Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Sauti za wanakijiji zasailia Mradi wa Milenia Mbola

Katika makala zilizopita tulieleza kwamba Mbola ilikuwa ni moja ya vijiji vya Milenia viliopo Afrika kusini mwa Sahara, vilivyochaguliwa na UM kufanywa vijiji vya mfano, ambavyo uzoefu wake ulitarajiwa kutumiwa kuongoza udhibiti bora wa miradi ya MDGs katika sehemu nyengine za taifa, na pia katika Afrika, kwa ujumla. Tangu Miradi ya Milenia ilipoanzishwa hadi leo huduma kadha wa kadha ziliekezwa Kijijini Mbola, Tanzania, hususan katika sekta za kilimo, elimu, miundo mbinu, afya na kadhalika, shughuli ambazo zilionekana kushika mizizi ya kutia moyo katika kukabiliana na matatizo ya umasikini, na katika huduma za kuwapatia wanakijiji wa Mbola natija za kuwanyanyua kimaisha.

Mashirika ya UM yanaendelea kuhudumia misaada ya kiutu Kenya

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) linaendeleza operesheni za kuwahamisha wahamiaji 6,500 wa Kenya waliokwama kwenye miji ya mipakani ya Busia na Malaba na kuwapeleka katika eneo la Mulanda, liliopo Uganda ya kati, ili kukidhia mahitaji yao ya kihali. Uhamisho huu ulilazimika ufanyike kwa sababu hali ya usalama, tuliarifiwa, ilizidi kuharibika nchini Kenya. ~

Taadhima ya Geneva inawakumbuka watumishi wa UM waliouawa Algiers

KM Ban Ki-moon, akijumuika na watumishi wa UM Geneva walifungua taadhima ya kuwaheshimu na kuwakumbuka wafanyakazi wenziwao 17 waliouawa na bomu la kujitolea mhanga Algeria mwezi uliopita, kwa kusimama kimya kwa dakika moja. Baada ya hapo KM alifunua rasmi ile bendera iliohifadhiwa ndani ya kioo kilichozungukwa na ubao wa matangazo, bendera ambayo ndio iliokuwa ikipeperuka kwenye ofisi za UM Algiers, na ilioraruliwa na kuchanwa na bomu la magaidi. KM alikabidhiwa bendera hiyo alipozuru ofisi za UM Algiers, siku chache baada ya tukio la magaidi kujiri.

Mwafaka wa amani Kivu unaungwa mkono na KM

KM wa UM amepongeza mwafaka uliopatikana majuzi kwenye Mkutano wa Amani, Usalama na Maendeleo kwa Kivu baada ya majadiliano ya karibu wiki mbili yaliofanyika kwenye mji wa Goma, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

WaSomali 130 ziada wafariki baada ya mashua yao kupinduka Yemen

Shirika la UM Linalohudumia Wahamiaji (UNHCR) limeripoti watu 130 ziada kutoka Usomali, wingi wao wakikimbia vurugu na fujo nchini mwao, walifariki mwisho wa wiki pale mashua yao ilipopinduka karibu na mwambao wa Yemen. Wahamiaji hawa walipigwa visu na magongo na kudhalilishwa na wale wafanyabiashara ya magendo ya kuvusha watu. Wingi ya wahamiaji walizama kwa sababu ya hali mbaya ya hewa iliosababisha mawimbi makali kupindua mashua yao.

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC azuru JAK

Luis Moreno-Ocampo, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimatifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) ameelekea Jamhuri ya Afrika ya Kati wiki hii kukutana na waathiriwa wa makosa karaha ya jinai ya vita yalioendelezwa nchini katika kipindi cha baina ya miaka ya 2002 na 2003. Kadhalika, atakapokuwepo mjini Bangui, JAK Moreno-Ocampo atakutana, kwa mashauriano, na wawakilishi wa jumuiya za kiraia, wenyeji husika na watumishi wa serikali. Ziara hii inafuatia tangazo la mwezi Mei 2007 ambapo Mwendesha Mashitaka aliripoti kwamba ataanzisha uchunguzi maalumu kuambatana madai ya kuwa jinai ya vita iliendelezwa dhidi ya utu, hususan yale makosa yanayoambatana na udhalilishaji wa kijinsia. Uchunguzi unafanyika kufuatia ombi liliopokewa na Mahakama kutoka Serikali ya JAK.

UM imeanzisha operesheni za kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko kusini ya Afrika

Ofisi ya UM inayohusika na Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kuongezeka kwa kiwango cha mara mbili idadi ya watu waliong’olewa makwao, kusini ya Afrika kutokana na mafuriko, katika kipindi cha wiki moja na kufikia 120,000 ziada. Hivi sasa Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) linasaidia kuhudumia misaada ya chakula Msumbiji, kwa kutumia helikopta, kwa waathirwa wa mafuriko 13,000 waliopatiwa makazi ya muda kwenye kambi za wahamiaji.

Hapa na pale

Shirika la Haki za Wafanyakazi wa Kimataifa (ILO) limetoa ripoti mpya yenye kuzingatia ‘Mwelekeo wa Ajira Duniani kwa 2008’ na kuonya kwamba kwa kulingana na takwimu za ILO watu milioni 5 watanyimwa ajira mwaka huu kwa sababu ya kutanda kwa misukosuko ya uchumi, ambayo huchochewa na machafuko kwenye soko la mikopo, pamoja na mfumko wa bei za mafuta katika soko la kimataifa.~