Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hali ya Zimbabwe inasailiwa na BU

Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa, Lynn Pascoe Ijumanne alizungumzia hali Zimbabwe na wajumbe wa Baraza la Usalama. Baadaye alikutana na waandishi habari wa kimataifa ambao aliwabainishia taarifa isemayo kwamba UM upo tayari kusaidia kwa kila njia, kwa kupitia diplomasiya ya kikanda, ili kuharakisha suluhu ya kuridhisha kwa mzozo uliojiri Zimbabwe kufuatilia uchaguzi wa taifa.

ICC kutangaza hati rasmi ya kumshika kiongozi wa CNDP katika JKK

Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) imetoa hati rasmi ya kumkamata Bosco Ntaganda, kiongozi wa jeshi la mgambo la CNDP, baada ya kutuhumiwa, katika siku za nyuma, kuwalazimisha watoto wenye umri mdogo kujiunga na kundi lao na kushiriki kwenye mapigano, hasa katika wilaya ya utajiri mkubwa wa maadini ya Ituri, iliopo mashariki ya JKK; na alituhumiwa kurudia vitendo hivyo pia katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kwamba matokeo ya utafiti wa karibuni yamethibitisha asilimia 4 tu ya wahamiaji wa Iraq waliopo Syria, waliohajiri makwao kwa sababu ya vurugu wapo tayari kurejea nchini kwao. Asilimia 95 ya wahamiaji hawa waliihama Iraq kutokana na vitisho pamoja na ukosefu wa usalama kijumla.

Tathmini ya Mjumbe wa Tanzania kuhusu kikao cha UNCTAD XII

Taasisi ya UM juu ya Masuala ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ilikutana Accra, Ghana kwenye kikao cha 12 kuzingatia matatizo ya uchumi maendeleo katika mataifa masikini yanayochochewa na utandawazi wa kihorera kwenye soko la kimataifa. Mkutano ulihudhuriwa na wajumbe karibu 4,000 waliowakilisha serikali, sekta za biashara na vile vile wawakilishi wa jumuiya za kiraia.

CEB kuanzisha tume mpya kudhibiti mfumko wa bei za chakula duniani

Baada ya mashauriano siku mbili kwenye mji wa Bern, Uswiss baina ya KM Ban Ki-moon na viongozi wa lile bodi la wakurugenzi wa mashirika 27 ya UM (CEB), ambapo kulizingatiwa hatua za dharura za kukabiliana na mzozo wa kupanda kwa bei za chakula na nishati duniani, kuliafiwa na washiriki wa mashauriano hayo kuanzisha tume mpya maalumu ya kazi, itakayoshughulikia taratibu za kuudhibiti vyema mgogoro kwa kuwasaidia zaidi ule umma wa kimataifa ulio dhaifu.

FAO yataka kilimo kipatiwe kinga inayofaa katika nchi masikini

Jacques Diouf, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) amewasilisha ripoti muhimu iliopendekeza jumuiya ya kimataifa kujinyakulia fursa iliojitokeza hivi sasa ili kurasimu mipango mipya ya kujikinga na tatizo la chakula, tatizo ambalo huenda likaibuka tena katika siku zijazo. Alitaka misaada ya wahisani wa kimataifa iwekezwe zaidi kwenye sekta ya kilimo.

Wakariri wa haki za binadamu wana wasiwasi na hali Zimbabwe

Wakariri sita wa UM wanaohusika na haki za binadamu wamenakiliwa wakisema wana wasiwasi kuhusu kuporomoka kwa haki za binadamu na kuzuka kwa hali ya mtafaruku Zimbabwe kufuatia uchaguzi wa raisi na bunge uliofanyika March 29. Wataalamu hawa wanahusika na masuala ya mauaji ya kihorera, udhalilishaji wa wanawake, haki ya kupata makazi, haki ya uhuru wa kusema na hifadhi kinga dhidi ya mateso. Kwenye ripoti iliotolewa Geneva wataalamu hawo walibainisha kwamba wamepokea ripoti zenye kuaminika, zilizoelezea ya kuwa tangu uchaguzi ulipomalizika nchini Zimbabwe, vitendo vya vitisho na uonevu vilikithiri dhidi ya wale raia waliodhaniwa na kutuhumiwa kupigia kura, au kuunga mkono, chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) na wale waliohusika na Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC).