Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya na Burundi miongoni mwa nchi 37 zinazohitaji msaada wa chakula- FAO

Familia huko Garissa nchini Kenya wanatembea kuelekea sehemu ambayo wataweza kupata maji. Picha: UNICEFKenya/2017/Serem

Kenya na Burundi miongoni mwa nchi 37 zinazohitaji msaada wa chakula- FAO

Mavuno mengi ya nafaka ulimwenguni bado hayajaweza kusaidia kuondokana na ukosefu wa chakula katika nchi 37 duniani, 29 kati ya hizo zikiwepo barani Afrika.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la chakula na kilimo duniani, FAO iliyotolewa leo huko Roma, Italia ikiangazia matarajio ya mazao na hali ya chakula.

Ripoti imesema kuwa mavuno ya nafaka yako juu lakini ukame, mafuriko na mizozo isiyoisha vimesababisha nchi kama vile Somalia, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Kenya kuhitaji msaada wa chakula kutoka nje.

Mathalani kutokana na mapigano, shughuli za kilimo zimekoma nchini CAR na hata kama chakula kinapatikana, ukosefu wa usalama unakwamisha usambazaji wa chakula kwa wahitaji.

Nchini Kenya nako ukosefu wa mvua umekwamisha kilimo na ufugaji na watu wapatao milioni 2.6 hawana uhakika wa kupata chakula.

Maeneo mengine ambako hali ya chakula si shwari ni Bangladesh, Yemen, Syria na Malawi.