Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

KM amenasihi Mataifa kuharakisha Mkataba mpya kudhibiti bora uchafuzi wa hali ya hewa

Ijumapili KM Ban Ki-moon alihutubia Chuo Kikuu cha Kyoto, Ujapani kwenye mhadhara maalumu uliokusanyisha mamia ya wanafunzi, wasomi na wawakilishi wa sekta binafsi, pamoja na jumuiya za kiraia. Kwenye risala yake KM alikumbusha juu ya umuhimu wa kuyahamasisha Mataifa Wanachama kushirikiana, kidharura, kwenye zile kadhia zitakazosaidia kufikia mapatano mapya mnamo mwisho wa 2009, kama ilivyokubaliwa naMkutano wa Bali mwaka jana.

Dereva wa WFP Sudan Kusini ameuawa kwa kuvizia

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuuliwa dereva wao aliyeajiriwa kutoka Uganda, Muzamil Ramadan Sida mwenye umri wa miaka 28 ambaye alishambuliwa kwa kuvizia kwenye barabara ya Juba-Yei, Sudan kusini, baada ya kuteremsha shehena ya chakula kwenye ghala za WFP ziliopo Juba. Marehemu Sida ni dereva wa tano wa WFP kuuawa Sudan Kusini tangu mwanzo wa mwaka.

Mataifa masikini yapatiwa vipimo vya kisasa kutambua haraka TB sugu

Mashirika ya Kimataifa – ikijumuisha Shirika la Afya Duniani (WHO), Ushirikiano wa Kukomesha TB, UNITAID na Taasisi ya Kisasa ya Kubainisha Magonjwa Mapya – yametangaza kipimo kipya cha afya kutumiwa na mataifa masikini kutambua haraka zaidi ugonjwa wa kifua kikuu usiokubali tiba ya madawa ya mchanganyiko (yaani maradhi ya TB-MDR). Vipimo hivi vitatumiwa katika mataifa yanayoendelea 16, na vina uwezo wa kubainisha maradhi baada ya siku mbili tu, badala ya miezi mitatu, kama ilivyokuwa ikifanyika katika siku za nyuma.

Hapa na pale

Naibu KM wa UM Asha-Rose Migiro, kwenye risala alioitoa mbele ya wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika unaofanyika Sharm el-Sheikh, Misri kuanzia Ijumatatu amepongeza uamuzi wa kuingizwa mada inayohusu Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwenye ajenda yao - hususan lile saula la kuyapatia mataifa yanayoendelea usafi wa mastakimu na maji salama.

Mjadala wa kiwango cha juu wafunguliwa Makao Makuu na ECOSOC

Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) Ijumatatu ya tarehe 30 Juni limeanzisha majadiliano ya kiwango cha juu, kitachoendelea mpaka Alkhamisi Julai 03 ambapo wanachama wa kimataifa watazingatia masuala yanayoambatana na taratibu za kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa duniani, hususan katika nchi zinazoendelea, pamoja kujadilia tatizo la muongezeko wa bei za chakula na nishati kwenye soko za kimataifa na vile vizingiti vinavyokwamisha na kuzorotisha juhudi za kusarifisha maendeleo.

UNESCO kuanzisha muungano wa manispaa za kimataifa dhidi ya ubaguzi

Kwenye Warsha juu ya Haki za Binadamu unaofanyika Nantes, Ufaransa kulianzishwa na Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) jumuiya mpya ya muungano wa miji ya kimataifa, itakayoshirikisha manispaa za miji hiyo kwenye juhudi za kuandaa mitandao itakayoshughulikia juhudi za kuimarisha sera bora za kupiga vita kipamoja ubaguzi wa rangi na, kutunza tabia ya kuheshimiana, kwa kupendekeza kusuluhisha matatizo ya ubaguzi wa rangi kwa mazungmumzo badala ya adhabu, na kuhakikisha pia tamaduni tofauti au tabia anuwai zilizoselelea kwenye maeneo yao zinaruhusiwa kustawi bila ya pingamizi. ~

Mkataba wa Maziwa Makuu ya Afrika umepewa nguvu ya sheria

Mnamo tarehe 21 Juni 2008 mataifa manane kati ya 11, wanachama wa Taasisi ya Mkutano wa Kimataifa ya Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR) yaliridhia Mwafaka juu ya Usalama, Utulivu na Maendeleo katika Maziwa Makuu. Mataifa haya manane yalioridhia mkataba yalijumuisha Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kideomkrasi ya Kongo, Kenya, Jamhuri ya Kongo, Rwanda, Tanzania na Uganda.