Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Timu ya wataalamu wa UM wanaotathminia mahitaji kwenye maafa imewasili wiki hii Port Moresby, Papua New Guinea kujaribu kuchanganua mahitaji ya kihali kwa watu 32,000 ambao, mnamo tarehe 08 Disemba 2008, waliharibiwa makazi baada ya kina cha maji kufurika kwenye kisiwa chao. Ofisi ya UM juu ya Uratibu wa Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kwamba wataalamu hao wa UM, wakiwakilisha mashirika mbalimbali, wanatazamiwa kusalia kwenye visiwa vya Papua New Guinea kuendeleza uchunguzi wao baina ya siku saba hadi kumi.

Ijumaa Baraza la Usalama limepitisha, kwa kauli moja, azimio liliodhamiria kukuza uwezo wa kikazi kwa Tume Inayosimamia Utekelezaji wa Vikwazo vya Silaha dhidi ya Usomali. Kwa mujubu wa azimio utaratibu unaodhibiti vyema vikwazo ndio wenye matumaini ya kurudisha utulivu na amani katika Usomali, eneo ambalo tangu 1991 limenyimwa fursa ya kuwa na serikali kuu ya kuendesha shughuli za nchi. Kwa hivyo, Baraza la Usalama limeamua kuongeza, kwa mwaka mmoja, shughuli za Tume juu ya Vikwazo vya Silaha dhidi ya Usomali, vikwazo ambavyo vilipitishwa na UM miaka 16 iliopita. Azimio limesisitiza ya kuwa hali katika Usomali inahatarisha amani ya kimataifa na utulivu wa eneo la Pembe ya Afrika, na kuamrisha Mataifa yote, hususan yale jirani na Usomali, kuhishimu vikwazo vya kimataifa, na kuchukua kila hatua kuhakikisha wanaotengua kanuni hizo wanafikishwa mahakamani.

Alain LeRoy, KM Mdogo juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM aliwasilisha mbele ya Baraza la Usalama taarifa yake juu ya hali karibuni katika eneo la mtafaruku na vurugu la Sudan magharibi la Darfur. Aliwaambia wajumbe wa Mataifa 15 yanayowakilishwa katika Baraza la Usalama kwamba vitendo vya kutumia mabavu katika Darfur vinaendelea bila kupungua, wakati mgogoro wa umwagaji damu kineoe unaingia mwaka wa sita. Miezi ya karibuni, alisisitiza LeRoy, UM ulishuhudia muongezeko mkubwa wa mashambulio dhidi ya wahudumia misaada ya kiutu katika Darfur, na vile vile dhidi ya walinzi wa amani wa vikosi vya UNAMID, ambavyo huwaklilisha majeshi mseto ya UM na Umoja wa Afrika. Kadhalika Mkuu wa Idara ya UM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani alibainisha watu waliong’olewa makazi Darfur, hivi sasa wamepatiwa hifadhi kwenye mastakimu dhaifu, ya muda, na wakati huo huo kueleza kupamba kwa mapigano ya kikabila na mapambano kati ya Serikali na wanajeshi wa mgambo, hali ambayo alihadharisha inachangisha na kupalilia zaidi fujo na vurugu Darfur.