Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kura kuhusu Yerusalem yaghubika mkutano wa Miroslav

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Picha: UM/Evan Schneider

Kura kuhusu Yerusalem yaghubika mkutano wa Miroslav

Kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika kesho ili kujadili na kupigia kura azimio la kupinga uamuzi wa Marekani kutambua Yerusalem kama mji mkuu wa Israel, kimeghubika mkutano wa mwisho wa mwaka wa Rais wa Baraza hilo na waandishi wa habari hii leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani.

Mathalani waandishi wa habari walimuuliza Miroslav Lajčák iwapo kikao hicho hakitaibua kauli za chuki na uhasama kufuatia ghasia zilizoibuka baada ya kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hoja hiyo siku mbili zilizopita..

(Sauti ya Miroslav Lajčák)

“Natumaini na ninatarajia kuwa tutahifadhi hadhi ya Baraza Kuu na pia ya Umoja wa Mataifa. Naamini kuwa tunaweza kujadili hoja yoyote hata kama ni nyeti kwa misingi ya kuwajibika na kuheshimiana na kwa heshima ya shirika.”

Bwana Lajčák akaulizwa je azimio hilo litakuwa na athari gani?

(Sauti ya Miroslav Lajčák)

“Siko hapa kubashiri kuhusu kikao cha kesho. Mimi nitakuwa mwenyekiti wa kikao hicho nilichoitisha kwa mujibu wa kanuni zilizoanzisha Baraza Kuu. Jukumu langu hapa ni kulinda kanuni hizo, katiba na hadhi ya Baraza Kuu.”

Kikao cha kesho kimeitishwa dharura baada ya azimio lililowasilishwa na Misri mbele ya Baraza la Usalama la kulaani hatua ya Marekani kutambua Yerusalem, kugonga mwamba.