UM kujumuika na Kenya kudhibiti utulivu na kuhudumia misaada ya kiutu nchini
KM wa UM Ban Ki-moon ameripotiwa kuingiwa na ‘wahka’ mkuu kuhusu ongezeko la hali ya wasiwasi, na mfumko wa vurugu liliotanda karibuni nchini Kenya, kufuatia uchaguzi uliomalizika wiki iliopita. Msemaji wa KM aliripoti kwamba Bw. Ban alishtushwa sana na taarifa alizopokea zilizothibitisha kwamba darzeni za raia waliunguzwa moto majuzi katika mji wa Eldoret walipokuwa ndani ya kanisa. Kadhalika KM aliarifiwa watu mia tatu ziada walishauawa baada ya kufumka ghasia na vurugu kufuatia kumalizika kwa uchaguzi wa taifa na kutangazwa matokeo ambayo hayakuwaridhisha baadhi ya vyama vilivyoshiriki kwenye upigaji kura huo.
Timu ya UM Inayosimamia Udhibiti wa Maafa ya Dharura imekutana na wawakilishi wa Jumuiya ya Msalaba Mwekundu ya Kenya (KRCS) na kusailia nawo ushirikiano unaotakiwa kuhudumia vizuri zaidi mahitaji ya kiutu kwa waathiriwa wa hali ya vurugu. Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kuwa inakabiliwa hivi sasa na matatizo ya kugawa misaada ya kiutu na kihali kwa umma muhitaji nchini Kenya. Kwa mujibu wa Mkuu wa Ofisi ya UM Nairobi, Anna Tibaijuka baadhi ya barabara zinazotumiwa kusafirishia shehena za misaada hiyo kutoka Bandari ya Mombasa, njia hizo zimekutikana kuwa na matatizo, kwa sababu ya kuwepo vizingiti aina kwa aina, hali ambayo alisema Tibaijuka huchelewesha na kuathiri zile operesheni za ulinzi wa amani za UM katika mataifa jirani, ambazo hutegemea misaada hiyo kuhudumia umma muhitaji, mathalan zile huduma za kutuma misaada ya kihali katika Sudan Kusini, Uganda na baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC)zimekutikana kuzorota na kupwelewa kwa muda hivi sasa.
Mashirka ya UM yanayohusika na mfuko wa maendeleo ya watoto, UNICEF, huduma za wahamiaji, UNHCR, pamoja na miradi ya chakula WFP yamejumuika kuwasaidia kipamoja raia 100,000 katika eneo la kaskazini ya Mkoa wa Bonde la Ufa/Rift Valley, kupata nafaka na mafuta ya kupikia baada ya kung’olewa makwao kwa sababu ya kuzuka vurugu. Tuliarifiwa kwamba umma huu ulinaswa wenye eneo lenye utata, na hivi sasa umekosa chakula, maji, makazi na pia mafuta ya kupikia na madawa. WFP imeufadhilia umma huu misaada ya kihali kwa mwezi mzima.
Kwa ripoti ziada juu ya hali nchini Kenya, mtayarishaji vipindi AZR, alipata fursa ya kumhoji, kwa njia ya simu, mwanahabari aliopo Nairobi wa Redio China Kimataifa, Xie Yi.
Sikiliza ripoti kamili kwenye idhaa ya mtandao.