Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano

Washiriki wa #CPD50 wapaza sauti maswala ya afya

Mkutano wa 50 wa  kamisheni ya idadi ya watu na maendeleo wa Umoja wa Mataifa #CPD50 umeingia siku ya nne ambapo washiriki kutoka nchi mbali mbali wamekusanyika kwa ajili ya kujadili maswala ya ukuaji wa idadi ya watu na mienendo pamoja na ujumuishwaji wa ukuaji huo katika mikakati ya maendeleo.

Katika maswala ya idadi ya watu kunaibuka pia afya ya uzazi na usawa wa kijinsia na hizo ni baadhi ya mada ambazo zimejadiliwa hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Basi ungana na Grace Kaneiya katika Makala hii na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.

Wanasesere wabeba historia ya wakimbizi kutoka Syria

Mapigano nchini Syria yameingia mwaka wa saba sasa, nuru ya kumalizika ikiwa haionekani. Wananchi wamekimbilia nchi jirani kusaka hifadhi wengine wamesalia nchini humo, huduma za msingi za kiutu zikikumbwa na mkwamo. Kwa wale waliosaka hifadhi ikiwemo nchini Lebanon, wanasaka mbinu za kuelezea madhila yao na hata ndoto zao wakati huu ambapo milio ya risasi na makombora inalia kila uchao. Je wanafanya kitu gani ambacho pia kinawaingizia kipato ugenini huku wakisaidia wakimbizi wenzao? Ungana basi na Assumpta Massoi kwenye makala hii.

Upatikanaji wa tiba dhidi ya kifua kikuu Tanzania

Moja ya malengo ya maendeleo endelevu ni kutokomeza janga la ugonjwa wa kifua kikuu au TB ifikapo mwaka 2030. Mkakati wa shirika la afya ulimwenguni, WHO wa kutokomeza TB unataka kupunguzwa kwa vifo vitokanayvo na ugonjwa huo kwa asilimia 90 na kupunguza visa vyake kwa asilimia 80. Malengo haya yatafikiwa iwapo tiba sahihi itapatikana kwa wakati sahihi kwa wagonjwa, pia mikakati ya kuzuia kueneza ugonjwa. Je nchini Tanzania upatikanaji wa huduma ya TB ukoje?

Umuhimu wa vyandarua katika kujikinga na malaria

Shirika la afya ulimwenguni, WHO kwenye ripoti yake ya mwaka 2016 iliyotolewa Desemba 13 kwa ajili ya malaria linaeleza kuwa watoto na wanawake wajawazito barani Afrika wana fursa ya kudhibiti Malaria.  Miongoni mwa mbinu za kukabiliana na ugonjwa huo hatari ni kutumia vyandaraua. Nchini Tanzania juhudi za kukabiliana na malaria kupitia mkakati wa kitaifa zinaendelea ili kuutokomeza.

Katika makala hii, Bwana Mabamba Mpela Junior, wa redio washirika Umoja redio ya Kigoma Tanzania anamulika umuhimu wa vyandarua katika kujikinga na malaria nchini humo, ungana naye..

Wanyamapori wainua vipato na elimu Uganda.

Takwimu  za benki ya dunia za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa Sekta ya utalii nchini Uganda huiliingizia taifa asilimia 3.7 ya pato la ndani  . Uwepo wa mbuga za wanyama ni sehemu ya mchango wa pato hilo.

Mbuga hizo za wanyama zimekuwa na manufaa kwa wakazi nchini humo hususani wale waishio jirani na mbuga za wanyama. Manufaa hayo sio tu ya kipato bali pia kielimu ambapo wanafunzi katika maeneo hayo wanasema wanyama huwasaidia katika masomo.

Biashara ya utumwa yaacha alama Amerika Kusini

Tarehe 25 Machi kila mwaka kunaadhimishwa  siku ya kimataifa ya kumbukizi ya wahanga wa utumwa na biashara ya utumwa. Mwaka huu kumbukizi hizo zinaangazia jinsi wahanga wa biashara ya utumwa wanavyoendelea kuchangia na kuleta mabadiliko katika jamii duniani kote.  Katika makala hii Amina Hassan anaangazia jinsi biashara hiyo inavyoendelea kuvutia utamaduni katika jamii fulani Amerika ya Kusini.  Ungana naye

Mikopo yalenga kukwamua wanawake kiuchumi nchini Tanzania

Umaskini uliokithiri umepunguzwa zaidi ya maradufu katika nchi mbali mbali duniani tangu mwaka 1990. Wakati hii ikiwa ni hatua kubwa, bado yaelezwa kuwa mtu mmoja kati ya watano katika nchi zinazoendelea anaishi kwa kutumia chini ya dola moja na senti ishirini na tano kila siku na kuna mamilioni wengi ambao wana kipato kidogo zaidi tu ya kiwango hicho huku kukiwa na hatari ya watu kutumbukia katika dimbwi la umaskini.

Calypso yarithishwa kizazi hadi kizazi

Fasihi simulizi inaenezwa kutoka jamii moja hadi nyingine kwa njia mbali mbali ikiwemo matamasha. Miongoni mwa fasihi hizo ni utamaduni wa mtindo wa Calypso ambao huweka bayana historia ya jamii hususan ya nchi za Caribea.

Mtindo huu umeorodheshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO kama turathi za tamaduni zisizogusika za kibinadamu. Je nini hufanyika na hurithishwa namna gani? Ungana basi na Assumpta Massoi anayekupeleka huko Venezuela.

Wanawake wadhihirisha kuwa kazi ni kazi bora iwe halali

Mkutano wa 61 wa kamisheni ya hali  ya wanawake duniani, CSW61 ukiendelea kushika kasi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, nchini Tanzania wanawake wa mashinani wameanza kuonyesha bayana kuwa zama za kazi fulani ni za wanaume na nyingine ni za kike zimepitwa na wakati. Mathalani udereva wa magari ya abiria, uwakala wa wasafiri na nyinginezo nyingi. Je ni wapi huko? Paulina Mpiwa wa radio washirika Sengerema FM mkoani Mwanza amevinjari wilayani Sengerema.