Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

BK linajadilia taratibu za kupunguza ajali za barabarani duniani

Ijumatatu Baraza Kuu la UM limeitisha kikao maalumu, cha wawakilishi wote, katika Makao Makuu ili kuzingatia usalama barabarani baada ya ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonya ya kuwa athari zinazotokana na ajali za barabarani zimeanzisha “mgogoro mpya wa hatari, kwa afya ya jamii” takriban kote duniani. Kwa mujibu wa ripoti ya WHO athariza za ajali za barabarani zinalingana na madhara yanayotokana na maradhi ya kifua kikuu, malaria na UKIMWI dhidi ya umma wa kimataifa.

Madereva wa huduma za maji Darfur waachiwa huru na majambazi

Shirika la UNICEF limeripoti faraja mwisho wa wiki iliopita baada ya kupokea taarifa kuhusu kuachiwa huru wale madereva wanne, watumishi wa Shirika la Maji la Sudan waliotekwa nyara wiki mbili nyuma katika jimbo la vurugu la Darfur Kaskazini. Madereva wanne hawa hivi sasa wamesharejeshwa kuungana na aila zao. Lakini vile vifaa vya thamani vilivyobebwa kwenye magari ya madereva wa Shirika la Maji la Sudan havijapatikana tena na vimepokonywa na maharamia. Huduma shirika za za maji zinazotekelezwa na Shirika la Maji la Sudan pamoja na UNICEF katika Darfur Kaskazini huwasaidia makumi elfu ya raia wa eneo hilo kupata maji safi ya kunywa na matumizi ya nyumba.

Balozi wa Tanzania katika UM afafanua maana ya Siku ya Kuwakumbuka Waathiriwa wa Utumwa Duniani

Tarehe 25 Machi iliadhimishwa kwenye Makao Makuu na UM, kwa mara ya kwanza kihistoria, kuwa ni Siku ya Kumbukumbu za Kimataifa kwa Waathiriwa wa Utumwa na Biashara ya Utumwa katika Ngambo ya Bahari ya Atlantiki. Kwenye taadhima za siku hiyo kulifanyika warsha maalumu kuzingatia \'athari na makovu ya utumwa kwa binadamu\'; na vile vile kuliandaliwa maonyesho na tafrija aina kwa ina za kukumbusha umma na kuwaelimisha kuhusu msiba na madhara yalioletwa na utumwa.

UNHCR imefanikiwa kurejesha Sudan Kusini wahamiaji 100,000

Wiki hii Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti tukio la kihistoria ambapo operesheni za kurejesha wahamiaji wa Sudan wa Kusini zilirajisiwa kukamilisha jumla ya wahamiaji 100,000 waliofanikiwa kurejeshwa makwao, kwa khiyari, kutoka mataifa jirani ya Uganda, Kenya na Ethiopia. Wahamiaji hawa walikuwa wakiishi kwa muda mrefu kwenye nchi jirani kufuatia mapigano yaliozuka kwenye maeneo yao katika siku za nyuma.

Maendeleo ya karibuni Burundi kuisumbua Kamisheni ya Ujenzi wa Amani

Kamisheni ya UM Kufuatilia Ujenzi wa Amani kwenye yale mataifa yaliobuka kutoka mazingira ya vurugu na mapigano, imewasilisha ripoti mpya kuhusu hali nchini Burundi ambapo ilisema jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi juu ya uamuzi wa lile kundi la Palipehetu-FNL wa kujitoa na kutoshiriki kwenye Utaratibu wa Jumla wa Pamoja wa Kusimamia na Kuthibitisha Kusitishwa kwa Mapigano, mradi ambao ulianzishwa 2006.

Baraza la Haki za Binadamu limesihi Mataifa kutotumia ubaguzi wa rangi kupiga vita ugaidi

Alkhamisi wajumbe 47 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu walipitisha Geneva maazimio sita muhimu kuhusu taratibu za kuimarisha haki za kimsingi za binadamu duniani. Miongoni mwa maazimio hayo muhimu lilikuwemo pendekezo maalumu liliopitishwa, kwa kauli moja, na bila ya kura, ambalo lilionya Mataifa Wanachama yote dhidi ya tabia ya kutafautisha kisheria watu, kwa sababu ya jadi, asili, dini au kabila, kwa kisingizio ya kupiga vita ugaidi.

Matokeo ya Malengo ya Milenia Duniani ni ya mchanganyiko, asema NKM Migiro

Naibu KM (NKM) wa UM, Asha-Rose Migiro Alkhamisi alihutubia Mkutano wa Kuzingatia Hali ya Dunia kwa Sasa uliofanyika Chuo Kikuu cha Columbia, mjini New York ambapo alidhihirisha kwamba kumepatikana matokeo ya mchanganyiko kwenye zile juhudi za kimataifa za kukamilisha, kwa wakati, Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yaliokusudiwa kupunguza umasikini kwa nusu katika nchi zinazoendelea itakapofika 2015.