kuwa katika mwaka 2007 watumishi 42 wa UM waliuawa katika sehemu kadha za dunia wakati walipokuwa wanatekeleza wajibu wao wa kazi – idadi hiyo ilijumuisha vile vile wafanyakazi 17 waliouawa mnamo Disemba 11 na bomu la kujitolea mhanga katika mji wa Algiers, Algeria.

Alisema kuwa wafanyakazi wa jumuiya ya kimataifa bado wanaendelea kuomboleza vifo vya wenziwao na raia wengine waliouawa katika 2007 kwenye mzingira ambayo kunahitajika kufanyike mapitio haraka juu ya taratibu za kuimarisha usalama wa watumishi wa UM kimataifa. Alisitiza ni muhimu kwa Idara ya Usalama ya UM, na vile vile Mataifa Wanachama, kuhakikisha watumishi wa UM, pote walipo, katika sehemu kadha wa kadha za dunia, kuwa wanapatiwa kinga maridhawa na hifadhi inayofaa wanapoendeleza kazi zao. Kadhalika, Raisi wa Chama cha Watumishi wa UM alipendekeza kwamba wale wanaoendeleza vitendo vya uhalifu dhidi ya wafanyakazi wa UM ni lazima washikwe na kufikishwa mahakamani na Mataifa Wanachama, nchi ambazo ndizo zenye dhamana kisheria ya kuimarisha usalama wa taifa. Alishtumu kuwa ni nadra kushtakiwa au kufikishwa mahakamani wale watu wanaoendeleza makosa dhidi ya wafanyakazi wa UM, hali ambayo alikhofu hushadidia miongoni wale wenye azma ya uovu dhana ya uhuru wa kutoadhibiwa pindi watahujumu au kuwashambulia watumishi wa UM.

Mashambulio ya makusudi dhidi ya watumishi wa UM bado yanaendelezwa hivi sasa katika pembe mbalimbali za dunia, kuanzia Sudan hadi Uganda, na katika maeneo ya Afghanistan hadi Nepal, mashambulio ambayo yameshaangamiza maisha ya wafanyakazi wa kiraia kadha wa kadha pamoja na wanajeshi walioshiriki katika kuyatekeleza maadili ya UM ulimwenguni, katika kukuza maendeleo ya uchumi na jamii na natija zake, kusawazisha usalama na amani na vile kuimarisha haki za binadamu kwa wote.