Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za UNAMID katika Darfur zahitajia msaada ziada kidharura, asisitiza KM

Operesheni za UNAMID katika Darfur zahitajia msaada ziada kidharura, asisitiza KM

Ripoti ya KM juu ya suala la kupeleka vikosi mseto vya UNAMID vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika Darfur imeonya kwamba mafanikio yaliojiri kwa sasa ni haba sana, na hayataviwezesha vikosi hivyo vya kimataifa kuyatekeleza majukumu yake kama ilivyodhaminiwa na Baraza la Usalama. Hali hii, alitilia mkazo, itaunyima umma wa Darfur utulivu na amani ya wa muda mrefu inayotakikana kidharura katika eneo lao.

Ripoti ilibainisha kwamba hadi hii leo UNAMID imekosa kufadhiliwa na Mataifa Wanachama ndege zinazohitajika kuimarisha ulinzi halisi wa amani katika Darfur. Kadhalika ripoti ya KM ilionya kwamba Serikali ya Sudan bado haina imani juu ya mchango wa vikosi vya UNAMID. Ripoti ya KM imesisitiza kwamba vikosi mseto vikikabidhiwa idhini ya kutumia nguvu za kijeshi kutunza amani vitachangia pakubwa katika kuimarisha usalama wa muda mrefu katika jimbo hilo la Sudan magharibi.