Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Waasi wa CNDP wakumbushwa na UNHCR kuhishimu haki halali za wahamaji waliopo Rutshuru katika JKK

Shirika la UNHCR limetoa mwito maalumu unaowataka waasi wafuasi wa kundi la CNDP la Laurent Nkunda, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) kuhakikisha raia waliomo kwenye maeneo wanayoyadhibiti wanapatiwa hifadhi na ulinzi, kwa kufuatana na kanuni za kiutu za kimataifa, hususan wale raia wahamiaji wa ndani ya nchi 10,000 waliopo karibu na kambi ya vikosi vya ulinzi amani vya UM vya MONUC, katika Rutshuru, [kilomita 80 kutoka mji wa Goma].

Ofisa wa WHO anasema hali ya afya Zimbabwe inashtusha

UM umeripoti idadi ya vifo Zimbabwe sasa hivi kutokana na maradhi ya kipindupindu imezidi 1,100. Dktr Dominique Legros, Ofisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ambaye alikuwa Zimbabwe karibuni aliwaambia waandishi habari Geneva Ijumaa kwamba huduma za afya zimeharibika sana nchini na mahospitali yanafanana na mahame ya vizuka na pepo, kwa sababu wahudumia afya hawalipwi na wameamua kutokwenda kazini. Dktr Legros anatupatia maelezo zaidi:

'Utambuzi wa mfumo wa ujinsiya utegemee sera za kitaifa na usishurutishwe kimataifa', nchi wanachama zakumbushana

Kwenye majadiliano yaliofanyika Alkhamisi katika ukumbi wa Halmashauri ya Baraza Kuu juu ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) kuzingatia “haki za binadamu, utambulishi wa kijinsiya na ujinsiya”, kulipigwa kura, isiyokuwa na masharti ya kiseheria, ambapo Mataifa Wanachama 66 yalitoa mwito wa kutaka kufutwa kwenye sheria zile amri zinazotafsiri vitendo vya ubasha, usagaji na usenge kuwa ni uhalifu. Kikao hiki kilidhaminiwa na balozi za mataifa ya Argentina, Brazil, Croatia, Gabon na pia Norway, Ufaransa na Uholanzi

Hapa na Pale

Timu ya wataalamu wa UM wanaotathminia mahitaji kwenye maafa imewasili wiki hii Port Moresby, Papua New Guinea kujaribu kuchanganua mahitaji ya kihali kwa watu 32,000 ambao, mnamo tarehe 08 Disemba 2008, waliharibiwa makazi baada ya kina cha maji kufurika kwenye kisiwa chao. Ofisi ya UM juu ya Uratibu wa Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kwamba wataalamu hao wa UM, wakiwakilisha mashirika mbalimbali, wanatazamiwa kusalia kwenye visiwa vya Papua New Guinea kuendeleza uchunguzi wao baina ya siku saba hadi kumi.

Changanuo ya FAO juu ya hali ya chakula na mavuno 2008

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) Alkhamisi limechapisha ripoti yenye kuthibitisha katika 2008 ulimwengu ulishuhudia idadi kubwa ya mavuno ya mazao ya nafaka, jumla iliovunja rikodi, na yenye matarajio ya kukidhi mahitaji kwa miaka ya 2008/2009, na kuweka [kando] akiba wastani ya chakula duniani kwa matumizi ya baadaye.

Hapa na Pale

Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) Alkhamisi imemhukumu Protais Zigiranyirazo kifungo cha miaka 20, kwa makosa dhidi ya ubinadamu na mauaji ya halaiki katika Rwanda mnamo 1994. Zigiranyirazo, shemeji wa marehemu Raisi Habyarimana, alituhumiwa kushiriki kwenye vitendo vya uhalifu wa pamoja, kwa lengo la kuendeleza mauaji ya halaiki na kuangamiza Watutsi wa Bonde la Kesho, na vile vile kwa kusaidia kuhamasisha mauaji ya halaiki kwenye vizuizi vya barabarani katika eneo la Kiyovu. Lakini Mahakama ilimtoa hatiani Zigiranyirazo kwa tuhumu za kuhusika na njama za kurahisisha mashambulio dhidi ya Watutsi, na kumtoa dhamana ya madai ya kuwa alifanya makosa ya jinai kwa ushirikiano na kundi la Interahamwe, kundi la wanamgambo wa Kihutu wenye siasa kali.