Wapatieni makazi ya kudumu wahamiaji 1,300 Libya- UNHCR
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limetoa wito kwa serikali zote duniani kutoa hifadhi wa kudumu kwa wahamiaji 1300 walioko katika mzingira magumu nchini Libya.
Volker Turk ambaye Kamisha msaidizi wa UNHCR kwa ajili ya ulinzi kwa wakimbizi amesema hali ya wahamiaji hao nchini Libya ni ya kusikitisha sana, hivyo wahisani wanahitajika kusaidia kuwapatia makazi ya kudumu.
Turk amesema kutokana na hali ya sintofahamu, UNHCR imechukua hatua ya kuhamisha familia 25 ya wahamiaji kutoka Eritrea, Ethiopia na Sudani kuelekea makazi ya mpito nchini Niger wakati wanaendelea kufuatilia suala la makazi ya kudumu .
Aidha Turk anaendelea kukemea vitendo vya kikatili vinavyofanyiwa wahamiaji nchini Libya huku akitoa wito kwa mamlaka ya Libya kuchukua hatua ya kisheria kwa yeyote anayejihusisha na vitendo vya unyanyasaji kwa wahamiaji katika maeneo mbalimbali chini Libya.