Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwe makini maendeleo yasisababishe zahma- Lajčák

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák akimwagilia maji kwenye mti aliopanda kwenye msitu wa Karura ulioko mjini Nairobi, nchini Kenya. (Picha:PGA-Twitter)

Tuwe makini maendeleo yasisababishe zahma- Lajčák

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák aliyeko ziarani nchini Kenya, amesema maendeleo hayapaswi kusababisha uharibifu wa mazingira.

Amesema hayo jijini Nairobi, wakati akifunga mjadala kuhusu sayansi, sera na biashara, mjadala uliofanyika kwa siku mbili.

Bwana Lajčák amesema hayo akizingatia kuwa harakati za sasa za maendeleo duniani zimekumbwa na vikwazo kama vile majanga ya asili na yale yanayosabishwa na binadamu ambavyo vyote vinatishia siyo tu uwepo wa binadamu bali pia sayari dunia.

Hata hivyo amesema tayari sayansi ilitabiri uharibifu wa mazingira, huku nao ujuzi wa asili ukionya harakati za kupuuza mazingira.

Kwa mantiki hiyo amependekeza mambo matatu, mosi sera zinazotungwa na serikali zitokanane na taarifa za kisayansi.

Pili ametaka uzingatiaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris akisema nyaraka hizo zitakuwa  hazina maana kama zitapuuzwa.

image
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák akihutubia kwenye kikao mjini Nairobi, Kenya leo disemba 3, 2017. (Picha:PGA Twitter)
Pendekezo la tatu la Bwana Lajčák  ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kuweka mizania ya sera, sayansi na biashara. Hivyo amesema wakiwemo vijana na wadau wengine ili kila mtu atekeleze wajibu huo.

Rais huyo wa Baraza Kuu ametumia fursa hiyo kutangaza kuwa tarehe 30 mwezi Mei mwakani ataitisha tukio maalum linalohusisha vijana na elimu kwa lengo la kusongesha Umoja wa Mataifa karibu na vijana.

Mapema Bwana Lajčák alishiriki katika tukio la kando kuhusu umuhimu wa misitu ambapo alisema kuwa rasilimali hiyo ni muhimu na pia chanzo muhimu cha uhai.

Na kwa mantiki hiyo akaelezea furaha yake kwa kuweza kushiriki kupanda mti katika msitu wa Karura ulioko mjini Nairobi.

Amekumbusha kuwa misitu ina kazi kubwa pia ya kufyonza hewa ya ukaa ambayo ni  moja ya vyanzo vya mabadiliko ya tabianchi.