Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Ripoti ya UM inasema ukamataji wa kihorera Sudan umetanda nchi nzima

Ripoti ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu (OHCHR) kuhusu Sudan, iliowasilishwa rasmi leo Ijumaa mjini Geneva, inasema ukamataji wa kihorera wa raia na uwekaji kizuizini kwa watu wasio hatia, umezagaa katika sehemu nyingi za nchi, na ni vitendo ambavyo ripoti ilisema hufungamana na ukiukaji wa haki za binadamu unaoambatana na watu kuteswa na vitendo vyengine vya uoenevu na unyanyasaji.

FAO imemtunukia Raisi wa Malawi 'Nishani ya Agricola' kwa kujitegemea chakula

Raisi wa Malawi, Bingu wa Mutharika ametunukiwa \'Nishani ya Agricola\' na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) kwa mchango wake muhimu katika kurekibisha uchumi wa kilimo nchini. Malawi siku za nyuma lilikuwa ni taifa lilioshuhudia uhaba mkubwa wa chakula. Lakini baada ya kujulishwa sera mpya ya kilimo Malawi imefanikiwa kuzalisha kiwango cha kujitosheleza cha chakula.

Hapa na Pale

KM Mdogo juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, John Holmes, Ijumaa alikamilisha ziara ya siku mbili katika mji wa Juba, Sudan Kusini ambapo alikutana, kwa mazungumzo na wawakilishi wa serikali ya jimbo. Aliwaahidi UM utawasaidia kukabiliana na masuala muhimu ya kijamii, hususan yale yanayofungamana na sekta ya afya. Kabla ya hapo, Holmes alikutana na Raisi wa Sudan kusini, Salva Kiir na walishauriana taratibu zinazohitajika kuharakisha utekelezaji kamili wa mapatano ya jumla ya amani katika eneo la Sudan kusini.

Mapigano Rutshuri yalazimisha raia kuelekea Uganda kunusuru maisha

Shirika la UM la Kuhudumia Wahamiaji (UNHCR) limeripoti maelfu ya raia wa eneo la Kivu Kaskazini, katika JKK, wameonekana wakimiminikia kwenye mji wa Ishasha, mipakani Uganda, kujiepusha na mapigano na vurugu liliofumka katika siku za karibuni kwenye maeneo yao, yalioendelezwa na wapiganaji waliochukua silaha.

Twamkumbuka Mama Afrika - Miriam Makeba

Tarehe 27 Novemba 2008 ni Siku Kuu ya Kutoa Shukrani nchini Marekani, na kawaida ofisi zote hufungwa, ikijumuisha vile vile ofisi za Makao Makuu ya UM, ziliopo jiji la New York, Marekani. Hata hivyo, Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM imewajibika kutayarisha vipindi katika siku hii. Ilivyokuwa hii ni Siku Kuu ya Kutoa Shukrani, nasi pia tumeamua kuandaa makala maalumu, yenye kuwasilisha shukrani za jumuiya ya kimataifa, kwa ujumla, kuhusu mchango wa Balozi Mfadhili wa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO), Mama wa Afrika, msanii maarufu wa Afrika Kusini, marehemu Miriam Makeba katika kuhudumia kihali umma uliokabiliwa na matatizo ya ufukara na hali duni.~