Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Fafanuzi za Mjumbe wa Tanzania juu ya kikao cha Kamisheni ya CSW

Kamisheni ya UM juu ya Haki za Wanawake, au Kamisheni ya CSW ilifungua rasmi kikao cha mwaka, cha 52, mnamo Ijumatatu ya tarehe 25 Februari, kuzingatia masuala kadha kuhusu hadhi ya wanawake duniani, kufuatia mapendekezo yaliotolewa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Beijing juu ya Wanawake, pamoja na yale maazimio ya kikao maalumu cha 23 cha Baraza Kuu la UM juu ya usawa wa kijinsiya na maendeleo ya wanawake kwa karne ya ishirini na moja.

UM yaunga mkono mwafaka wa Kenya kuunda Serikali ya Muungano

KM Ban Ki-moon Alkhamisi alitoa taarifa rasmi iliyoyapongeza “Maafikiano ya Ushirikiano wa Serikali ya Muungano” nchini Kenya, mapatano ambayo anaamini yatakapokamilishwa yatasaidia kuwasilisha suluhu ya kuridhisha kwa makundi yote yanayohusika na mzozo uliolivaa taifa lao katika wiki za karibuni.

Mchochezi wa mauaji Rwanda kumalizia kifungo Utaliana

Georges Omar Ruggu, mwandishi habari wa redio aliopatikana na hatia ya kuchochea mauaji ya halaiki dhidi ya raia wenye jadi ya KiTutsi nchini Rwanda katika 1994, na ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 12 na Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) alihamishwa Alkhamisi kwa ndege ya kijeshi kutoka kizuizini Arusha, Tanzania na kupelekwa kifungoni Utaliana kumaliza adhabu yake.

Maelfu ya raia CAR wakimbilia vichakani na kunyimwa mahitaji ya kimsingi

Toby Lanzer, Mshauri wa Umoja wa Mataifa juu ya Misaada ya Dharura kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kwenye mkutano na waandishi habari katika Makao Makuu ya UM alibainisha kwamba mashirika ya UM yanakabiliwa na tatizo gumu la kuhudumia misaada ya kiutu fungu kubwa la wahamiaji wa ndani ya nchi 200,000 waliokimbilia vichakani kaskazini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR). Wahamiaji hawa huwa wanakimbilia vichakani kuwakwepa majambazi wenye silaha ambao hushambulia raia kihorera.

KM wa UM ayapongeza maafikiano ya Serikali ya Muungano Kenya

KM Ban Ki-moon ameyapongeza, kwa moyo thabiti, yale “Maafikiano ya Ushirikiano wa Serikali ya Muungano” kwa Kenya, yaliyotangazwa Alkhamisi mjini Nairobi ambapo juhudi za kusuluhisha kipamoja mzozo uliolivaa taifa baada ya matokeo ya uchaguzi, zimezalisha mafanikio ya kuridhisha.

Mashirika ya UM yanuia kukomesha ukeketaji wa watoto wa kike duniani

Mashirika kumi ya Umoja wa Mataifa - yakijumuisha yale mashirika yanayoshughulikia huduma za kudhibiti UKIMWI (UNAIDS), kuimarisha miradi ya maendeleo (UNDP), maendeleo ya elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), Kamisheni ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (UNECA) na Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu Duniani, UNFPA; na vile vile yale yanayohusika na ulinzi wa haki za binadamu (OHCHR), huduma za wahamiaji (UNHCR), mfuko wa maendeleo ya watoto (UNICEF), mfuko wa maendeleo ya wanawake (UNIFEM) na pia afya ya kimataifa (WHO)- Ijumatano yametoa ripoti ya pamoja iliyoahidi kuchangisha kila juhudi ili kukomesha ile tabia haribifu ya kutahiri watoto wa kike, katika kipindi cha kizazi kimoja, pote duniani.